Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
anayeshughulikia Utumishi na Utawala Bora, Selemani Jafo.
WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya ALAT wamesema wakala wa Ufundi
na Umeme (Tamesa) ni jipu linalohitaji kutumbuliwa. Walitoa hoja hizo
juzi mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Suleiman Jafo wakati
wakichangia hoja kwenye mkutano mkuu wa ALAT.
Wajumbe hao waliomba serikali kuangalia muundo wa utendaji wa Tamesa
kwani umejaa mizengwe mingi huku wakiwa hawana wataalamu katika suala
zima la utengenezaji wa magari.
Mmoja wa wajumbe alisema kuna maelekezo magari yote ya halmashauri
kutengenezwa na Tamesa lakini yakienda huko hakuna mafundi bali wanawapa
watu wengine watengeneze na gharama zinakuwa kubwa mara mbili.
Naibu Waziri alisema anaichukua hoja hiyo kuifanyia kazi na atakwenda
kuangalia ni nini kinatokea. Alisema pamoja na nia njema, lakini
kutokana na wajumbe wengi kugusia suala hilo inaonesha wazi kuwa
utekelezaji hauko sawa na hivyo ni lazima kuangalia kuna tatizo gani.
Jafo alisema serikali itatoa mafunzo kwa madiwani kwa kushirikiana na
Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Uongozi Institute kuhakikisha
madiwani wanapata mafunzo ya kuweza kusimamia vyema miradi ya wananchi
na maendeleo yao.
Pia alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejielekeza kuhakikisha sekta
za umma zinapata ushirikiano wa kutosha kutoka sekta binafsi ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Aidha alisema nchi haiwezi kujengwa bila kuwa na ushirikiano na sekta
binafsi na kuwataka wakurugenzi kutenga maeneo ya uwekezaji wakati huu
ambapo ujenzi wa viwanda unasisitizwa.
“Kila halmashauri itenge eneo kwa ajili ya uwekezaji kwa kutumia
sekta binafsi. Stendi ya mabasi ya Morogoro ni mfano wa kuigwa kwani
walitumia wadau kuwekeza na kuna aina ya uwekezaji ikiwamo maeneo ya
benki, maduka na baada ya muda itakuwa halmashauri yenye pato la uhakika
la ndani,” alisema.
Aliwataka mameya na wenyeviti wa halmashauri kwenda kusimamia
ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki kuwe na ufanisi.
Aliwataka wakurugenzi wasikubali kuangushwa na watumishi wa chini.
Alisema baadhi ya maeneo, wakuu wa idara wana sauti kuliko wakurugenzi.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 10 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment