Saed Kubenea |
Kubenea amehukumiwa ad habu hiyo jana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumtia hatiani katika kosa la kumtukana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Thomas Simba alikubaliana na ombi la mshitakiwa huyo na kumhukumu adhabu ya kukaa nje miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hilo.
“Nakubaliana na maombi ya mshitakiwa aliyotoa mahakamani hapa, hivyo anastahili kupewa adhabu ya huruma na mahakama inampa adhabu ya kukaa nje kwa muda wa miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hili,” alisema Hakimu Simba.
Pamoja na adhabu hiyo, mshitakiwa Kubenea pia atasaini karatasi ya mahakama ambayo inaonesha kukubali kwa adhabu hiyo. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Simba alisema mshtakiwa huyo ametiwa hatiani baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wa mashahidi watatu kutoka upande wa mashitaka waliotoa mahakamani hapo.
Alisema katika ushahidi wake, shahidi namba moja katika kesi hiyo, Makonda alidai Desemba 14, 2015 katika kiwanda cha TOOKU Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External, Kubenea akimtolea lugha chafu kuwa ni kibaka, mjinga, mpumbavu na kwamba nafasi yake ni ya kupewa.
Alisema baada ya kuchunguza ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imethibitisha pasi na kuacha shaka kuwa maneno hayo yangeleta uvunjifu wa amani, na hivyo mahakama ilimtia hatiani kwa lugha ya matusi.
Hata hivyo upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Mtalemwa Kishenyi ulidai mahakamani hapo kuwa hauna kumbukumbu za nyuma kuhusu hatia za mshtakiwa.
Kabla ya kupewa kwa adhabu hiyo, Kubenea aliiomba mahakama hiyo impe adhabu nafuu, ambayo itamfanya aendelee kuhudumia wananchi wake. Kubenea alijitetea kuwa bado wananchi wake wanahitaji awahudumie kwa kuwa ni mbunge wa Ubungo na pia upande wa Jamhuri, umekiri kuwa hana rekodi ya mashtaka, hivyo aliomba mahakama hiyo impunguzie adhabu.
“Mimi nilienda katika kiwanda hicho kwa ajili ya kutatua mgomo uliokuwepo baina ya wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho na kulikuwa hakuna uvunjifu wa amani kama jinsi ilivyoripotiwa, ” alidai Kubenea na kuongeza; “Naiomba mahakama yako inipe adhabu nafuu ambayo nitaweza kuwatumikia wananchi wangu.”
Hata hivyo kutokana na maombi hayo , hakimu Simba alisema kesi kama hiyo, hukumu yake inaweza kuwa ni faini au kwenda jela bila faini au mahakama inaweza kumuachia bila masharti yoyoye .
Chanzo HabariLeo
0 comments:
Post a Comment