Mwanasiasa machachari wa upinzani kutoka Zanzibar, Juma Duni Haji ambaye
alikuwa mgombea mwenza wa aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka
jana kupitia Chadema, amerejea katika chama chake cha CUF.
Duni
amerejea CUF ikiwa imepita miezi takribani tisa tangu alipojiunga na
Chadema ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akizungumza mara baada ya kumalizika
kwa mkutano wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad na
waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Duni alisema:
“Nimerudi nyumbani
CUF na Chadema nilikwenda ili kutimiza matakwa ya kikatiba kwa kuwa
mgombea mwenza wa urais lazima atoke upande wa pili wa Muungano. Hiyo ni
kwa mujibu wa matakwa ya Katiba yetu.”
Mara baada ya Lowassa
kupitishwa na Chadema na Ukawa kuwa mgombea wa urais, Duni ambaye
alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na Waziri wa Afya wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) alionekana kuwa na sifa ya kuwa mgombea mwenza
na hivyo kupewa kadi ya Chadema.
Mwanasiasa huyo amekuwa na
historia ndefu na mara tatu amewahi kuteuliwa na CUF kuwa mgombea mwenza
wa urais wa Jamhuri ya Muungano, akiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa chama
hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Jana, Duni alikuwa miongoni mwa
viongozi wa CUF waliokaa meza kuu na Maalim Seif wakati Katibu Mkuu
huyo akieleza mwelekeo wake na wa chama hicho baada ya kususia uchaguzi
wa marudio Zanzibar uliofanyika Machi 20, mwaka huu.
Akieleza
uamuzi wake huo Duni alisema: “Sioni ajabu yoyote mimi kurudi CUF. Kwa
nini nibaki Chadema? Siwezi kubaki kwa sababu kule nilikwenda kwa ajili
ya makubaliano tu.”
Huku akionekana kutotaka kueleza uamuzi wake
huo kiundani, Duni alisema pamoja na kuwa amerejea CUF, ushirikiano wa
chama hicho pamoja na vingine vinavyounda Ukawa vya Chadema, NCCRMageuzi
na NLD, uko palepale.
Akieleza jinsi CUF walivyompokea, Naibu
Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema ni
faraja kubwa kwa mwanasiasa huyo kurejea nyumbani.
“Jana (juzi)
saa 10.30 jioni katika tawi la CUF la Kibeni lililopo katika Wilaya ya
Kaskazini Unguja jimbo la Mkwajuni ndipo Duni alipofanyiwa hafla fupi ya
kukaribishwa tena katika chama chetu na kupewa kadi,”alisema Mazrui.
“Alirejesha
kadi ya Chadema na kuchukua na CUF. Tunamkaribisha sana na tunampongeza
kwa kuiwakilisha vyema Chadema na Ukawa katika Uchaguzi Mkuu.”
Mazrui
alisema si jambo la ajabu kwa mwanasiasa huyo kurejea CUF kwa sababu
awali alikuwa katika chama hicho ila aliondoka kwa ajili ya kwenda
kutimiza matakwa na ushirikiano ndani ya Ukawa.
“Ndani ya Ukawa
lengo letu ni moja wala hilo lisikufanye ukafikiri tofauti... usidhani
kuwa kuna tofauti yoyote eti kwa sababu ya uamuzi huu wa Duni,” alisema
Mazrui.
Credit Mpekuzi Blog kwenye simu yako
0 comments:
Post a Comment