Bunge
linaanza rasmi usajili wa wabunge na watumishi wa Bunge hilo pamoja na
wageni mbalimbali, wanaoingia bungeni kwa kutumia mfumo wa kisasa wa
kuchukua alama za vidole.
Sambamba
na mfumo huo, Bunge pia limetoa taarifa rasmi ya kudhibiti urushaji wa
matangazo ya Bunge ambayo sasa vyombo vya habari vya kielektroniki
havitaruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa bunge na kamera kwa lengo la
kurekodi yanayoendelea.
Na
badala yake, jukumu la kurusha matangazo ya vikao vya Bunge litafanywa
na Bunge lenyewe kupitia Feed Maalum ili kurahisisha kila kituo cha
redio na televisheni kupata matangazo hayo kwa sehemu walipo bila
kufunga mitambo yao bungeni.
Hayo
yalibainishwa jana na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah wakati
akitoa taarifa kwa Naibu Spika wa Bunge hilo, Dk Tulia Ackson alipofanya
ukaguzi wa ukarabati uliofanywa ndani ya Ukumbi wa Bunge linaloanza
vikao vyake vya Bajeti katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 mjini hapa.
Dk
Kashilillah alisema kuanzia jana wabunge wataanza usajili kwa njia ya
kuchukuliwa alama za vidole badala ya utaratibu wa zamani wa kujisajili
kwa kutumia makaratasi.
Alisema
usajili huo utachukua alama za vidole vyote 10 na lengo la kutumia
mfumo huo ni kuboresha kanzi data ya Bunge na kwamba usaili huo
utapunguza pia matumizi ya makaratasi ambayo yana gharama.
“Tumeanza
usajili huo leo (jana) kwa wabunge waliofika, ila tutaendelea kusajili
nadhani ndani ya wiki tutakuwa tumekamilisha kazi hiyo, na tumejipanga
kuifanikisha kwa haraka,” alisema Dk Kashilillah.
Akizungumzia
usajili huo, Dk Kashilillah alisema utasaidia kufahamu idadi ya wabunge
waliohudhuria vikao vya bunge na hivyo itakuwa rahisi kwenye kazi ya
upigaji kura wakati wa kupitisha hoja mbalimbali.
Alisema
Bunge limeboreshwa na kuwa la kisasa zaidi ambapo kila meza ya mbunge
ndani ya ukumbi huo, itakuwa na ‘tablet’ itakayomuwezesha kufuatilia
majadiliano ya bunge hata ya siku zilizopita na pia wabunge wataweza
kuona ratiba ya shughuli mbalimbali za Bunge.
Akizungumzia
elimu kwa wabunge hao juu ya matumizi ya mfumo huo, Dk Kashilillah
alisema wameandaa utaratibu wa kuwaelimisha wabunge hao juu ya matumizi
ya mfumo huo, ili iwe rahisi kwao kuutumia.
Naye
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Bunge, Didas
Wambura alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha matangazo ya bunge
yanapatikana kwenye vituo vya televisheni kama ilivyopangwa.
Wambura
alisema kuanzia sasa Bunge litarusha matangazo ya Bunge lenyewe kupitia
feed maalumu ili kurahisisha kila kituo cha televisheni na redio kupata
matangazo hayo kwa sehemu walipo, bila kufunga mitambo yao bungeni.
“Tutarusha matangazo ya Bunge wenyewe tutatumia Feed Maalumu itakayorushwa na satelaiti ya INTELSAT 17,” alisema Wambura.
Kutokana
na hatua hiyo, vituo vya televisheni na redio nchini havitaruhusiwa
kuingiza kamera zao ndani ya Ukumbi wa Bunge kurekodi vikao hivyo na
badala yake wanapaswa kutumia Masafa ya Matangazo ya Bunge.
Katika
mabadiliko hayo, pia idadi ya viti vipya 94 vimefungwa ndani ya Ukumbi
wa Bunge hilo na hivyo kufanya idadi ya vitu vyote vya ukumbi kuwa 404.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge,
Owen Mwandumbya alisema watakaa na wadau wote wa habari ili kuona ni
namna gani wataweza kupata matangazo hayo.
“Haturuhusu
wapiga picha za televisheni na redio kuingia na kamera ndani ya Ukumbi
wa Bunge kurekodi, kazi hiyo itafanywa na Bunge, ila waandishi wa habari
wa magazeti na wapigapicha za mnato wataendelea kuingia,” alisisitiza Mwandumbya.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment