Raisi Yoweri Musseveni wa Uganda akiwa katika mkutano wa 13 wa ushoroba wa kasikazini jijini Kamapala jana ambapo Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga. Katika mkutano huo Rais
Museveni alitangaza rasmi kwamba bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima katika Ziwa Albelt nchini Uganda litapita katika Ardhi ya Tanzania kwenda bandari ya Tanga.
BOMBA la mafuta ghafi kutoka Hoima katika Ziwa Albert nchini Uganda, sasa ni rasmi
kwamba litapita katika ardhi ya Tanzania kwenda Bandari ya Tanga,
ambako ndiko meli kubwa za mafuta, zitakapotia nanga kubeba mafuta hayo
kwenda sehemu mbalimbali duniani.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, imeeleza
kuwa Serikali ya Uganda imetangaza rasmi uamuzi wake wa kutumia bandari
hiyo.
Kwa hatua hiyo, bomba hilo linalotakiwa kuwa limekamilika ifikapo
2018, litaingilia Mkoa wa Kagera kutoka nchini Uganda na kupita katika
mikoa ya Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma hadi Bandari ya
Tanga.
Rais Museveni
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, ndiye
aliyetangaza uamuzi huo wakati wa mkutano wa 13 wa Ushoroba wa Kaskazini
uliomalizika jijini Kampala jana.
“Ujumbe wa Tanzania uliokamilisha mazungumzo hayo na kushuhudia
utangazwaji wa hatua hiyo, uliongozwa na Dk Augustine Mahiga, Waziri wa
Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,”
imeeleza taarifa hiyo.
Mbali na kiongozi huyo, taarifa hiyo imeeleza kuwa jopo la wataalamu
lililoshiriki katika mazungumzo hayo, liliongozwa na Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambalo litaendelea kubakia Kampala
kukamilisha mpango huo wa bomba la mafuta ghafi, ambalo litanufaisha pia
nchi zingine za Afrika Mashariki na Kati.
Mchakato ulivyokuwa
Awali, serikali za Uganda na Kenya, ziliwahi kufikiria kupitisha
bomba hilo katika ardhi ya Kenya, kwa nia ya kutumia bandari
itakayojengwa ya Lamu nchini humo.
Hata hivyo, wakati hatua za kina hazijachukuliwa, Rais wa Tanzania,
Dk John Magufuli na Rais Museveni walikutana mwanzoni mwa mwezi uliopita
na baada ya mazungumzo yao, wakatoa agizo kuwa mchakato wa ujenzi wa
bomba hilo, ufanyike kwa kasi.
Baada ya kikao cha marais hao kutoa agizo hilo, kilifuata kikao cha
Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total, tawi la Afrika
Mashariki, Javier Rielo, ambapo kiongozi huyo wa kampuni alimhakikishia
Rais Magufuli kuwa kampuni yao itaanza ujenzi wa bomba hilo haraka
iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.
Katika mazungumzo hayo, Rielo alimueleza Rais Magufuli kuwa kampuni
yake inatarajia kutumia Dola za Marekani bilioni 4 ambazo tayari
zimeshaandaliwa.
Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha
mafuta ghafi mapipa 200,000 kwa siku kutoka Ziwa Albert nchini Uganda,
hadi Bandari ya Tanga na ujenzi wake unatarajiwa kuzalisha ajira za moja
kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
Makubaliano ya awali
Katika utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli na Rais Museveni, Machi
17 mwaka huu, serikali za Tanzania na Uganda pamoja na kampuni ya Total
E&P Uganda na Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC),
walitia saini mpango wa pamoja wa utekelezaji wa mradi huo.
Mpango huo ulitiwa saini na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania,
Profesa Muhongo; Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda,
Irene Muloni; Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio na Meneja
Mkuu wa Total E&P Uganda, Adewale Fayemi.
Kwa nini Tanzania
Baada ya utekelezaji wa agizo hilo kufikia hatua ya mkataba kuliibuka
mjadala kuhusu uhakika wa bomba hilo kupita Tanzania baada ya Rais wa
Kenya, Uhuru Kenyatta kukutana na Rais Museveni, kujaribu kuangalia
uwezekano wa bomba hilo kupitia Kenya kwenda Lamu.
Pamoja na jitihada hizo, Bandari ya Tanga, ilibakia kuwa eneo pekee
lenye mazingira bora, nafuu na yenye ufanisi kwa utekelezaji wa mradi
huo.
Uzoefu
Mbali na Bandari ya Tanga kuwa ya kimkakati zaidi katika utekelezaji
wa mradi huo, taarifa za ndani za wataalamu wa mafuta, zilionesha kuwa
pia Tanzania ndiyo yenye uzoefu wa muda mrefu na wa hivi karibuni wa
ujenzi, uendeshaji, ulinzi na uelimishaji jamii katika miradi ya bomba
la mafuta.
Uzoefu wa muda huo mrefu unatajwa kuwa ni wa ujenzi, uendeshaji na
uhudumiaji wa Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama) tangu mwaka
1968, likitoka Dar es Salaam mpaka Ndola Zambia.
Bomba hilo lenye kipenyo cha nchi 8 mpaka 12 na urefu wa kilometa
1,710; kati ya hizo kilometa 860 zipo kwenye ardhi ya Tanzania na
limekuwa likipitisha mafuta tani milioni 1.1 kwa mwaka.
Tanzania pia ina sifa ya uzoefu wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji
wa bomba la gesi kutoka Songo Songo mpaka Dar es Salaam, lenye kipenyo
cha nchi 12 na urefu wa kilometa 25 kutoka kisiwa cha Songo Songo mpaka
Somangafungu.
Pia kuna bomba lingine la urefu wa kilometa 207 na kipenyo cha nchi
16, kutoka Somangafungu mpaka Ubungo Dar es Salaam, mbali na bomba kubwa
la gesi kutoka Mtwara mpaka Kinyerezi Dar es Salaam lenye zaidi ya
kilometa 490.
Lipo pia bomba la gesi linalotoka Mnazi Bay kwenda Mtwara, urefu wa
kilometa 27 na kipenyo cha nchi 8, ambalo limeanza kutumika tangu 2006.
Uzoefu wa kazi
Katika ujenzi na uendeshaji wa mabomba hayo kwa miaka mingi, Tanzania
imejijengea uzoefu wa kazi ya kupata ardhi kwa ajili ya kupitisha
miundombinu ya bomba, tofauti na ugumu uliopo kwa nchi shindani ya Kenya
na kusimamia masuala ya kimazingira.
Tanzania pia imefanikiwa katika kusimamia wakandarasi wa kimataifa na
matarajio ya umma wakati wa ujenzi na uendeshaji wa miradi hiyo na hata
katika ulinzi wa miundombinu hiyo ambao umekuwa ukishirikisha jamii.
Utayari
Bandari ya Tanga
Sifa nyingine iliyochangia Tanzania kukubalika zaidi katika mradi huo
kwa kiwango cha kusaini mkataba wa utekelezaji tofauti na Kenya, ni
utayari na mazingira wezeshi ya asili ya Bandari ya Tanga.
Wakati Kenya wakijadili namna bomba hilo litakavyotumia bandari
ambayo haijajengwa ya Lamu, kwa ajili ya kuuza mafuta, Bandari ya Tanga
yenyewe iko tayari kwa kazi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bandari ya Tanga imeshakamilisha
Tathimini ya Athari za Kimazingira (EIA) na Upembuzi Yakinifu, wakati
njia ya Tanga ya bomba hilo imekwishaainishwa na haitapitia katika
hifadhi za taifa wala mapori ya akiba.
Bandari ya Tanga inayo fursa ya kutumika zaidi na mradi huo, kwa kuwa
haina msongamano wa shughuli za bandari na tayari Serikali ya Tanzania
kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA), kwa mujibu wa taarifa hiyo,
imeshatenga fedha za upanuzi utakaohitajika na eneo.
Bandari hiyo pia imeunganishwa kwa reli na barabara za lami,
zinazokwenda nchi za jirani na hivyo iko tayari kuanza kutumika kwa
ajili ya kuingizia mizigo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
Bandari ya Tanga pia ndiyo yenye kingo za asili zinazoruhusu shughuli
za upakiaji mafuta kufanyika mwaka mzima bila kusimama, tofauti na
bandari zingine ambazo kipindi cha mawimbi makali ya bahari, huwa na
wastani wa siku 40 ambazo husababisha shughuli za upakiaji au upakuaji
mizigo kusimama.
Pia bandari hiyo inatumika na hivyo kuwa tayari kwa matumizi ya
haraka kama ilivyo dhamira ya Rais Magufuli na Rais Museveni, na hata
ujenzi wa boya la kupakia mafuta unatarajiwa kuchukua mwaka mmoja tu
hivyo kukamilika Juni 2017, kabla ya muda uliowekwa na mwekezaji wa
kuanza kuuza mafuta wa 2018.
Gesi mikoa saba.
Mbali na fursa hizo za pekee, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa
TPDC, Dk Mataragio, mradi huo unafungua fursa kwa usambazaji wa gesi
asilia katika mikoa ya Kaskazini yaani Dodoma, Singida, Shinyanga,
Tabora, Geita, Mwanza na Kagera na vile vile nchi za jirani ambazo
zitahitaji gesi ya Tanzania. Pamoja na hayo, kutakua na ujenzi wa
barabara mpya kiasi cha Kilometa 200 na uboreshaji wa barabara zilizopo
kiasi cha Kilometa 150 na madaraja.
Aidha utekelezaji wa mradi huo pia utachochea shughuli za utafiti wa
mafuta Tanzania, kwani bomba hilo linapita maeneo ambayo yana uwezekana
mkubwa wa kuwa na mafuta, hivyo uwapo wa miundombinu unavutia zaidi
uwekezaji katika shughuli za utafiti wa mafuta na gesi.
Fursa nyingine inayotajwa ni ya matumizi ya reli ambapo takribani mabomba 123,000 yatasafirishwa katika kipindi cha ujenzi huo.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 23 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment