Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Ufundi na Teknolojia, Profesa Joyce
Ndalichako amezuia Ulaji wa Sh bilioni 4 zilizokuwa zitumike kwa ajili
ya semina ya siku nne.
Akizungumza wakati akifunga mkutano mkuu
wa tatu wa maofisa elimu mkoa na wilaya nchini, Profesa Ndalichako
alisema amezuia mafunzo yaliyokuwa yagharimu Sh4 bilioni ambayo mtu
mmoja alitengewa Sh4 milioni kwa ajili ya semina ya siku nne.
“Ina
maana kila mtu alikuwa alipwe shilingi milioni moja kwa siku. Kweli
hatuoni aibu kutumia fedha hizo kwa mafunzo. Watu walewale wanaokwenda
kwa mafunzo yaleyale,” alisema.
Alisema wakati hayo yote yakitendeka,
wanafunzi wananyeshewa mvua kwa kukosa madarasa na wanakaa chini kwa
kukosa madawati.
Profesa Ndalichako, pia alisema amegundua
ufisadi katika Sh66 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mafunzo, ujenzi na
ukarabati wa miundombinu ya shule nchini.
Alisema Novemba mwaka
jana, Serikali ilitoa Sh63 bilioni katika mikoa yote nchini, kwa ajili
ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu.
Profesa Ndalichako
alisema baadhi ya fedha hizo zilitolewa bila kufuata utaratibu sahihi,
hivyo kufanya wengine kutofahamu kama kuna fedha kama hizo zilitolewa.
“Kuanzia
Jumatatu nitapeleka orodha na kiasi cha fedha kilichopelekwa kwa Ma-RC
(wakuu wa mikoa) na Ma-DC (wakuu Wilaya) nchini ili mzione. Fedha
zitawatokea puani…cha mtu sumu, kama ulikula fedha hizo uhakikishe
unazirejesha.”
Bila kumtaja jina, Profesa Ndalichako alisema kuna mtu alitumia Sh60 milioni kukarabati darasa moja la shule ya msingi.
“Hiyo
ni ukarabati wa darasa tu la shule za msingi. Wale waliokula fedha hizo
nawaambia zitawatokea puani, hatuwezi kuwavumilia,” alisema.
Akimkaribisha
mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Maofisa Elimu wa Wilaya na Mikoa (Redeoa),
Juma Kaponda alishauri walimu wa shule za msingi waimarishwe kwa maarifa
na lugha ya Kingereza.
Hata hivyo, alisema ni vyema stashahada ya elimu ya msingi ifundishwe kwa Kingereza .
Credit;Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment