Raisi John Magufuli.
SASA ni wazi kwamba kasi ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli,
imeanza kuisambaratisha Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, inayoundwa na
vyama kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), baada ya jana
wabunge hao kususa hotuba ya Waziri Mkuu.
Mapema asubuhi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwasilisha Hotuba ya
Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Fedha za Ofisi hiyo kwa mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
Hotuba hiyo iliwasilishwa baada ya kukamilika kwa mjadala kuhusu
Mpango wa Maendeleo wa Taifa, uliowasilishwa na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Philip Mpango, Aprili 20, mwaka huu bungeni mjini Dodoma.
Katika mjadala huo, wabunge wa upinzani waliopata nafasi ya kujadili
Mpango huo wa Serikali, walishindwa kujizuia na kukiri kuwa Rais
Magufuli ni Rais wa mfano ambapo Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza
(Chadema), alikwenda mbali zaidi kwa kusema Tanzania imepata Rais sawa
na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Jana baada ya Waziri Mkuu kukamilisha hotuba yake kama ilivyo kawaida
ya Kanuni za Bunge, hotuba hiyo ilifuatiwa na maoni ya Kamati za Kudumu
za Bunge zinazoangukia katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Katika mpangilio huo wa kawaida wa Bunge la Bajeti, taarifa ya kwanza
ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria,
Mohammed Mchengerwa na baadaye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ukimwi, Constantine Kanyasu aliwasilisha maoni ya Kamati hiyo
kwa niaba ya Mwenyekiti wake, Hasna Mwilima.
Mbowe ‘ala kona’
Wakati ilipowadia zamu ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), kujitokeza mbele ya
wabunge kuwasilisha Mpango Mbadala wa Maendeleo wa Taifa na maoni ya
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu, kiongozi
huyo hakutokea.
Hatua hiyo ilimfanya Spika wa Bunge, Job Ndugai kutangazia Bunge kuwa
tofauti na ilivyo kawaida, alikuwa hajapokea taarifa ya Kambi hiyo
kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu na kusema suala hilo ni la ajabu na
halijawahi kutokea.
“Waheshimiwa Wabunge nafikiri mambo mazuri yaliyopo ndani ya hotuba
ya Waziri Mkuu yamewaduwaza wenzetu wa Kambi ya Upinzani na
kuwasambaratisha, maana hadi sasa sijapata hotuba ya maoni yao, kwani
baada ya kukamilika kwa taarifa za Kamati wao ndio walipaswa kufuatia,”
alisema Spika Ndugai na kuendelea; “Kwa vile hawa ni ndugu zangu na
natambua mchango wao mkubwa kwa Bunge hili, nawapa nafasi ya kujipanga
zaidi ili saa 10 wakati Bunge litakaporejea niwape nafasi ya kwanza ya
kuwasilisha hotuba yao,” aliongeza Spika na kusitisha shughuli za Bunge
mchana jana.
Bunge larejea, wasusa
Ilipofika saa 10 jioni jana, Bunge lilirejea kuendelea na kikao na
kama ilivyotarajiwa, Mbowe alitakiwa kuwasilisha Mpango Mbadala wa
Maendeleo wa Taifa na maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mpango wa
Serikali, pamoja na maoni ya Kambi hiyo kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu.
Tofauti na matarajio hayo, Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Mbowe ambaye hivi karibuni ameonesha waziwazi kukerwa na
utumbuaji majipu unaofanywa na Rais Magufuli, alisimama na kutangaza
kususa Hotuba ya Waziri Mkuu.
Akitoa sababu, Mbowe alisema wanasusa kushiriki mjadala wa Hotuba ya
Ofisi ya Waziri Mkuu kutokana na sababu tatu; mosi, ikiwa ni madai ya
Serikali kufanya kazi bila kuwa na mwongozo wa utendaji wake wa kazi kwa
wizara mbalimbali. Madai mengine kwa mujibu wa Mbowe, ni uvunjwaji wa
Katiba na sheria za nchi na kupokwa uhuru na madaraka ya mhimili wa
Bunge.
Mwenyekiti awashauri
Kutokana na kauli hizo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisimama
na kutoa ufafanuzi wa madai hayo kwa kusema hoja zilizotolewa na
wapinzani ni nzito na kuwashauri watafute msaada wa kisheria.
“Kwanza hoja iliyopo mezani ni mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu na
ofisi yake, sasa hii hoja mliyowasilisha ni kitu tofauti kabisa na
kinachojadiliwa, na kwa vile mmetoa madai mazito ya kuvunjwa kwa Katiba,
niwashauri mkatafute msaada wa kisheria, hapa tuendelee na hoja iliyopo
mezani,” alisema Chenge.
Alifafanua kwamba kwa kuwa wamedai Katiba imevunjwa, ni vyema baada
ya kupata ushauri wa kisheria, waende katika mhimili wa dola unaotafsiri
Sheria, ambao ni Mahakama kwa kuwa suala hilo la tafsiri bungeni si
mahala pake.
Baada ya kuwapa ushauri huo, Chenge alisema ni vyema mjadala wa
Waziri Mkuu uendelee kama ulivyokuwa kwenye ratiba ya mjadala na iwapo
kambi hiyo itashiriki, ni sawa na iwapo hawatashiriki ni uamuzi wao pia.
Watoka, Mbowe afafanua
Kauli hiyo ya Chenge ilisababisha Mbowe akifuatwa na wabunge wa
upinzani kuanza kutoka mmoja mmoja na walipofika nje ya ukumbi,
waandishi wa habari wakamfuata kiongozi huyo, ili atoe ufafanuzi.
Akizungumzia madai yao nje ya ukumbi wa Bunge, Mbowe alisema kambi
hiyo, haitachangia chochote kwenye mjadala wa Waziri Mkuu ila
hawataondoka bungeni.
Katika kile kinachodhihirisha mpango huo ulikuwa umeandaliwa ili
kuwavuruga Spika Ndugai au Naibu Spika Tulia Ackson, Mbowe alieleza
kushangazwa kuona viongozi hao kutokuwepo na badala yake Chenge, ambaye
ni Mwenyekiti wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa zamani kukalia kiti cha
Spika.
“Hatutaondoka bungeni ila tumekubaliana hatutachangia chochote kwenye
wizara hii hadi pale ufumbuzi wa madai yetu utakapopatikana. Kwanza
tunashangaa, tulijua anayeongoza kikao jioni hii ni Spika au Naibu Spika
ila wamemuweka Mwenyekiti Chenge ambaye anajua Sheria ili atuvuruge,”
alisema Mbowe.
Akifafanua madai yao aliyowasilisha bungeni alisema Sheria ya mwaka
1980 ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mawaziri kifungu cha 5 (1) inaweka
masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa
majukumu ya Serikali yake na kuutangaza katika gazeti la Serikali.
Majipu yawagusa.
Alidai mpaka sasa Serikali inafanya kazi bila kuwa na mwongozo wa
utendaji wa kazi kwa wizara mbalimbali na kwamba hiyo ina maana kuwa
Serikali inafanya kazi kwa kauli za Rais na mawaziri, ndio maana
kinachoonekana ni mambo ambayo hayaeleweki ya utumbuaji majipu kwa kuwa
Serikali haifuati mwongozo wowote wenye msingi na uhalali wa kisheria.
Madai hayo ya Mbowe si mapya, kwani alianza kuyatoa mwishoni mwa
Februari mwaka huu, ambapo wakati huo alionya alichoita fukuza fukuza ya
watumishi wa umma bila utaratibu, huku akiomba viongozi wa dini
kumsaidia kukemea.
Mbali na Mbowe, katika kile kilichoonekana kuwa hawaridhishwi na
utumbuaji majipu, aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa,
mwanzoni mwa mwezi huu, alirejea kauli hiyo ya Mbowe, kwa namna
nyingine.
Lowassa yeye alidai kuwa utumbuaji majipu umesababisha hali mbaya ya
maisha kwa wananchi, kwa kuwa watumishi hao wa umma wameachishwa kazi.
Mgombea huyo alienda mbali zaidi na kudai kuwa, anasononeshwa anapoona
watu wanaachishwa kazi katika mashirika ya umma.
Sh bilioni 6
Akizungumzia madai ya Serikali kuvunja Katiba na sheria kuhusu Bunge
la Bajeti, Mbowe alidai Serikali imekiuka Katiba kwa kutumia fedha
ambazo hazikuidhinishwa na Bunge na kusema jambo hilo linaua dhana ya
madaraka ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri Serikali.
Mbowe katika hilo, alikuwa akizungumzia Sh bilioni 6, ambazo Bunge la
Jamhuri ya Muungano katika kumuunga mkono Rais Magufuli, liliziokoa
baada ya kubana matumizi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo posho, safari
za nje na viburudisho na kuzikabidhi kwa Rais Magufuli.
Tayari Rais Magufuli alishaagiza fedha hizo zitumike kununua madawati
kwa kila jimbo. Madai mengine ni yale ya Bunge kusitisha kuonesha
shughuli za Bunge hilo moja kwa moja kwenye televisheni mbalimbali na
hivyo kuwanyima uhuru wananchi wa kufuatilia.
Akizungumzia hoja hiyo, Mbowe alimuomba Rais Magufuli kuingilia kati ili matangazo ya Bunge yarejee kama ilivyokuwa awali.
“Tunamuomba Rais Magufuli aingilie kati suala hili kwa sababu na yeye
ana nguvu kisheria ya kuzungumzia hilo. Aseme kama ni yeye aliyetoa
amri ya Bunge kutooneshwa live, basi aone haja ya kuamua matangazo hayo
yarejee kwa manufaa ya umma,” alisema Mbowe.
Chanzo HbariLeo.
Friday, 22 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment