Wilson Kabwe.
RAIS John Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
Salaam, Wilson Kabwe kutokana na kashfa ya ufisadi katika utekelezwaji
wa mikataba inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato ya stendi ya Ubungo na
kodi ya uegeshaji magari katikati ya mji.
Hatua hiyo ya Rais Magufuli, imetokana na kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwasilisha mbele yake taarifa ya Kamati
aliyoiteua kwa ajili ya kuchunguza kwa undani utekelezwaji wa mikataba
hiyo hasa katika eneo la mapato.
Makonda aliwasilisha ripoti hiyo Dar es Salaam jana wakati wa
uzinduzi wa daraja jipya na la kisasa kuliko yote Afrika Mashariki na
Kati la Kigamboni, ambalo kwa sasa limepewa jina jipya na Rais Magufuli
la Daraja la Nyerere.
Akizungumza mara baada ya kupatiwa taarifa hiyo, Rais Magufuli
alisema akiwa kama Rais wa Tanzania hatoweza kuwavumilia viongozi
wanaotumia jasho la wananchi kujinufaisha.
“Nasema wazi hapa viongozi wa namna hii kwangu hawana nafasi, sasa
nawauliza wananchi, kwa kiongozi kama huyu mnashauri nimchukulie hatua
gani?” Rais Magufuli alihoji wananchi waliohudhuria uzinduzi wa daraja
hilo la Nyerere ambao walijibu kwa pamoja “mtumbue.” “Sasa nachukua
fursa hii kumsimamisha kazi Kabwe na ninaitaka Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) ianze kuchukua hatua za kuchunguza suala
hili, endapo atathibitika hakuhusika sina tatizo, lakini akithibitika
kuhusika, hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi yake,” alisisitiza.
Pamoja na hatua hiyo ya kumsimamisha kazi Kabwe, pia Dk Magufuli
aliagiza Mkurugenzi atakayekaimu nafasi hiyo ya Ukurugenzi wa Jiji kwa
muda, aanze mara moja kusimamisha mikataba yote ya ukusanyaji mapato
stendi ya Ubungo na ule wa maegesho wa NPS hadi uchunguzi ukamilike.
Alisema amekuwa akichukua hatua hizo alizoziita maamuzi magumu kwa
kuwa ni dhahiri wananchi wamekuwa wakiitabika kwa muda mrefu kwa kukosa
huduma bora, wakati kuna baadhi ya watu wamekuwa wakijilimbikia fedha na
kujinufaisha wao binafsi.
“Narudia tena sina simile kwa watu wa aina hii, na mara zote
wakitokea mbele yangu nitawatumbua majipu. Viongozi wanaotaka kufanya
kazi na Serikali yangu wajipange kukabiliana na kuvumbua mabaya yote
dhidi ya wananchi. Watanzania wameteseka mno sasa huu ndio wakati wao wa
kujidai,” alisema Rais Magufuli.
Awali akitambulisha viongozi wa mkoa waliohudhuria sherehe za
uzinduzi huo, RC Makonda, pamoja na mambo mengine alibainisha kuwa muda
mfupi tangu ashike wadhifa wa Ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliunda
kamati ndogo kwa ajili ya kuchunguza mikataba katika stendi ya Ubungo na
wa maegesho ya magari katikati ya jiji.
Alisema kamati hiyo ilibainisha mambo mengi yanayofedhehesha kuhusu
mikataba hiyo, likiwemo suala la Mkurugenzi wa Jiji Kabwe, kusaini
mikataba miwili tofauti ya ukusanyaji wa mapato katika stendi hiyo ya
Ubungo kwa kutumia sheria ndogo tofauti ikiwemo iliyopitwa na wakati.
“Mkataba moja ulisainiwa Januari 30, mwaka jana kwa kutumia sheria
ndogo ya mwaka 2009 na mwingine ulisainiwa Januari 31, mwaka huu kwa
kutumia mkataba wa mwaka 2004 na mbaya zaidi mikataba yote hii
imesainiwa na mtu mmoja Kabwe,” alisema Makonda.
Alifafanua kuwa Sheria ndogo ya mwaka 2004 ya ukusanyaji mapato ndani
ya kituo hicho, inaonesha kuwa kila basi linatakiwa kutozwa Sh 4,000
hivyo makusanyo halisi kwa mwezi ni Sh milioni 42 kutokana na mabasi 350
yanayoegeshwa kituoni hapo.
Hata hivyo, alisema kutokana na mabadiliko ya tozo, sheria hiyo
ilibadilishwa mwaka 2009 na kila basi likawa linatozwa Sh 8,000 na hivyo
makusanyo ya mwezi yakapanda na kufikia Sh milioni 82 kwa mwezi.
“Lakini cha kushangaza tumebaini kuwa bado kampuni inayokusanya
mapato katika kituo cha Ubungo, inawasilisha mapato hayo kwa kutumia
sheria ya mwaka 2004 yaani Sh milioni 42 badala ya Sh milioni 82 kwa
mwezi…” …” Mbaya zaidi kamati ile katika ukaguzi wake, ilikuta kampuni
ya ukusanyaji mapato hayo stendi ya Ubungo inayo Sheria ya mwaka 2009
lakini katika nyaraka za Halmashauri ya Jiji zinaonyesha sheria
inayotumika ni ya mwaka 2004,” alisisitiza Makonda.
Kwa mujibu wa Makonda, kwa hali ilivyo tangu sheria ndogo ya mwaka
2009 ipitishwe haijawahi kutumika na hivyo kulisababishia hasara jiji
hilo ya Sh bilioni tatu kutokana na mapato katika stendi hiyo kuendelea
kuwasilishwa kwa kutumia sheria ya mwaka 2004.
“Ukipiga hesabu za harakaharaka utagundua kuwa kila mwezi Sh milioni
42 zimekuwa zikipotelea kwenye mikono ya wachache, kwa maana hiyo
kuanzia mwaka 2009 Sh bilioni tatu zimepotea na kila mwaka tumekuwa
tukipoteza Sh milioni 500, huu ni ufisadi wa aina yake kwa kweli,”
alisema.
Aidha Makonda alisema pia kamati yake iligundua aina nyingine ya
ufisadi ndani ya kituo hicho cha Ubungo kwa baadhi ya watu wakiwemo
vigogo kuhodhi mabanda ya biashara yaliyomo ndani ya kituo hicho na
kutoza kodi kubwa zaidi ya mara 10 ya ile inayostahili.
“Kwa mujibu wa taratibu, kila kibanda mle ndani ya stendi kinatakiwa
kukodishwa kwa Sh 100,000 hadi Sh 200,000 kwa mwezi, lakini tumebaini
kuwa wapo watu wachache wamevihodhi na kuvikodisha kwa zaidi ya Sh
milioni 1.5, kwa mwezi,” alisema.
Kuhusu mkataba wa maegesho katikati ya jiji kupitia Kampuni ya
National Parking System (NPS), alisema kamati hiyo pia imebaini kuwa
Halmashauri ya Jiji imeiongezea mkataba wa miezi 10 kampuni hiyo kinyume
cha taratibu wakati mkataba wake ulikuwa umeshamalizika.
Alisema mara baada ya mkataba huo kumalizika Agosti mwaka jana
kampuni hiyo iliandikiwa barua ya kuongezewa mkataba wa miezi sita na
baadaye miezi minne kwa madai kuwa mchakato wa kutafuta mzabuni bado
haujakamilika.
“Kiutaratibu mheshimiwa Rais, mkataba unapoisha lazima ufanyike
mchakato wa kutafuta mzabuni mpya na hata mwekezaji aliyepo anaruhusiwa
kushiriki kuomba tena, lakini kilichofanyika ni kinyume kabisa, wakati
tunajua kwa sasa eneo la mapato ya maegesho ni kubwa na maeneo mengi
yameongezeka kuna nini hapa? Alihoji.
Alisema endapo viongozi hawatokuwa waaminifu katika maeneo mbalimbali
yanayohusu fedha, kuna uwezekano mkubwa wa fedha za wananchi kupotea .
“Naomba Takukuru waendelee na uchunguzi wa suala hili ili waliohusika na haya wachukuliwe hatua,” alisisitiza Makonda.
Pamoja na hayo, alielezea mikakati yake akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku wafanyabiashara kuweka
biashara zao katika maeneo yasiyoruhusiwa na badala yake waende kwenye
maeneo yaliyopangwa.
“Juzi nilisikitika sana nilipata taarifa kuwa kuna kijana mmoja
mtembea kwa miguu kwa bahati mbaya alikanyaga nyanya za mfanyabiashara
aliyezipanga kwenye njia ya wapita kwa miguu, matokeo yake walimvamia na
kumpiga hadi kumuua. Huu ni uuaji huyu kijana alikuwa na haki. Kuanzia
sasa kila eneo la Dar es Salaam litumike kwa mujibu wa utaratibu wake,”
alisisitiza.
Aidha alimuahidi Rais Magufuli kuwa kwa kushirikiana na viongozi
wenzake, watasimamia miundombinu yote ya Serikali isiharibiwe na
wananchi wasiopenda maendeleo ikiwa ni pamoja na kung’arisha majengo
yaliyopo katikati ya mji ikiwemo ukuta wa Ikulu kwa kuyapaka rangi.
Jumapili, Makonda alitoa ripoti ya kamati hiyo ndogo aliyoiunda na
kutangaza wazi kuwasilisha majina ya Kabwe na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji,
Sarah Yohana kwa mamlaka za kinidhamu ili wachukuliwe hatua kutokana na
yaliyobainishwa kwenye mikataba hiyo.
Aidha aliweka wazi kuwa kutokana na madudu hayo yaliyobainishwa na
kamati hiyo, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, hataki kufanya kazi
tena na Kabwe pamoja Yohana.
chanzo HabariLeo.
Tuesday, 19 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment