Mjanae wa Rais wa kwanza baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere akiwa mwanawe,
Makongoro Nyerere na msaidizi wake akifurahia mandhari wakati
walipotembelea Daraja la Nyerere, lililopo Kigamboni Dar es salaam.
MJANE wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama
Maria Nyerere ametembelea Daraja la Nyerere linalounganisha eneo la
Kigambaoni na Kurasini, Dar es Salaam na kuipongeza Serikali na wananchi
wote wa Tanzania, kwa kufanikisha ujenzi wa daraja hilo kubwa na la
kisasa kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.
Mama Maria aliyeongozana na mwanawe, Makongoro Nyerere alisema
kukamilika kwa daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu Sh bilioni
254.12, kumekamilisha mpango wa miaka mingi ulioanzishwa na Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa na nia ya kujenga daraja katika
eneo hilo la mkondo wa bahari, lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti
haikuwezekana.
Aidha, alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuamua daraja hilo liitwe
Daraja la Nyerere kwa heshimu ya Baba wa Taifa; na alibainisha kuwa
uamuzi huo, utaviwezesha vizazi vijavyo kutambua juhudi zilizofanywa na
mumewe katika ujenzi wa nchi.
“Mimi ninamshukuru sana Rais John Magufuli kwa maana ilikuwa lipewe
jina lake, lakini yeye Mungu akamjalia akasema kwamba hapana, tukumbuke
tulikotoka, kwa hiyo najisikia vizuri sana, na familia nayo inajisikia
vizuri sana, lakini zaidi na Watanzania wanajisikia vizuri sana, kwa
maana watakuwa wanaulizana Nyerere alikuwa ni nani?” alisisitiza Mama
Maria.
Daraja la Nyerere lenye urefu wa meta 680, upana wa meta 32, njia
sita za magari na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5,
lilifunguliwa na Dk Magufuli wiki moja iliyopita na linakuwa kiunganishi
muhimu kati ya Kigamboni na katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 27 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment