KAMPUNI ya uwindaji na utalii wa picha ya Mwiba Holding Limited
imemchefua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutokana na madai ya kunyanyasa
Watanzania na kutoa angalizo kwamba itafutiwa uwekezaji huo.
Mwiba Holding Limited inayofanya utalii wa uwindaji na picha katika
Pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu katika mkoa wa Simiyu,
inashutumiwa kwa vitendo vya unyanyasaji wa wananchi wanaozunguka eneo
la ranchi walilolitwaa kuendesha shughuli hiyo.
Mbunge wa Meatu, Salum Khamis, alidai mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa
kuwa kampuni hiyo inanyanyasa Watanzania kwa kuwateka, kuwatesa na
kwamba imeingia mikataba ya ovyo yenye harufu ya rushwa na vijiji saba
katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao.
Wilaya ya Meatu iliyoanzishwa Julai 1, 1987, ina ukubwa wa kilometa
za mraba 8,835, na asilimia 49 ya eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za
wanyamapori ambazo ni Pori la Akiba la Maswa, sehemu ya Hifadhi ya
Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na WMA. Kutokana na madai
hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Eraston
Mbwilo, kuchunguza madai hayo na ifikapo Ijumaa wiki hii, awe amempa
ripoti.
“Leo (juzi) ni tarehe tano… Hadi tarehe kumi na moja nipate ripoti.
Ikibidi waondoe, siyo lazima abaki yeye. Mwekezaji lazima afuate
masharti, kama sivyo afutwe aondoke. Huo mwiba utamchoma mwenyewe,”
aliongeza Waziri Mkuu huku akishangiliwa na wananchi wa Meatu.
Katika maelezo yake baadaye kwa gazeti hili, Mbunge Salum alidai kuwa
Mwiba Holding Limited na kampuni dada ya TGT imemilikishwa hekta 12,000
katika kijiji cha Makao kwa ushirikiano na Halmashauri, na kupewa
ranchi ambayo ilikuwa inategemewa na wananchi kwa kilimo na mifugo.
Aidha, alisema vijiji vya Mwangudo, Irambandogo, Sungu, Mbushi,
Lukale na Sapa vimejumuishwa katika WMA na wawekezaji hao kuchukua hekta
29,000 na kuingia mkataba mwingine na kijiji cha Mwangudo na kupewa
hekta nyingine 79,000.
Alidai kuwa wawekezaji hao wanatumia askari wao wanaolipwa mishahara,
na kwamba katika mikataba hiyo, Halmashauri inalipwa Sh milioni 40 kwa
mwaka na kijiji cha Makao Sh milioni 24, fedha alizoeleza kuwa ni ndogo
kulinganisha na mapato ya Mwiba inayomiliki hoteli ya nyota tano katika
eneo hilo.
Alivitaja vitendo vya unyanyasaji vinavyofanyika kuwa ni pamoja na
mifugo kufukuzwa kwa kutumia helikopta na kuingizwa makorongoni pamoja
na askari wake kuwafuata wananchi umbali wa kilometa 50 na kuwatesa.
Akizungumzia tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Onesmo
Lyanga alisema kwa kuwa Waziri Mkuu amemwagiza Mkuu wa Mkoa kufanya
uchunguzi, ni vyema wao wakasubiri uchunguzi huo na kama kutakuwa na
jukumu linalowataka kulifanya, watafanya hivyo.
Chanzo HabariLeo.
Monday, 7 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment