Monday, 1 February 2016

Tagged Under:

JK apata uteuzi mwingine Afrika

By: Unknown On: 21:19
  • Share The Gag

  • Rais Mstaafu, Dk Jakaya Kikwete.
    RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amekubali uteuzi wa kuwa Balozi wa Heshima wa kuhamasisha masuala ya afya na kuwataka Wakuu wa Nchi za Afrika kuweka kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za afya katika jamii.
    Kikwete aliyasema hayo mjini Addis Ababa nchini Ethiopia juzi, wakati akitoa salamu zake baada ya kukubali kuwa Balozi wa Heshima wa ‘Africa United’ kupitia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Gavi.
    “United Africa” ni mpango uliobuniwa kusaidia uhamasishaji wa masuala ya afya ukiongozwa na Gavi, CAF, Umoja wa Afrika, Benki ya Dunia na CDC Foundation na wameamua kutumia michezo kama nyenzo mojawapo ya kufanya kampeni ya kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa masuala ya afya yanayolikabili Bara la Afrika.
    Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Jopo la watu mashuhuri la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya namna bora ya kuendeleza na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu hususani katika afya ya uzazi ya mama na mtoto, alisema upatikanaji wa chanjo utasaidia kuokoa vifo vingi vya watoto Afrika.
    “Upatikanaji wa chanjo ni muhimu kwa kuokoa maisha ya watoto barani Afrika na dunia kwa ujumla. Chanjo itakuwa muhimu kwa kuzuia vifo zaidi ya milioni 1.5 vinavyotokea kila mwaka,” alisema Kikwete katika hotuba yake iliyopatikana Dar es Salaam jana.
    Alisema chini ya uongozi wake ataelekeza zaidi katika uhamasishaji wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kwa kuzingatia kuwa chanjo ni muhimu katika kuokoa afya za watoto.
    Kikwete alisema United Africa utazinduliwa rasmi katika Fainali za Nne za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zinazoendelea nchini Rwanda ambako sasa zinaingia hatua ya nusu fainali. Balozi huyo ameomba kuungwa mkono katika kampeni hiyo ya upatikanaji wa chanjo na huduma za afya.
    U t e u z i huo umekuja huku Rais huyo mstaafu akiteuliwa pia kuwa Mjumbe Maalumu wa AU nchini Libya.

    Chanzo Gazeti la HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment