Wafugaji na abiria wa mabasi ya abiria yakiwa yamekwama kwa zaidi ya saa tisa katika eneo la
Chalinze Nyama, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma jana baada ya maji ya
mafuriko kukata mawasiliano ya barabara kutokana na mvua.
MAGARI zaidi ya 1,500 jana yalikwama kwa saa tisa katika eneo la
Chalinze Nyama ,Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na kusababisha adha
kubwa kwa abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Kanda
ya Ziwa na wale wa kutoka Dodoma kwenda Morogoro na Dar es Salaam.
Kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari zaidi ya kilometa 10 kutoka
upande mmoja kwenda upande mwingine kutokana na mafuriko hayo
yalisababishwa na mvua iliyonyesha kuanzia juzi jioni na kusababisha
barabara kujaa maji kiasi cha njia kushindwa kuonekana.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ambaye alifika eneo la
Chalinze Nyama kujionea hali halisi, aliwataka madereva kuchukua hadhari
ya hali ya juu pindi wanapopita kwenye eneo lililojaa maji. Pia
aliwataka wananchi wanaoishi mabondeni kuhama kwani mvua bado zipo na
zinaendelea kunyesha.
Mvua hiyo iliyonyesha usiku kucha, ilianza saa tatu usiku hadi
asubuhi, imeharibu pia miundombinu ya barabara kwani nguzo za umeme
katika maeneo kadha wa kadha pembezoni mwa barabara kuu katika Wilaya ya
Chamwino eneo la Kijiji cha Chalinze Nyama zilionekana kuinama na
kukaribia kuanguka.
Kulingana na maelezo ya wakazi wa kijiji hicho ambako magari yote
yaliyoanza safari ya kutoka mjini Dodoma kwenda Dar es Salaam na
Morogoro yalikwama baada ya maji mengi kusambaa juu ya daraja na
kusababisha magari yashindwe kupita, walisema yalisababisha hofu kubwa
kwa wenyeji na wasafiri pia.
Maji ya mafuriko hayo yaliyokuwa yakitiririka kutoka maeneo ya
milimani Kata ya Hombolo yalianza kujaa barabarani na maeneo ya
kuzunguka nyumba za wakazi wa Kijiji cha Chalinze Nyama, yakiwafanya
wenyeji kukaa nje maeneo ya mwinuko wakiwamo akina mama na watoto wao
wadogo pamoja na wazee.
Takribani kaya zisizopungua 100 na magari zaidi ya 1,500 yakiwamo
mabasi ya abiria na malori yalizuiwa kuendelea na safari zao na askari
wa usalama barabarani ili kuepusha kutokea kwa ajali au kusombwa na
maji. Kwa kiasi barabara hiyo kuu ilifungwa kwa muda kuanzia saa 12:00
alfajiri hadi saa tisa alasiri baada ya maji kupungua ndipo
yaliporuhusiwa kuendelea na safari.
“Ilipofika saa nne hivi kuna basi lilijaribu kupita lakini
likaserereka abiria wakatokea madirishani baada ya hapo hakuna gari
ambalo liliruhusiwa kupita mpaka sasa,” alisema mkazi mmoja wa Chalinze
Nyama.
Aidha, familia inayosadikiwa ni ya Shehe wa Msikiti wa Jumuiya ya
Ahmaddiyya uliopo kijijini hapo jirani na barabara itokayo Dodoma kwenda
Dar es Salaam, walijikuta nyumba yao imezungukwa na maji ya mafuriko
hayo na kushindwa kutoka nje hadi Jeshi la Zimamoto kutoka Dodoma Mjini
walipokuja kuwanusuru.
Familia hiyo ya mama na wanawe wanne wadogo, ilijikuta katika wakati
mgumu, na mama huyo alisema hadi alfajiri hawakujua endapo maji
yalizunguka nyumba yake na kusababisha hofu na wao kushindwa kutoka nje.
Pia mvua hiyo imesababisha miundombinu ya umeme hususani nguzo
zinazosambaza umeme kwenye kijiji hicho kwenda hadi wilayani Kongwa
kuanguka na kusababisha umeme kukatika tangu usiku huo wa saa tisa usiku
hadi jana. Mafundi wa Tanesco walionekana wakifanya kila juhudi
kurekebisha hali hiyo ili zisianguke katika maeneo ya watu.
Pia nyumba za wanakijiji wapatao 30 wa Kijiji cha Nzali, Kata ya
Hombolo Wilaya ya Chamwino pia hawana mahali pa kuishi kutokana na
athari za mvua hiyo. Hadi saa tisa alasiri, maji yalikuwa yakitiririka
kwa wingi japo magari yalishaanza kuruhusiwa kuendelea na safari.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema serikali itahakikisha wananchi walioathirika wanapata huduma zote.
Chanzo HabariLeo.
Tuesday, 5 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment