Wizara
ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa
imejipanga kuwapeleka kwenye Balozi zake nje Watumishi wapatao 105 na
kuwarejesha nchini wengine 79 ambao miongoni mwao muda wao wa utumishi
balozini (Tour of Duty) umemalizika na wengine kustaafu kwa mujibu wa
sheria za Utumishi wa Umma. Kwa kawaida tour of duty kwa Watumishi nje
ni ya muda wa miaka minne (4).
Tanzania
ina Balozi 35 nje ya nchi ambazo kwa ujumla wake zina Watumishi 234.
Miongoni mwa Watumishi watakaorejea nchini wamo Mabalozi, Maafisa,
Wahasibu na Makatibu Muhtasi.
Hadi
sasa Mabalozi waliorejea nchini ni watatu (3) ambao ni Balozi Peter
Kalaghe aliyekuwa Uingereza, Balozi James Msekela aliyekuwa Italia na
Balozi Batilda Burian aliyekuwa Japan.
Itakumbukwa
kuwa, Januari 25, 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja
Mabalozi hao ambao mikataba yao iliisha na wengine kwa ajili ya
kupangiwa majukumu mengine.
Aidha,
jumla ya Watumishi tisa wa kada mbalimbali waliokuwa Balozini
wamerejea nchini hadi sasa na wengine wanaendelea kurejea kulingana na
upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha jukumu hilo.
Utaratibu
wa kuwapeleka na kuwarejesha Watumishi Balozini ni wa kawaida na upo
duniani kote kwa mujibu wa sheria za kimataifa ukiwemo Mkataba wa Vienna
unaotoa mwongozo kwenye masuala ya kidiplomasia.
Wizara itaendelea kupeleka Watumishi wenye sifa na tija kwa taifa ili kuiwakilisha nchi kikamilifu.
WAKATI HUOHUO,
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Oman Mhe. Dkt. Ali Bin Masoud Al
Sunaidy alifanya ziara ya kikazi nchini Tanzania kuanzia tarehe 12
April hadi 14 April, 2016.
Lengo
la ziara hiyo lilikuwa ni kushiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji
baina ya Tanzania na Oman, kongamano hili lilikuwa na kauli mbiu ya ‘’
Oman Tanzania Road show : Exploring Opportunities in Investment and
Business between Tanzania and Oman’’.
Ziara
na kongamano hili imelenga zaidi katika sekta za Madini, Kilimo na
uboreshaji wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Miundombinu na Mawasilisno,
Uvuvi, Usafirishaji, Utalii, Petroli na Gesi. Mgeni Rasmi katika
kongamano hili alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan
Katika
ziara hii, Mhe. Waziri Al Sunaidy aliongozana na ujumbe wa watu 108
ambapo 12 walikuwa ni Maafisa kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali ya
Oman na wengine waliobaki kutoka Sekta Binafsi kutoka nchi hiyo kwa
lengo la kukutana na Taasisi kama hizo hapa nchini.
Kwa
upande wa Tanzania wafanyabiashara 190 walishiriki na wenzao kutoka
Oman katika kongamano na baadae katika mikutano ya ana kwa ana (Business
to Business meetings).
MAFANIKIO YA ZIARA
1.Wakati
wa ziara hiyo, Tanzania na Oman zilisaini mkataba wa makubaliano ya
ushirikiano baina ya Tanzania Chambers of Commerce na Oman Chambers of
Commerce wa kuanzisha Kampuni ya Oman Tanzania Investment Company
(OTIC). Kampuni imeanzishwa kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji
Tanzania na Oman na imeazimia kuanza na mtaji wa Dola za Marekani
milioni 25 ambazo zitatumika kutoa mikopo kwa wawekezaji ;
2.Serikali
ya Oman imeonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha Sukari cha Kagera
(Kagera Sugar) na kukipa uwezo wa kuzalisha tani 400,000 ambazo zitauzwa
katika soko la Tanzania. Uzalishaji huu pia utahusisha uzalishaji wa
Umeme, spiriti na hamira itokanayo na mabaki katika kuchakata sukari.
Umeme utaingizwa katika gridi ya Taifa wakati spiriti ambayo ni muhimu
katika matumizi ya tiba itauzwa katika masoko ya ndani na nje ya
Tanzania. Aidha, Oman inahitaji hamira ambayo inahitajika kwa kiasi
kikubwa nchini humo na nchi zingine za mashariki ya kati ;
3.Mbali
na uzalishaji wa sukari, Serikali ya Oman pia inakusudia kuingia ubia
na Kagera Sugar katika kilimo cha umwagiliaji cha uzalishaji wa mazao ya
chakula kwa ajili ya matumizi ya Oman na Tanzania. Utekelezaji wa
miradi hii utaleta faida kwa Tanzania ikiwa ni kuongeza uzalishaji wa
sukari na hivyo kupunguza pengo kati ya uzalishaji na mahitaji halisi ya
sukari, lakini pia unategemea kuzalisha nafasi zaidi ya 5,000 za ajira
na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira ;
4.Serikali
ya Oman pia ilionyesha nia yake ya kuangalia uwezekano wa kuwekeza
katika mradi wa uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Tanga lakini pia
kuziwezesha bandari za Tanzania kuwa na ushirikiano na zile za Oman ;
5.Wawekezaji
kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za
kisasa mkoani Mtwara ili kuondoa tatizo la makazi stahili kwa watendaji
wakuu wa makampuni ya mafuta na shughuli zinazoendana na sekta hii ambao
hulazimika kila siku kusafiri kwa ndege kutoka Dar Es Salaam kwenda
Mtwara na kurudi jambo ambalo lina gharama kubwa pamoja na ombi la ekari
1,000 kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga na maua;
6.Wawekezaji
kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika maeneo kadhaa
ikiwemo uzalishaji wa mitamba na chakula cha mifugo huko Mivumoni,
Tanga, ranchi na machinjio ya Ruvu, miundombinu na viwanja vya ndege,
ujenzi wa nyumba za kisasa Kigamboni na Zanzibar pamoja na miradi
mingine katika sekta ya utalii pamoja na kuwekeza katika sekta ya
viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo ;
7.Wafanyabiashara
wa Tanzania wamepata nafasi ya kutambua fursa zilizopo Oman ikiwa ni
pamoja na upatikanaji wa soko kwa bidhaa za chakula kama vile matunda,
nyama, unga, sukari, hamira nk; na
8.Tanzania
kwa ujumla ilinufaika kwa kutangaza fursa za uwekezaji ambazo zipo
katika sekta zinazolengwa na wawekezaji wa Oman lakini pia kubaini fursa
zilizopo Oman ambazo wafanya biashara wa Tanzania wanaweza kunufaika
nazo pamoja na kuwaunganisha wafanya biashara wa Tanzania na wenzao wa
Oman katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu.
Hivyo,
utekelezaji wa matarajio haya unategemea kuongeza ajira, kuongeza ubora
na thamani ya mazao ya kilimo na kutanua wigo wa masoko kwa bidhaa za
Tanzania na pia kukuza sekta ya viwanda nchini.
Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment