Monday, 18 April 2016

Tagged Under:

Serikali yazibana shule binafsi

By: Unknown On: 21:25
  • Share The Gag

  • Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa

    WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imeziagiza shule zote za binafsi kuwa na mihula miwili tu ya masomo kwa mwaka badala ya kuwa na mihula mitatu au minne kama ilivyo kwa sasa katika shule hizo.

    Agizo hilo liko kwenye Waraka wa Elimu Namba Moja wa Mwaka 2015, ambao unaeleza kuwa kuanzia sasa mihula ya masomo, itakuwa miwili kwa kila mwaka wa masomo kwa shule zote za serikali na zisizo za Serikali.
    Waraka huo uliosainiwa na Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa umefafanua kuwa kila muhula, utakuwa na likizo fupi na likizo ya mwisho wa muhula. Siku za masomo kwa mwaka zitakuwa ni 194.

    Waraka huo pia umeagiza wanafunzi wote, wapumzike mwezi Juni na Desemba na mashindano ya michezo ya shule za msingi (Umitashumta) na michezo ya sekondari (Umiseta), ifanyike mwezi Juni wakati wa likizo.
    Kutokana na agizo hilo, wamiliki wa shule zisizo za serikali wametakiwa kuwasilisha wizara ya elimu kalenda za mihula ya masomo. Nakala ya waraka huo wamesambaziwa wakaguzi wote wa shule, walioko kwenye kanda na wilaya kuhakikisha wanazifuatilia shule zote ili ziweze kutii agizo hilo la Serikali.

    Profesa Bhalusesa alifafanua katika waraka huo, umekazia Waraka wa Serikali Namba 5 wa mwaka 2012 ambao ulikuwa unaelekeza mihula ya masomo kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu, ifanane ili kuepusha usumbufu kwa walimu na kwa wanafunzi.
    “Bado kumekuwa na hali ya kutofautiana kwa tarehe ya kufungua na kufunga shule katika mihula hiyo kati ya shule za serikali zenyewe na kati ya shule za serikali na shule zinazomilikiwa na watu binafsi au mashirika ya dini. Hali hii imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wadau wa elimu wakiwemo wazazi na walezi wa wanafunzi,” ulisema waraka huo.
    Kauli ya Waziri.

    Akifafanua kuhusu waraka huo jana, Naibu Waziri Stella Manyanya alisema shule zote za binafsi na serikali ngazi ya awali, shule ya msingi na sekondari zitalazimika kufuata maagizo hayo ya Serikali.
    Alifafanua kuwa muhula wa kwanza ulianza Januari 6 hadi 10, 2016 na likizo fupi ilianza Machi 24, 2016 na kufungua Aprili 4, 2016 na watamaliza muhula huo Juni 10 hadi 14, 2016. Muhula wa pili ngazi hiyo ya elimu awali utaanza kati ya Julai 8 na 11, 2016 ambako shule zote zitafunguliwa.
    Likizo fupi wataanza Septemba 8, 2016 na watafungua Septemba 21, 2016 na muhula wa pili utamalizika kati ya Novemba 30 na Desemba 6, 2016.

    Manyanya alisema kwa upande wa kidato cha tano na sita, muhula wa kwanza utaanza kati ya Julai 8 hadi 11, 2016 na likizo fupi itaanza Septemba 8, 2016 na watafungua Septemba 21, mwaka huu wakati likizo ya Desemba watafunga kati ya Novemba 30 na Desemba 6, mwaka huu.
    Naibu Waziri huyo alisema michezo kwa mashindano ya shuleni itafanyika wakati wa likizo ya mwezi Machi na ile ya ngazi ya Taifa ifanyike wakati wa likizo ya mwezi Juni kama ilivyosisitizwa kwenye waraka huo wa elimu.

    TAMONGSCO yapinga
    Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo binafsi (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya akizungumzia waraka huo, alisema hawakubaliani na agizo hilo la Serikali la kuwa na mihula miwili mikuu na miwili mifupi kwamba inawapotezea muda wanafunzi na hivyo kusababisha wafeli kwa wingi kwenye mitihani yao ya mwisho.

    Aliongeza kuwa mihula ya shule za serikali, jumla yake ni minne na wala sio miwili. Aliongeza kuwa kwa mtazamo wa haraka, mihula hiyo inamfanya mwanafunzi akae nyumbani siku nyingi zaidi kuliko mihula mitatu ya shule zisizokuwa za Serikali.
    “Sisi ambao tuna mihula mitatu mwanafunzi anapoteza wiki sita tu kwa mwaka, lakini tukiamua kufuata waraka wa serikali mwanafunzi anajikuta anapoteza wiki nane, hizi ni siku nyingi kwa mwanafunzi kukaa nyumbani,” alisema Nkonya.

    Alisema Tamongsco baada ya kupokea barua za kuwataka wabadilishe mihula ya masomo, wameshaiandikia wizara na kuwapa ufafanuzi kuwa licha ya kuwa na mihula hiyo siku za masomo zimebaki kuwa 194 ambayo inashauriwa na Serikali yenyewe.
    “Sisi tunagombana na Serikali kwa sababu wanataka tufuate mihula yao, sisi tunaona kwamba tukifuata hayo maelekezo yao watoto wengi watafeli kama ilivyo kwa shule za serikali ndio maana tunaendelea kupinga suala hilo,” alisema Nkonya.

    Baadhi ya shule binafsi zatii Gazeti hili limefanikiwa kupata barua za baadhi ya wanafunzi wanaosoma shule binafsi zilizoamua kuwaandikia wazazi na walezi kuwa wako kwenye maandalizi ya kuingia kwenye kalenda ya serikali ya kuwa mihula miwili ya masomo.
    “Serikali imeagiza shule zote zifuate kalenda kama zinavyofanya shule zake ili kurahisisha ufuatiliaji wa sera na maagizo mbalimbali ya kielimu. Hivyo nasi tukiwa ndani ya serikali hii hatuna budi kutii agizo hilo la Serikali. “Hivyo tunawatangazia kuwa tupo katika hatua za mwisho kuingia katika utaratibu ambao utatufanya tuwe na mihula miwili huku likizo ndefu zikiangukia mwezi wa Juni na Desemba,” ilisema barua ya shule moja binafsi ambayo gazeti hili limepata nakala yake.

    Licha ya shule hiyo, baadhi ya wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule za msingi za binafsi nao wamekiri kupokea barua kutoka kwa uongozi wa shule kuwa wanajiandaa kuanda mihula ya serikali, lakini suala la ada italipwa kwa mihula minne.
    “Sisi katika shule anayosoma mwanangu wameshaanza kuwa na mihula miwili, ila ada tunalipa mara nne kama ilivyokuwa hapo awali,” alisema mzazi mmoja ambaye hakutaja jina lake litajwe gazetini.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment