Karafuu ni moja ya rasilimali zilizopo Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed
Shein amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), haijapokea
taarifa ya kufutiwa misaada kutoka kwa nchi wahisani, mbali na taarifa
ya kujitoa kwa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC).
Alisema hayo jana baada ya kutangaza Baraza la Mawaziri na kusisitiza
kuwa, pamoja na kutokuwa na taarifa hiyo, Serikali ya Zanzibar na
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, zimejiandaa kutumia
rasilimali zake za ndani kuleta maendeleo.
Kwa mujibu wa Dk Shein, misaada ni njia moja ya kusaidia kuleta maendeleo lakini si ya lazima.
Alisema, SMZ imejipanga kuhakikisha inatumia vizuri rasilimali zake
kwa kukusanya mapato na kufanya kazi kwa ufanisi na ubunifu wa hali ya
juu.
“Hatujapata taarifa ya kusitishiwa misaada kutoka kwa wahisani, hata
hivyo, tumejipanga vizuri kuhakikisha tunatumia rasilimali zetu, taasisi
zinazokusanya mapato nchini na Bodi ya Mapato zitakusanya mapato
kikamilifu, ikiwa ni njia moja ya kupunguza utegemezi,” alisema.
Kauli hiyo ya Dk Shein imekuja siku chache baada ya Jumuiya ya Ulaya
(EU), kukanusha habari zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii na
kwenye baadhi ya magazeti kuwa wadau wa maendeleo, ikiwemo nchi zilizoko
katika jumuiya hiyo, wamejitoa kuchangia bajeti ya Tanzania.
Balozi wa EU, anayeongoza umoja wa nchi 28 ambazo ni miongoni mwa
wachangiaji wakubwa wa bajeti ya Serikali, Roeland van de Geer alisema,
ingawa hajafurahia kilichotokea Zanzibar, lakini hawajafikia uamuzi wa
kusitisha misaada kwa Tanzania.
Balozi huyo alisema, kwa uelewa wake, hata Marekani haijajitoa, ila
kilichotokea ni MCC ya nchi hiyo kusitisha uhusiano wake na Tanzania.
Makadirio ya bajeti ya Serikali ya mwaka huu yaliyotangazwa wiki hii
na Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango, ni Sh trilioni 29.5 huku Serikali
ikiwa imejipanga kupata Sh trilioni 18.46 kutoka katika vyanzo vya
ndani na misaada ikitarajiwa kuwa Sh trilioni 3.6.
Chanzo Habarileo.
Saturday, 9 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment