KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeshindwa kujadili Deni
la Taifa na kuagiza kukutana na idara na taasisi sita, zinazohusika na
deni hilo.
Uamuzi
huo wa kamati ulifikiwa jana jijini Dar es Salaam wakati Kamati hiyo
ilipokutana na Wizara ya Fedha na Mipango, kujadili taarifa yao ya fedha
kwa mafungu tofauti.
Idara
na taasisi hizo ni Idara ya fedha za Nje, Idara ya Sera na Uchambuzi,
Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume ya
Mipango na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Akitoa
uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hillary, alisema
kamati hiyo haiwezi kujadili na Wizara ya Fedha, Deni la Taifa kama
ambavyo linaonesha katika kifungu kinachotakiwa kujadiliwa, kwa sababu,
wizara hiyo inaelekezwa kulipa tu.
“Tumeshindwa
kujadili Deni la Taifa na Wizara ya Fedha leo (jana), hawa wanapokea
maelezo ya kulipa tu, hawajui vyanzo vya madeni vimetokea wapi, sasa
tumeona tukutane kwanza na hizo idara na taasisi husika watuambie chanzo
na deni likoje,” alisema Hillary.
Alisema
idara hizo na taasisi zitaandikiwa barua ili wanapokutana na kamati
waje na maelezo yanayojitosheleza kuhusu deni hilo la taifa ili baada ya
kamati kuhoji na kuelewa, ndipo wakutane na wizara kuendelea na
mjadala.
Awali
wakati kamati hiyo ikijadili na wizara hiyo kuhusu ripoti yake ya
hesabu, wajumbe wa kamati hiyo walihoji kero ya wastaafu ya
kucheleweshewa malipo yao ya pensheni na mirathi.
Akichangia
mjadala huo, Mjumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Munde
Abdallah alihoji ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu kutoka Hazina na
kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Alisema
wastaafu wengi wakiwemo walimu wamekuwa wakisumbuliwa kupeleka barua za
ajira na hati za malipo ya mshahara kwa mwezi, jambo ambalo ni kero na
wakati mwingine wastaafu hao huwa wamepoteza kumbukumbu hizo kwa kuwa ni
za muda mrefu, jambo ambalo linawafanya wacheleweshewe stahiki zao.
Akijibu
hoja hizo na nyingine, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Francis Mwakapalila
aliomba radhi kwa wastaafu wote ambao wamekuwa wakisumbuliwa kupeleka
vielelezo hivyo na kusisitiza kwamba ni wajibu wa mwajiri kuwa na
vielelezo vya watumishi wake.
Mwakapalila
alisema hivi sasa utaratibu unaotumika kwa wastaafu wanaolipwa na
Hazina hauna usumbufu na kwamba mirathi na pensheni zinazolipwa na
Hazina huenda moja kwa moja kwenye akaunti za wahusika na hazipitii tena
Hazina Ndogo.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment