Rais John Magufuli na Rais Paul Kagame wa Rwanda wakikata utepe kuzindua
Daraja la Kimataifa la Rusumo, linalotenganisha nchi hizo mbili kwenye
hafla iliyofanyika jana.
RAIS John Magufuli na Rais Paul Kagame wamezindua Daraja la Kimataifa
la Rusumo, linalounganisha Tanzania na Rwanda. Katika uzinduzi huo,
Rais Magufuli alitoa agizo la kufuta vituo kadhaa vya ukaguzi wa magari
ya mizigo yaendayo nchi za Maziwa Makuu vilivyoko Tanzania.
Vituo hivyo ni vilivyoko katika Barabara Kuu ya Dar es Salaam hadi
eneo hilo la mpakani la Rusumo na kubakiza vituo vitatu pekee. Magufuli
alitoa agizo hilo jana wakati wa uzinduzi wa daraja hilo pamoja na Kituo
cha Pamoja cha Forodha (OSBP) mpakani hapo katika wilaya ya Ngara kwa
upande wa Tanzania na eneo la Kirehe upande wa Rwanda.
Alitaja vituo vitakavyoendelea kufanya ukaguzi wa magari kuwa ni cha
Rusahunga mkoa wa Kagera, Singida na Vigwaza mkoani Pwani. Alisema
kuwepo kwa vituo vingi, kunasababisha msongamano na ucheleweshaji wa
magari na bidhaa, zinazosafirishwa na nyingine kuharibika njiani, kabla
ya kufika zinapopelekwa.
“Siku za nyuma kabla ya kuwepo miundombinu, kulikuwepo na
ucheleweshwaji mwingine ulikuwa wa makusudi kwa kuendekeza rushwa na
mwingine ukisababishwa na ukosefu wa miundombinu, kitu kinachotugharimu.
Tunatumia muda mwingi na kuwepo vituo vingi njiani, jambo
linalosababisha watu kusafiri kwa muda mrefu.
Safari ya siku mbili au tatu unatumia siku 15, sasa miundombinu ipo,
tusimamie usafirishaji ili tuweze kupandisha uchumi wa nchi yetu na
Afrika Mashariki na maendeleo ya wananchi wetu,” alisisitiza Magufuli.
Alisema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya watu walioko barabarani
kwenye vituo hivyo vya ukaguzi, kuwataka madereva wa magari ya mizigo
yaendayo katika nchi za Maziwa Makuu kila wakitaka kuanza safari, lazima
watenge fedha za rushwa kwa ajili ya kuacha katika kila kituo; na
endapo hawatofanya hivyo, hulazimishwa kuleta magunia ya mkaa, mbuzi au
kuku.
“Kuanzia leo nimepiga marufuku utaratibu huo, ndio maana nikaamua
vituo vipungue na kubaki vitatu tu, pia kama mtu ataendelea kuendekeza
rushwa hizo, aache kazi mara moja, hatuwezi kupata maendeleo kwa njia ya
rushwa wala kukwamishana,” aliagiza Rais.
Kuhusu daraja hilo lililojengwa awali mwaka 1977 , alisema lilikuwa
kikwazo cha kuharakisha maendeleo kwa nchi za Rwanda na Tanzania
kutokana na kiwango chake, lakini, sasa limejengwa kimataifa pamoja na
kituo cha OSBP.
Alisema ujenzi wa miundombinu hiyo, utaharakisha maendeleo ya nchi
hizo, kwani huo ndio msingi wa ushirikiano wa kweli, unaotakiwa kuwepo
kati ya nchi zinazounda Afrika Mashariki.
Magufuli alisema lengo la kuwepo vituo vya pamoja mipakani kama
kilichozinduliwa jana na marais hao ni kuwezesha watu kufanya kazi kwa
pamoja kwa ushirikiano wa kweli kati ya pande mbili, kwani asilimia 70
ya bidhaa za Rwanda hupitia Tanzania katika mpaka huo wa Rusumo.
Kufuatia uzinduzi huo, Magufuli aliwashauri wafanyabiashara wa
Rwanda, kuendelea kupitisha bidhaa zao Tanzania ili kufanya asilimia
hiyo kupanda na pia itasaidia nchi kuongeza mapato na kukua kwa uchumi
kutokana fedha itakayokuwa ikitolewa katika shughuli hizo.
Aliwataka wafanyabiashara hao, kuona fursa nya kutumia daraja hilo na
liwe chachu ya maendeleo kwa wananchi wa pande zote mbili kwani wote
wanategemeana. Magufuli aliwataka wasitengane maana raia wa nchi hizo ni
marafiki na ndugu wa muda mrefu na majirani kwa hiyo lazima wadumishe
amani iliyopo kupitia ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Rais wa Rwanda, Kagame alisema kuwepo kwa mradi huo
ni jambo kubwa katika maendeleo ya Tanzania na nchi yake kwa hiyo
amewashauri wananchi wa nchi hizo mbili kuendeleza amani iliyopo na
kuzidi kumuomba Mungu kuepusha majanga yasiyo na manufaa kwa jamii hizo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Mhandisi
Patrick Mfugale, akitoa taarifa juu ya mradi huo kwa marais hao, alisema
kuwa daraja la zamani lililokuwa na upana wa mita tatu, lilikuwa
likibeba tani 32 tu kwa wakati mmoja, wakati jipya lililozinduliwa, lina
upana wa mita 9.5 na linabeba tani 180 kwa wakati mmoja.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 6 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment