Thursday, 3 March 2016

Tagged Under:

Apiga marufuku malori barabara za manispaa Dar

By: Unknown On: 21:41
  • Share The Gag
  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik.

    MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amepiga marufuku utoaji wa vibali vya malori ya mizigo na magari yenye uzito wa zaidi ya tani 10 kuingia katika barabara zote zinazosimamiwa na Manispaa za jiji la Dar es Salaam.
    Barabara hizo ni zile zilizojengwa kwa kiwango cha lami na hatua hiyo inatokana na barabara hizo kuharibika kwa kipindi kifupi kutokana uzito jambo linaloisababishia Serikali hasara.
    “Kuanzia leo katika mkoa wangu ni marufuku kutoa vibali vya magari yenye uzito wa zaidi ya tani 10 kuingia kwenye barabara zetu, tunataka barabara zidumu, watakaokaidi watachukuliwa hatua,” alisisitiza Sadiki.
    Sadiki aliziagiza manispaa za jiji hilo kuweka alama za barabarani zinazoonesha zuio kwa magari yote yenye uzito wa zaidi ya tani 10 kupita kwenye barabara hizo ili wamiliki na madereva watakaokiuka agizo hilo wachukuliwe hatua kali za kisheria.
    Alikuwa akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es Salaam kwenye kikao cha kwanza kwa mwaka 2016. Alisema manispaa za jiji hilo zinatenga fedha nyingi kujenga barabara mpya na kufanya matengenezo ya zilizopo lakini nyingi zinaharibiwa na malori ya mizigo.
    Alisema baadhi ya magari yenye uzito wa tani 40 hudiriki kupita kwenye barabara za huduma ama za dharura (service road), madaraja na wakati mwingine maeneo ya waenda kwa miguu na kusababisha uvunjaji wa kingo za barabara na milingoti ya taa za barabarani na kuongeza kuwa vitendo hivyo vinaisababishia Serikali hasara kutokana na gharama ya matengenezo.
    Kuhusu ulinzi na usalama wa watumiaji wa barabara za jiji hilo, ameitaka Polisi kuendelea kuchukua hatua na kufanya operesheni dhidi ya madereva wa pikipiki (bodaboda) na bajaji wanaopitisha vyombo vyao vya usafiri kwenye njia za waenda kwa miguu na kusababisha usumbufu na ajali za mara kwa mara.
    ‘‘Ninaiagiza manispaa ya Kinondoni kuondoa wafanyabiashara wote walioko eneo la kituo cha kuzalishia umeme Ubungo, eneo lile ni hatari kwa usalama na maisha yao, kukaa pale ni kinyume cha sheria,’’ alisema Sadiki.
    Alisema mwaka huu Mkoa wa Dar es Salaam umetenga Sh bilioni 343.5 ikilinganishwa na Sh bilioni 266.6 zilizotengwa mwaka 2015/2016 kutekeleza ujenzi na matengenezo ya barabara katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo ili kupunguza msongamano wa magari.

    Chanzo HabariLeo.


    0 comments:

    Post a Comment