Serikali
imeagiza wamiliki wa migodi ya madini ya tanzanite ambao migodi yao
imesimama kwa muda mrefu bila uzalishaji kwa madai ya kutokuwa na
madini, warudishe leseni zao wizarani mara moja.
Kauli
hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Prosefa James Mdoe, mara baada ya kukagua migodi ya
tanzanite ya Kitalu B,D na kitalu C kinachomilikiwa na kampuni ya
Tanzanite One, akiwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge inayosimamia shughuli
za Wizara ya Nishati na Madini.
Profesa
Mdoe alisema Sheria ya Madini ya 2010 iko wazi kwa wamiliki wa migodi
ambao hawajazalisha kwa muda mrefu, kwa kuwa inataka warudishe leseni
ili wapatiwe eneo lingine lenye madini.
Amesema kuendelea kusimama au kuchimba na kuingia mgodi mwingine ni kinyume na sheria na hatua kali zitachukuliwa.
Katibu
Mkuu huyo alisema kuwa migogoro mingi ya wachimbaji wa tanzanite, ni ya
‘mitobozano’ kwa maana ya wachimbaji kuingia katika maeneo ya wenzao na
watu kutofuata sheria zilizowekwa na Serikali kwa sasa haitavumilia.
Alisisitiza
kila mchimbaji wa madini ya tanzanite wilayani Simanjiro, kuheshimu
sheria ya madini iliyowekwa na Serikali badala ya kufanya kazi ya
uchimbaji kwa kufuata sheria ambazo si rasmi.
‘’Mgodi
wako ukimaliza uzalishaji nirudishie leseni yangu, lakini kuchimba kwa
kwenda katika mgodi wa mchimbaji mwingine, ni kinyume na sheria,’’ alisema.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Chumbuni Zanzibar, Ussi
Salumu Pondeza, alisema wataishauri Serikali kushughulikia tatizo la
mtobozano mapema kabla ya mchimbaji kuingia gharama kubwa.
Alisema
pia wamejifunza mambo mengi katika ziara hiyo na wana mengi ya
kuishauri Serikali ili madini hayo yanufaishe nchi ya Tanzania na si
nchi nyingine.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment