BAADHI ya wabunge wamepongeza mapendekezo ya ukomo wa bajeti ya mwaka
2016/17, yaliyowasilishwa na Serikali kutokana na bajeti hiyo kwa mara
ya kwanza, kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa fedha za nje, lakini
pia kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha katika matumizi ya maendeleo.
Akizungumza baada ya Waziri wa Fedha na Mipango kuwasilisha
mapendekezo ya ukomo wa bajeti hiyo pamoja na mpango wa maendeleo kwa
mwaka huo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni
Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), alisema mambo mema yamefanywa.
Alisema mambo matatu makubwa yakitekelezwa, itakuwa imetibu kiu ya
watanzania ya muda mrefu, moja ni kupeleka fedha nyingi kwa maendeleo na
kubana matumizi ya kawaida na pili imepunguza utegemezi wa wafadhili,
kufadhili bajeti ya nchi. Alisema hilo ni jambo jema na kusisitiza kuwa
msingi iwekwe ya kuimarisha.
“Ukomo wa bajeti ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, hili nalo
katika serikali ya awamu ya tano wameliona na kweli tuwaunge mkono, sio
kila kitu tuone kibaya, cha msingi tuwape nafasi tuone watamalizaje huko
mbele kwenye utekelezaji”, aliongeza Mbowe.
Kwa upande wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo)
alisema serikali imethubutu kupanga kiwango kikubwa cha bajeti na ni
vyema kuwatia moyo na kuacha tabia ya kukosoa jambo kwa hatua ya awali.
Alisema kitendo cha kuweka asilimia 40 kwenye bajeti ya maendeleo ni
hatua kubwa na kwamba mpango wa serikali kurasimisha sekta isiyo rasmi,
wakiwemo wafanyabiashara ndogo na wengine ambao hawakuwa wakilipa kodi,
utasaidia kuongeza mapato ya kodi.
“Ni hatua kubwa sana, cha msingi ni kuhakikisha bajeti ya maendeleo
ambayo imetengewa asilimia 40 ya mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2016/17
inatekelezwa, ni vyema tuwatie moyo”, alisema Zitto .
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), alisema mapendekezo hayo
yametoa mwanga na unafuu kwa watanzania kwa kuwa kupitia Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17, ambao umegusa maeneo mengi nyeti
yanayowagusa wananchi.
“Ni bajeti nzuri, kwa kweli imezingatia zaidi matakwa ya wananchi
hasa katika eneo la matumizi ya maendeleo. Si kwamba bajeti za nyuma
zilikuwa mbaya. La hasha. Lakini kutokana na utegemezi mkubwa wa fedha
za nje, zilionekana kuwa hazitekelezeki,” alisema Ngeleja.
Kwa upande wa Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM) alisema
mapendekezo hayo, yametoa matumaini na mwanga mpya kwa watanzania, kwani
kwa mara ya kwanza Serikali inaonyesha nia ya dhati ya kuachana na
utegemezi.
“Bajeti imeweka wazi utegemezi wa wahisani uko asilimia 12 tu ya
bajeti yote, miradi mingi ilikuwa haitekelezeki au kumaliza kutokana na
wahisani wengi kutotimiza ahadi zao, lakini sasa Serikali imeamua
kujikita katika ukusanyaji wa mapato yake na kutegemea zaidi fedha za
ndani,” alisisitiza Mapunda.
Mbunge huyo alipongeza hatua za Serikali ya awamu ya tano za
kuhakikisha matumizi yote ya fedha za Serikali yanafuatiliwa, ikiwa ni
pamoja na kuweka mfumo wa kuhakiki matumizi na mapato yake kila mwezi
ili kuona kama yanawiana.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema kwa sasa yapo matumaini
ya miradi ya maendeleo kukamilika kutokana na bajeti nzima kujikita
katika fedha za ndani, kwani kiasi kinachotarajiwa kutoka kwa wahisani,
hata kisipotolewa, upo uwezekano wa fedha hizo kupatikana kupitia mapato
ya ndani.
“Hata hao wahisani mara nyingi wamekuwa wakitoa ahadi, lakini
utekelezaji wao unaambatana na masharti mengine ambayo hayana hata
msingi. Na upatikanaji wa hela yao umekuwa mgumu. Sio hata hizi Shilingi
trilioni tatu hata wasipoleta tuna uwezo wa kuzikusanya kutoka humu
ndani,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Mimi naunga mkono jitihada za serikali ambazo
zimefanya na kutuondoa katika utegemezi wa misaada sana. Mimi naamini
kuwa nchi yetu ni tajiri ina vitu vingi sana, ambavyo vinaweza
kutufikisha mahala tukajitegemea”.
Kwa upande wake, mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi),
alisema mapendekezo ya bajeti hiyo, hayana uhalisia na huenda
yasitekelezeke, kwa kuwa yameegemea zaidi katika mafanikio ya muda mfupi
yaliyopatikana katika ukusanyaji wa kodi na faini za wakwepa kodi.
Kuhusu ushauri wake wa namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza
kukwamisha utekelezaji wa mapendekezo ya bajeti hiyo, mbunge huyo
alisema “waulizeni CCM, hiyo si kazi yangu”.
Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) alisema baada ya kumaliza
habari ya faini za kodi na wale waliokwepa kulipa kodi, makusanyo
yatashuka kwa kiasi kikubwa. Alishauri kuibuliwa kwa maeneo mengi,
yaliyotekelezwa yanayoweza kulipishwa kodi, ikiwemo eneo la bahari
ambalo kwa mujibu wake kwa sasa limegeuzwa kama shamba la bibi.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly (CCM), alisema mpango na
mapendekezo ya bajeti ni mzuri, kwa kuwa vitu vingi vimelenga mahitaji
ya wananchi na sasa kiu ni kuona utekelezaji wake.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 6 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment