RAIS wa Vietnam, Truong Tan Sang
RAIS wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Truong Tan Sang, ameanza
ziara ya siku tatu nchini, ambapo pamoja na masuala mengine, atasaini
mkataba wa masuala ya Kodi na mwenyeji wake Rais John Magufuli.
Mkataba huo unalenga kuchochea biashara kati ya Vietnam na Tanzania
kwa kuwa utatoa fursa kwa wafanyabiashara wa pande zote kutotozwa kodi
mara mbili katika biashara na uwekezaji watakaoufanya.
Rais huyo anatarajiwa kupigiwa mizinga 21 leo, ikiwa ni pamoja na
kukagua gwaride rasmi, ambapo baadaye atatambulishwa kwa viogozi
mbalimbali wa Serikali, kabla ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa Dar es Salaam kuhusu ujio wa Rais
huyo wa Vietnam, baada ya viongozi hao kutia saini mkataba huo, mgeni
huyo na ujumbe wake atakwenda kwenye ofisi ndogo ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), iliyopo katika Mtaa wa Lumumba jijini humo kukutana na Mwenyekiti
wa chama hicho, ambaye ni Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Rais huyo wa Vietnam ambaye ni mmoja wa viongozi waandamizi wa Chama
cha Kikomunisti cha nchi hiyo chenye uhusiano wa muda mrefu na CCM,
atakwenda kwenye Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) Ubungo,
Dar es Salaam kutembelea viwanda na kupata taarifa za fursa za uwekezaji
katika sekta ya viwanda nchini.
Aidha, ratiba hiyo imeeleza kuwa atahudhuria mkutano wa biashara na
uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, kabla ya kukutana na Spika wa Bunge,
Job Ndungai na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein katika wakati
tofauti.
Pamoja na ujumbe wake atatembelea hifadhi ya wanyama ya Saadan
iliyoko Bagamoyo na kuondona nchini Machi 11 kuelekea Msumbiji kuendelea
na ziara yake.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 9 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment