Tanzania imesema
inasubiri ripoti ambayo imewataja wanajeshi wa Tanzania kuwa miongoni
mwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaotuhumiwa
kuhusika katika visa vya unyanyasaji wa kingono.
Jeshi la Tanzania
linakabiliwa na tuhuma tatu za unyanyasaji wa kingono kati ya tuhuma 69
zilizoorodheshwa kwenye ripoti hiyo inayoangazia tuhuma zilizotolewa
mwaka 2015.Visa hivyo viliongezeka kutoka kwa visa 52 mwaka 2014 na 66 mwaka uliotangulia.
Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Dkt Hussein Mwinyi, amenukuliwa na gazeti la Daily News mjini Dar es Salaam akisema nchi hiyo bado haijapokea ripoti hiyo.
“Tutakuwa katika nafasi nzuri ya kutangaza msimamo wa taifa letu tukipokea ripoti hiyo na kuitathmini,” waziri huyo alinukuliwa na gazeti hilo.
Tanzania ilikuwa na wanajeshi 2,158 na polisi 74 katika vikosi vya Umoja wa Mataifa mwaka jana.
Tanzania imeorodheshwa miongoni mwa nchi ambazo zinaongoza kwa visa vya unyanyasaji, ikiwa na visa vitatu.
Visa viwili vinahusu kushiriki ngono na watoto na kingine kinahusu uhusiano wa kimapenzi wa kumtumia vibaya mhusika.
Nchi hizo nyingine ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (inayoongoza ikiwa na visa saba), Morocco, Afrika Kusini, Cameroon, Congo na Gabon. Rwanda inaongoza kwa tuhuma dhidi ya polisi wake wanaohusika katika vikosi vya Umoja wa Mataifa ikiwa na maafisa watatu.
Chanzo BBC Swahili.
0 comments:
Post a Comment