Rais John Magufuli akimkaribisha Rais wa Vietnam, Truong Tang Sang alipowasili
kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam jana kwa mazungumzo akiwa kwenye
ziara ya siku nne nchini.
RAIS John Magufuli amesema anatamani mafanikio ya nchi ya Vietnam
kiuchumi na kubainisha kuwa ziara ya Rais wa nchi hiyo, Truong Tang Sang
nchini, ni fursa na changamoto kwa watanzania kujifunza mambo mengi,
yatakayosaidia kukuza pia uchumi wa Tanzania.
Aidha amehamasisha Watanzania kuchangamkia fursa na rasilimali
zilizopo nchini katika kujiinua na kuimarisha nchi yao kiuchumi. Alisema
Tanzania ni miongoni mwa nchi tajiri kwa rasilimali na fursa nyingi,
ingawa bado iko nyuma kimaendeleo. Kwa upande wake, Rais Sang amesema
nchi yake na Tanzania zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya
biashara, kilimo, viwanda na uvuvi lengo likiwa ni kuhakikisha nchi zote
zinanufaika kwenye ushirikiano huo.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na marais hao Ikulu
Dar es Salaam jana, Dk John Magufuli alisema ni wakati sasa wa Tanzania
kujifunza kutoka kwa nchi hiyo ya Vietnam ambayo pamoja na kukabiliwa
na vita ya muda mrefu, imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi
wa kati. “Ukweli ni kwamba ziara ya Rais Sang nchini kwetu ni muhimu
sana na imekuja kwa wakati muafaka.
Mwaka 1976 Rais wa Vietnam alikuja nchini na alichukua mbegu ya
korosho na kuipeleka nchini kwake, na leo hii Vietnam ni moja ya nchi
zinazoongoza kwa kuzalisha korosho duniani,” alisema. Alitaja mafanikio
mengine ya nchi hiyo ni pamoja na kuwa na uchumi wa kati, licha ya
kukabiliwa na mapigano ya muda mrefu. Ilipata uhuru wake mwaka 1945 na
ilidumu kwenye mapigano hadi Julai 2, mwaka 1976.
Alisema mwaka 1977 mapato ya kila raia wake yalikuwa ni dola 100,
lakini sasa imefanikiwa kupandisha mapato hayo na sasa kila raia wa nchi
hiyo mapato yake ni dola 2000 kwa mwaka na imepunguza kiwango cha
umasikini kwa asilimia 50. “Sisi tangu mwaka 1960 bado tuko kwenye nchi
masikini, kwa hiyo hii ni changamoto kwa nchi yetu. Tunatakiwa kujifunza
kuondokana na hali hii.
Wao uzalishaji kwa mchele wanalima mara tatu kwa mwaka, sisi tunalima
mara moja tu na inawezekana uzalishaji wetu ni mdogo sana,” alisema.
Alisema nchi hiyo pamoja na kuchukua mbegu ya korosho nchini, ndio nchi
inayoongoza kwa kuzalisha korosho duniani, wakati Tanzania ndio iliyotoa
mbegu hiyo, zao hilo badala ya kuzalishwa kwa wingi ndio uzalishaji
wake unafifia.
“Samaki sina uhakika kama walichukua huku, lakini leo hii Vietnam ni
wazalishaji wa samaki wakubwa sana. Lakini kwa nchi yetu ambayo ina
maziwa 21 na mito kila mahali na bahari lakini uzalishaji wa samaki uko
chini…” “Tuna ng’ombe zaidi ya bilioni 22 hadi bilioni 23 nafikiri
tunaweza kuwa wa pili barani Afrika baada ya Ethiopia, lakini ngozi zetu
za viatu hapa tunaagiza nje.
Kwa hiyo kwa hili watanzania tunatakiwa tusiogope kujifunza kwa wale
waliotutangulia ili na sisi nchi yetu iweze kufika mahali pazuri,”
alisisitiza Dk Magufuli. Alisema ujio wa Rais Sang pamoja na ujumbe wake
wa zaidi ya mawaziri takribani 20 na wafanyabiashara ni wakati pekee wa
Watanzania na wa Vietnam, kuimarisha ushirikiano uliokuwepo kwa zaidi
ya miaka 50 sasa kuhakikisha uhusiano unaleta maendeleo kwa pande zote.
“Ziara hii ni muafaka kwetu sisi watanzania kujenga uhusiano mzuri na
nchi ya Vietnam ili kuweza kujifunza na sisi tuweze kufikia lengo letu
la kuwa nchi ya kipato cha kati,” alisema. Pamoja na hayo, Rais Magufuli
alisema katika mazungumzo yake na Rais wa Vietnam alipata mwaliko wa
kutembelea nchi hiyo mwakani. “Kwa kweli mwaliko huu nimeupokea na
ninajisikia kuthaminiwa na kuheshimiwa sana,” alisema.
Kwa upande wake, Rais Sang alisema anajisikia fahari kuona uhusiano
kati ya Tanzania na nchi yake unaimarika. Alisisitiza kuwa uhusiano na
ushirikiano huo utaleta maendeleo ya dhati baina ya nchi hizo mbili.
Alipongeza serikali kupambana dhidi ya umasikini kwa kusisitiza kuwa
inafanya vizuri kiuchumi kwani ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo
uchumi wake unakua kwa kasi.
“Kama rafiki wa karibu tunavutiwa na maendeleo yenu hasa katika
kupambana na umasikini lakini pia ukuaji wa kasi wa uchumi wenu. Katika
mazungumzo yetu na Rais Magufuli tumezungumzia masuala mbalimbali ya
maendeleo, ikiwemo kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kilimo,
biashara na viwanda,” alisema rais huyo. Aidha, alisema uhusiano wa nchi
hizo mbili ni wa muda mrefu, kwani pamoja na umbali wa kijiografia
Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na
Vietnam.
Alisema ziara hiyo ni moja ya njia za kudumisha na kuboresha zaidi
uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Rais huyo alisema
kwenye mazungumzo yake na Magufuli, wamekubaliana kushirikiana katika
maeneo yatakayonufaisha nchi zote. Maeneo hayo ni kilimo, biashara,
viwanda na mawasiliano. Pia walisaini mikataba ya kutowatoza kodi mara
mbili wawekezaji na wafanyabiashara wanaowekeza katika nchi hizo.
Aidha Rais huyo alisema katika kikao chake na Rais Magufuli pamoja na
mawaziri wa nchi zote mbili wamekubaliana kuanzisha tume ya pamoja
itakayosimamia masuala ya uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo
mbili. Aidha marais hao walizungumzia masuala ya kimataifa ambapo wote
kwa pamoja walikubaliana suala la kuhakikisha amani na utulivu linapewa
kipaumbele na mataifa yote duniani.
“Tulikubaliana kuwa nchi zote zina wajibu wa kuhakikisha suala la
amani linapewa kipaumbele, ikiwemo na mataifa ya kimataifa kuwa mstari
wa mbele katika kuhamasisha na kutuliza vurugu zinazoibuka katika nchi
mbalimbali,” alisema. Alisisitiza kuwa amemwalika Rais Magufuli
kutembelea Vietnam wakati wowote. Tayari Marais wastaafu Benjamin Mkapa
na Jakaya Kikwete, walishafanya ziara katika nchi hiyo wakati wa utawala
wao.
Rais Sang aliyeongozana na ujumbe wa watu 51 ataendelea kuwepo nchini
kwa ajili ya kumalizia ziara yake katika maeneo mbalimbali, ikiwemo
kutembelea Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).
Chanzo habariLeo.
Wednesday, 9 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment