Waziri
wa Biashara na Viwanda wa Singapore, Dk. Koh Poh Koon, amesema
wamepanga kutumia bandari ya Dar es Salaam kuwa kiunganishi cha biashara
kati ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Dk.
Koon ameyasema hayo jana(Jumatano, Aprili 27, 2016), wakati
alipomtembelea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma,
na kwamba Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania
kwenda kufanya kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu
utakaosaidia uendeshaji wa bandari za Tanzania.
Dk.
Koon ambaye ameambatana na wafanyabiashara wakubwa wapatao 40,
amemweleza Waziri Mkuu kwamba kampuni ya Hyflux ya Singapore imeanza
kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalum la uchumi (Special Economic
Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitano
wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda vya kati
(light industries), maeneo ya biashara na nyumba za makazi zipatazo
37,000.
“Jiwe la msingi la mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na Waziri wa Biashara,Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage,” alisema.
Mbali
na ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, Dk Koon amweleza
Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia Tanzania kujenga uwezo wa
kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na uendeshaji wa
bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta.
“Hadi
sasa makampuni ya Singapore yaliyowekeza nchini ni pamoja na Pavillion
Energy ambayo imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 1.2 katika
sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani bilioni 3
kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant)
kitakachojengwa mikoa ya Kusini kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka
Ulaya na Marekani”.
Amesema
kampuni ya PIL ya Singapore inatarajia kuwekeza Dola za Kimarekani
milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa makampuni
ya gesi.
Amesema
lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo
pamoja na kuweka mikakati ya kuinua uchumi na kupanua wigo wa biashara.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa ameishukuru Serikali ya Singapore kwa
uwekezaji unaofanywa na makampuni yake nchini na kwa misaada ya
kiufundi ambayo wameitoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Ili
kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi, Waziri
Mkuu ameyakaribisha makampuni mengine ya Singapore kuja nchini kufanya
uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha
viwanda, mahoteli, kilimo na nishati.
Amemuahidi
Dk. Koon kwamba Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini
Mkataba wa Kuvutia na kulinda uwekezaji baina ya nchi mbili (Bilateral
Investment Protection and Promotion Agreement) na Mkataba wa Kuepuka
kutoza ushuru mara mbili (Double Taxation Avoidance Agreement) ili
kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Singapore.
Waziri
Mkuu, Majaliwa amewataka Watanzania kutumia fursa ya ushirikiano kati
ya Singapore na Tanzania kuanzisha biashara mpya zitakazowanufaisha
wote.
Waziri
Mkuu amesema Singapore ina uwezo mkubwa kibiashara pamoja na uzoefu wa
siku nyingi kwenye uendeshaji wa bandari hivyo Tanzania itapata nafasi
ya kujifunza namna ya uendeshaji katika sekta hizo.
Amesema
Tanzania imefungua milango ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa
Singapore kuja kuwekeza katika sekta za viwanda, usafiri wa anga na
kwenye Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ).
Credit;Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment