Sunday, 10 April 2016

Tagged Under:

Vyama vya siasa vyafurahishwa na Shein

By: Unknown On: 22:05
  • Share The Gag

  • Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein akimuapisha Hamad Rashid Mohamed kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi katika hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu.

    KLABU ya Viongozi wa Vyama vya Siasa nchini imefurahishwa na uamuzi wa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa hatua yake ya kuwateua wawakilishi kutoka vyama vya upinzani, huku ikielezwa ni hatua za kuigwa na viongozi wote wa Afrika.
    Wakati Rais Shein akipongezwa kwa hatua hiyo ya kuunda Baraza la Mawaziri lenye mawaziri watatu wa vyama vya upinzani, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameshauri CUF na CCM kuangalia uwezekano wa kumaliza mgogoro baina yao.
    Vyama tisa kupitia klabu ya viongozi vilivyompongeza Dk Shein ni ADA-TADEA, United Peoples Democratic Party (UPDP), Chausta na Sauti ya Umma (SAU). Vingine ni Chama cha Wakulima (AFP) na Chama cha Kijamii (CCK).
    Akizungumza kwenye hafla hiyo kwa niaba ya vyama vingine, Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa alisema Rais Shein amejitahidi kufanya demokrasia ionekane kuchukua mkondo wake.

    Alisema hatua ya Dk Shein kuteua wawakilishi hao kuwa Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ni hatua ya kuigwa na kupongezwa kwani ameonesha ukomavu wa kidemokrasia.
    “Kwanza tunampongeza Dk Shein kwa ushindi wa tetemeko aliopata…lakini kubwa ni kumpongeza kwa hatua yake ya kuteua wawakilishi na baadaye kuwa mawaziri katika vyama ambavyo havikuwa na uwakilishi, ameonesha kuwa inawezekana,” alisema Dovutwa.
    Alisema Dk Shein amefungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini kwa uteuzi huo. “Tunatoa mwito kwa viongozi wa Afrika wayaone haya, tunaposema Serikali ya Umoja wa Kitaifa basi taifa lionekane, isiwe taifa la watu wawili au watatu, huyo ni mtu na familia yake…taifa lazima likusanye watu wote na taaswira ya kitaifa ionekane,” alisema Dovutwa.
    Akizungumzia sababu ya vyama hivyo kukataa kujiunga na vyama vinavyounda Ukawa, alisema walikwepa kudhalilishwa kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wagombea wa vyama vinavyounda umoja huo katika maeneo mbalimbali.

    “Lakini kuna watu wanasema uchaguzi wa marudio ulikuwa na upungufu, hao wana haki kabisa kwa sababu ndio ubinadamu, lakini na sisi tunaoona uchaguzi ulikuwa sawa tuna haki zaidi kwa sababu ndio utu wenyewe huo,” alisema Dovutwa.
    Katibu Mkuu wa Chama cha AFP, Rashid Rai alisema, chama chake kitampa ushirikiano Dk Shein katika kila jambo lenye maslahi kwa wananchi na taifa kwa ujumla. “Dk Shein amefanya kitu kikubwa sana katika taifa hili, wapo wanaobeza maamuzi yake, wapo wanaoona hajafanya kitu na wapo wanaoona Zanzibar bado kuna matatizo, lakini hakuna kitu kama hicho shida ya Zanzibar ilikuwa ni kupata viongozi na hilo limefanyika,” alisema Rai.
    Katika hatua nyingine, klabu hiyo ya Viongozi wa Vyama vya Siasa iliyozinduliwa rasmi jana, ilielezwa kwamba awali ilikuwa ikiitwa Umoja wa Vyama visivyo na Uwakilishi Bungeni.


    “Licha ya kuwa na tofauti za kisera na itikadi za vuyama hizo hatuingilii, hapa tuna ajenda moja tu tunayoibeba ya kuangalia namna gani vyama hivi vitakaa sawa kiuchumi na kisiasa,” alisema.
    Aidha, alisema umoja huo pia utatumika katika kuunga mkono jitihada za serikali za kuwashawishi wananchi kujiunga na Bima ya Afya ili wanachama wake waweze kuwa na bima ili kuwa na uhakika wa huduma za afya kwa kuwa ugonjwa hauna hodi.
    Alisema hatua hiyo inatokana na Wenyeviti wa vyama vitatu ambao ni Paul Kyara wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), John Chipaka wa ADA TADEA, na James Mapalala wa Chausta kuwa wagonjwa, hivyo wao wataanza kuwa mfano kwa kujiunga na bima ya afya kwa wale ambao hawajajiunga.

    Maridhiano CUF, CCM
    Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Kitila Mkumbo, ameshauri vyama hasimu visiwani Zanzibar ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kuangalia uwezekano wa kumaliza mgogoro unaoendelea visiwani humo kwa maslahi ya Zanzibar.
    Akizungumzia mustakabali wa kisiasa visiwani humo hasa baada ya Rais wa Zanzibar Dk Shein kukamilisha kuunda Serikali kwa kuunda Baraza la Mawaziri, alisema hali ya kisiasa Zanzibar bado si shwari kutokana na chama kikuu cha upinzani cha CUF kujitoa kisiasa .
    “Si mara ya kwanza kwa Zanzibar kuunda Serikali yenye wapinzani, wenyewe wamejiwekea utaratibu wa Serikali ya Umoja kupitia Katiba yao, ila wapinzani hawa wa sasa sote tunajua ni sawa na Serikali moja ya CCM, sidhani kama wataweza kutekeleza maridhiano yaliyofikiwa mwaka 2010,” alisema.

    Hata hivyo, alisema ili hali ya kisiasa iweze kutengemaa visiwani humo ni lazima wanasiasa hasa wale wanaohusisha vyama viwili hasimu kuona umuhimu wa kutatua tatizo la kisiasa kwa mustakabali wa Zanzibar.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment