Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa
nchini kuchukua hatua kali kwa wote waliosababisha kuwepo kwa watumishi
hewa. Amesema suala hilo la watumishi hewa limeisababishia serikali
hasara kubwa hivyo ni lazima watu wote waliohusika katika mchakato huo
wabainishwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za utumishi.
Waziri Mkuu, Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akipokea taarifa ya
maendeleo ya Mkoa wa Lindi iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Godfrey
Zambi katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi wilayani Ruangwa .
Waziri Mkuu alisema kazi ya kubaini watumishi hewa inalenga kuokoa
fedha za serikali ambazo zilikuwa zinalipwa watumishi waliokufa,
kustaafu wengine ni wale ambao wahusika walijiwekea majina na kisha
fedha kuingia mifukoni mwa wajanja.
“Makatibu tawala wa mikoa ndio wakuu wa watumishi katika mikoa, hivyo
ni lazima tusikie wamechukua hatua gani kwa wote waliosababisha kuwepo
kwa watumishi hewa na si kukaa kungoja maagizo ya Rais,” alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zambi katika taarifa yake kwa Waziri
Mkuu alisema mkoa huo una jumla ya wafanyakazi watoro 57 na hewa saba
ambao ni marehemu, wastaafu waliokuwa wanalipwa mishahara na
kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 36 kwa mwezi mmoja.
Alisema kazi hiyo ya kubaini watumishi hewa na watoro itakuwa
endelevu. Alisema wameanzisha timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi
kubaini sababu zilizosababisha watumishi waliokufa au kustaafu kuendelea
kulipwa.
Rais John Magufuli wakati akiwaapisha wakuu wapya wa mikoa Machi 15
mwaka huu, aliwapa siku 15 kuhakikisha wanabaini watumishi hewa wote
katika mikoa yao na kuwaondoa katika mfumo wa malipo.
Baada ya kufanyika, jumla ya watumishi hewa 7,795 walibainika ambao
wameisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 7.5. Fedha zarejeshwa
Fedha za mishahara ya baadhi ya watumishi hewa zilizokuwa zikilipwa
kwenye halmashauri nchini zimeanza kurudishwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Sulemani Jafo alisema hayo juzi wakati akifunga mkutano wa
Jumuiya ya Tawala za Mikoa Tanzania (ALAT). Katika mkutano huo, Jafo
alisema anazo taarifa za halmashauri moja ambayo imerejesha Sh milioni
tano.
Ameagiza fedha zote zinazorudishwa, zikatiwe risiti. Katika mkutano
huo, Naibu Waziri alihoji kama zipo halmashauri zilizoanza kurejesha
fedha hizo, wakurugenzi wapatao watano walisimama kuthibitisha kufanya
hivyo kwenye halmashauri zao.
Hata hivyo, waliposimama kwa sekunde chache, hawakutaja halmashauri
zao wakaketi na mkutano ukaendelea. Naibu Waziri alisisitiza wakurugenzi
wa halmashauri kuhakikisha watumishi wote hewa wanarudisha fedha
walizokuwa wakilipwa.
Alisema hilo ni agizo la Rais John Magufuli na kwa dhamana waliyopewa
wakurugenzi, wanapaswa kusimamia kuhakikisha hakuna watumishi hewa
kwenye maeneo yao. “Kikubwa zaidi ni kuondokana na suala la watumishi
hewa kwani linaipunguzia serikali uwezo katika jukumu lake la kuhudumia
wananchi,” alisema.
Kufikishwa mahakamani Wakati Naibu Waziri akihimiza wakurugenzi
watendaji kufuatilia fedha hizo za watumishi hewa, Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe, ametaka wafikishwe mahakamani na wakati
huo huo fedha hizo zilizolipwa kila mwezi, zirejeshwe.
Mbali na kuwafikisha mahakamani watumishi hao, Mkuu wa Mkoa ameagiza
uchunguzi wa kina ufanyike kwa watumishi wengine hewa ambao wanaoneshwa
kuwa walistaafu, wagonjwa, waliokufa, kuacha kazi; kutaka taarifa zao
ziwasilishwe ofisini kwake kwa hatua zaidi.
Dk Kebwe alitoa agizo hilo hivi karibuni wakati akizungumza na
watumishi wa idara mbalimbali za serikali wa halmashauri ya Wilaya ya
Kilosa ikiwa ni ziara yake ya kwanza wilayani humo tangu ateuliwe
kushika wadhifa huyo.
Alisema katika uhakiki wa watumishi hewa katika halmashauri za mkoa
wa Morogoro, waliobainika ni 122 na kwamba ufuatiliaji zaidi unaendelea .
“Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mna watumishi hewa 29 , kati ya hao 17
ni watoro ...nakutaka Mkuu wa Wilaya na ODC, hawa watoro watafuteni
wapelekeni mahakamani na warejeshe fedha za serikali zikatiwe ritisi na
hawa ni wezi, “ alisema Kebwe.
Alimtaka Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa
kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina
kuhusu watumishi ambao wameoneshwa wamefariki, kustaafu , ugonjwa na
kuacha kazi ili kubaini ukweli wa jambo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele, alisema hivi sasa wako
makini kuhakikisha hakuna mtumishi hewa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kilosa na ofisi yake kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama
vinafuatilia mtandao uliokuwa umezalisha watumishi hewa na eneo mojawapo
ni la Idara ya Utumishi.
Akaunti za watumishi hewa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilosa, Idd Mshili, alimwomba Mkuu wa Mkoa kuwezesha kupata
zuio mahakamani akaunti za watumishi hewa ziweze kufungwa.
Mshili alisema, katika uhakiki wa watumishi hewa, halmashauri
ilibaini kuwa na watumishi hewa wapatao 29 , kati yao, watano ni
waliostaafu, sita ni marehemu, mmoja aliacha kazi na watumishi 17 ni
watoro.
Alisema halmashauri hiyo ina jumla ya watumishi 3,860 wa kada
mbalimbali huku kukiwa na upungufu wa watumishi 1,982 , sawa na asilimia
34 ya mahitaji ya watumishi wote 5,842.
“Pamoja na jitihada za Serikali za kukabiliana na tatizo hili, bado
upungufu huu umejitokeza zaidi kwenye sekta za elimu, afya , kilimo na
mifugo,” alisema Mshili. Habari imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma; John
Nditi, Morogoro na Mwandishi maalumu, Lindi.
Chanzo HabariLeo
Sunday, 10 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment