Makamu wa Raisi Samia Suluhu Hassani akiwasha mwenge wa Uhuru kuzindua rasmi mbio za mwenge huo kwa mwaka 2016. Sherehe hiyo ilifanyika
katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Kulia ni Waziri wa
Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoo Zanzibar Moudelin Castiko.
SERIKALI ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, itaendelea kupambana
na vitendo vya rushwa na ufisadi kwa nguvu zote bila kutetereka.
Lengo la hatua hiyo ni kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya
Serikali na kuboresha uwajibikaji na maadili katika usimamizi wa
rasilimali za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema hayo katika hotuba yake
kwa Taifa wakati wa sherehe ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru
uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Hivyo aliwaomba Watanzania wote kuunga mkono kwa vitendo juhudi na
maelekezo ya Dk Magufuli za hatua anazozichukua dhidi ya vitendo vya
rushwa na ufisadi nchini. Kutokana na hatua hizo, Makamu wa Rais alisema
hadi sasa jumla ya kesi 596 za rushwa zinaendelea mahakamani na jumla
ya Sh 6,543,342,793 tayari zimeokolewa.
“Naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha Watanzania wenzangu kujiepusha
na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa,” alisema Samia na aliwataka
watumishi wa umma, watumishi katika sekta binafsi, wajasiriamali na kila
mmoja kujiepusha na vitendo vya rushwa na kutekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia katiba, sheria, kanuni, miongozo na taratibu zilizowekwa.
“Kama nilivyokwishasema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zinaendelea
kuhimiza mapambano dhidi ya Rushwa chini ya kaulimbiu “Timiza Wajibu
wako, kata Mnyororo wa Rushwa,” aliongeza Makamu wa Rais.
Samia alisema suala la rushwa limeongelewa mara nyingi na athari zake
zinajulikana ikiwa ni pamoja na ubadhirifu wa mali za umma, mikataba
isiyofaa kwa taifa na udanganyifu na kupokea fedha ili kukiuka sheria
kwa manufaa binafsi huchangia kwa kiwango kikibwa kuwanyima wananchi
hazi zao na kudhoofisha ustawi wa taifa letu.
Mbali na hatua hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuendelea na
mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, pia alisisitiza kwa mara nyingine
kwa kusema kuwa Serikali haina nia ya kumwonea mtu inapochukua hatua ya
kutumbua majipu kwa watumishi wa umma.
Akishangiliwa na wananchi wakati akiwahutubia kwenye sherehe hizo,
Makamu wa Rais alisema lengo la Serikali la kutumbua majipu ni
kurekebisha na kurejesha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji serikalini
kama ilivyoagizwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili
Watanzania wote wafaidike na matunda ya nchi yao.
“Mnasikia katika Serikali ya Awamu ya Tano tunarekebishana, majipu
yanatumbuliwa ...kwa kweli hatuna nia ya kumwonea mtu, tunarekebishana
na hilo ndilo lililomo katika agizo ya Ilani yetu ya CCM ili
kuwanufaisha Watanzania wote wafaidi matunda katika nchi yao,” alisema
Makamu wa Rais.
Chanzo HabariLeo.
Monday, 18 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment