Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hammad.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad amesema
uamuzi wa chama chake kususia uchaguzi wa marudio uliafikiwa na Baraza
Kuu la Uongozi na hauna uhusiano na taarifa kwamba amenunuliwa na Chama
Cha Mapinduzi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha Seif amelazimika kutolea ufafanuzi ukarimu aliofanyiwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kumlipia safari ya matibabu kwenda
India; Serikali ya Jamhuri ya Muungano kulipa gharama za kuwepo katika
Hoteli ya Serena na kutembelewa na viongozi wa ngazi za juu akisema,
havina uhusiano na kurubuniwa.
Katika kile kinachoonekana ni ‘kuwaangukia’ wanachama wake kupitia
mkutano wa waandishi wa habari aliofanya jana mjini hapa, Seif alisema
huo ni ukarimu na utamaduni wa viongozi unaotokana na ubinadamu .
Alisema uamuzi wa kujitoa katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20
ulitokana na chama hicho kutokubaliana na uamuzi uliofikiwa na Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa sababu uchaguzi huo ulikidhi mahitaji na
matarajio ya wananchi CUF iwe madarakani.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar
kupitia CUF, zipo taarifa kutoka kwa baadhi ya watu wanaodai kwamba
alijitoa kwenye uchaguzi huo wa marudio baada ya kurubuniwa na CCM ili
ipate ushindi mkubwa.
“Taarifa hizo hazina harufu ya ukweli,” alisema. “Kilichofanywa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kugharimia safari yangu ya kwenda
India matibabuni pamoja na kutembelewa na viongozi wa ngazi za juu
akiwemo Rais John Magufuli , kwanza ni wajibu wa serikali kwa sababu
mimi ni Makamo wa Kwanza wa Rais mstaafu….lakini huo ndio ukarimu na
uhusiano wetu Watanzania unaotokana na ubinadamu,” alisema.
Alisema msimamo wa CUF kutoitambua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein, upo pale pale kwa sababu chama hicho
kinaamini kilishinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 kwa kupata
majimbo ya uchaguzi ya Unguja na Pemba.
“Chama cha CUF hakijabadili msimamo wa kutoitambua Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein kwani sisi
tunaamini kwamba tulishinda katika uchaguzi wa Oktoba 25 kwa kupata
ridhaa ya wananchi walio wengi ambao walikipigia kura chama chetu na
kupata ushindi wa majimbo yaliyopo Unguja na Pemba,” alisema.
Juzi wakati Rais wa Zanzibar akizungumza na waandishi wa habari na
kutangaza Baraza la Mawaziri, Ikulu, alisema ushindi wake unatambuliwa
na wananchi walio wengi ambao ndiyo walioipa ridhaa CCM na kushika
hatamu ya kuongoza dola kwa asilimia 91.4.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 10 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment