Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa na naibu waziri , Dk Khamis Kigwangala wakikagua mashine ya mobile digital x-ray wakati
walipotembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM) jana. Kulia ni Kaimu Mkuu wa hospitali hiyo Profesa Gesai.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania imeanza kuwa kimbilio
katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo na figo, kwa wagonjwa kutoka
nchi za jirani.
Alisema hayo jana alipotembelea hospitali ya Benjamini Mkapa, iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Majaliwa alisema, Serikali itaimarisha huduma hizo katika hospitali
hiyo, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Mloganzila,
ziwe vituo vya kitaaluma ili wananchi wapate manufaa ya uwepo wake.
Alisema, kupatikana kwa huduma hizo za magonjwa makubwa nchini
kutasaidia kuondoa gharama ambazo Serikali huingia kuwapeleka Watanzania
kutibiwa nje ya nchi.
“Hivi sasa Taasisi ya Jakaya Kikwete imeanza kutibu magonjwa ya moyo
na upasuaji. Tunataka matibabu yote ya figo, hata ya kubadilisha figo
yafanyike ndani ya nchi, hilo linawezekana. Wataalamu tunao, tena wengi
ni Watanzania na wanafanya kazi nyumbani kwa moyo wakijua kuwa wanaokoa
maisha ya ndugu zao na wazazi wao,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema, uwepo wa hospitali hizo ni kimbilio kwa Watanzania na kwa
wagonjwa wanaotoka nchi jirani, ambapo kwa sasa Tanzania imeanza kupokea
wanaotoka Malawi, Msumbiji, Comoro, Kenya na Uganda. Alisisitiza
umuhimu wa kuimarisha ulinzi katika kituo hicho, ili vifaa vilivyopo
viendelee kuwepo.
Aliongeza kuwa, Serikali imeamua kuiwezesha hospitali ya Benjamini
Mkapa ijitosheleze kwa kutoa huduma za matibabu kwa wakazi wa Kanda ya
Kati, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi, ili kuwapunguzia gharama za
kwenda Muhimbili.
“Hivi sasa kuna vyuo vikuu hapa nchini vinavyosomesha Watanzania
utaalamu wa juu wa tiba, ikiwemo UDOM, chuo hiki kitakuwa kituo cha
Watanzania kupata taaluma ya tiba kwa magonjwa yote makubwa, ili
wananchi wapate manufaa ya uwepo wake,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema kuna changamoto ya baadhi ya mashine kukaa
nje ya vyumba vilivyokusudiwa na kushindwa kufungwa kutokana na udogo wa
vyumba ikilinganishwa na ukubwa wa mashine.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 9 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment