Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu ametoa siku tatu kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake
Tanzania (TWB), awasilishe maelezo kwa nini benki hiyo inatoza kiwango
kikubwa cha riba kwa wanawake katika mikopo, wakati inapewa fedha na
Serikali kwa ajili ya kusaidia kundi hilo.
Pia waziri huyo ametangaza kiama kwa wakurugenzi wote wa halmashauri
za wilaya wasiotenga asilimia tano ya bajeti yao kwa ajili ya mfuko wa
maendeleo ya wanawake, kuwa kuanzia sasa, watakaoshindwa kutimiza agizo
hilo, watatumbuliwa majipu. Alisema hayo jana kwenye kilele cha
maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, jijini Dar es Salaam.
Alisema alishitushwa na taarifa aliyopatiwa juzi katika sherehe za
kukabidhi mikopo kwa wanawake zilizofanywa na Benki ya Posta Tanzania
(TPB), baada ya kubaini kuwa benki hiyo ya wanawake inatoza kiasi
kikubwa cha riba katika mikopo yake.
“Nilisikitika sana kusikia eti TPB inatoza vikundi vya akina mama
riba ya asilimia 11 wakati benki ya wanawake inatoza riba ya zaidi ya
asilimia 19. Hili siwezi kulikubali hivi inaingia akilini kweli wanawake
kushangilia benki nyingine wakati ipo benki ya wanawake kwa ajili yao,
tena iliyoanzishwa kwa ruzuku ya Serikali? Alihoji.
Alimtaka Mkurugenzi wa benki hiyo, Margareth Chacha (aliyekuwepo
kwenye maadhimisho hayo), kumpatia maelezo ndani ya siku tatu kwa nini
benki hiyo inatoza kiwango hicho kikubwa cha riba. “Nataka mnieleze kwa
nini benki hii si rafiki kwa wanawake wakati inapewa fedha na Serikali.”
Alisema imemuumiza kuona wanawake wa jiji la Dar es Salaam
wakiikimbia benki yao iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwakwamua kimaendeleo
na kukimbilia benki nyingine. “Nawahakikishia wanawake wenzangu hili ni
jipu tutalitumbua.”
Alisema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha
inawawezesha wanawake kiuchumi na ndio maana ilianzisha benki hiyo ya
wanawake, mifuko mbalimbali ya maendeleo ya wanawake, Taasisi za Kuweka
na Kikopa (Saccos) na Vikoba.
Katika eneo la mifuko ya maendeleo ya wanawake, Waziri huyo
alifafanua kuwa Serikali kwa mujibu wa Sheria ilianzisha mifuko hiyo na
kuzitaka halmashauri zote nchini kutenga kiasi cha asilimia tano katika
bajeti yake kwa ajili ya mifuko ya maendeleo ya wanawake.
“Nafahamu kwamba katika halmashauri nyingi hili limekuwa halifanyiki.
Napenda niweke wazi kuwa hatutashindwa kuwawajibisha wakurugenzi wote
wasiotenga kiasi hiki cha fedha kwa ajili ya mfuko wa wanawake.
Kuanzia sasa Mkurugenzi yeyote asiyetenga asilimia tano kwanza ni
adui wa wanawake na pili tutampeleka kwa Rais John Magufuli kwa hatua
zaidi,” alisisitiza. Aidha alisisitiza kuwa wizara yake itatafuta orodha
ya wakurugenzi wote wasiotenga kiasi hicho cha asilimia 50 kwa ajili ya
wanawake na kuiwasilisha orodha hiyo kwa Dk Magufuli kwa kuwa si tu
wamewadharau wanawake, lakini pia wamedharau agizo la Rais huyo.
Alisema pamoja na jitihada zinazoendelea kufanyika kuwainua wanawake
ili kuweza kufikia lengo la 50 kwa 50 kama ilivyo kauli mbiu ya
maadhimisho ya wanawake mwaka huu inayosema 50 kwa 50 ifikapo 2030;
tuongeze jitihada, bila kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi, lengo
hilo haliwezi kutimia ipasavyo.
Alisema kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2010 katika kila Watanzania
100, 23 ni wanawake wenye kipato kinachozidi au sawa na wanaume. “Sasa
kwa nini tusiwe wote na kipato sawa 50 kwa 50 hili linawezekana
tukitekeleza mipango yetu ipasavyo.”
Akizungumzia mafanikio ya Serikali katika kuhakikisha usawa na haki
kwa wanawake, alisema kwa sasa Tanzania imepiga hatua na kiwango cha
uwiano kati ya wanaume na wanawake katika ngazi za maamuzi kimepanda
ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Angela Kairuki, aliwataka wanawake kutumia fursa hiyo
kutafakari nafasi ya wanawake na mtoto wa kike katika jamii, ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha wanashiriki katika ngazi za maamuzi.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 9 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment