1.0 Mnamo tarehe 09/4/2015
ulifanyika mgomo wa madereva nchini uliohusu malalamiko na kero mbalimbali
za madereva.
Katika kuzipatia ufumbuzi kero hizi, tarehe 02/5/2015 aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda, aliunda Kamati ya Kudumu ya Kutatua Kero na Changamoto mbalimbali katika Sekta ya Usafirishaji.
Kamati hiyo
inaundwa na Wajumbe kutoka Serikalini,
Umoja wa Madereva na Vyama vya Madereva, Vyama vya Watumiaji wa
Huduma za Usafiri, pamoja na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji. Kutokana
na vikao vilivyofanywa na Kamati hiyo kero na changamoto mbalimbali
zilibainishwa na kufanyiwa kazi. Baadhi zimefanyiwa kazi na kukamilishwa;
nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi ili kukamilishwa na nyingine zitaendela
kufanyiwa kazi kwa kuwa ni masuala endelevu.
2.0 Kwa kipindi chote cha
utekelezaji wa hatua za kutatua kero na changamoto hizo, kumekuwa na utoaji wa
taarifa mbalimbali miongoni mwa wadau kuhusu utendaji na hatua zinazochukuliwa
na Kamati. Taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kinyume na mamlaka na taratibu
zilizokubaliwa na Kamati na zimekuwa zikipotosha umma juu ya usahihi wa hatua
na hali halisi ilivyo.
Utaratibu huo umekuwa ukisababisha madhara mbalimbali
ikiwemo matishio ya migomo miongoni mwa madereva, taharuki miongoni mwa
watumiaji huduma na hasara mbalimbali kwa kutokuwepo kwa uhakika wa huduma kwa
siku husika.
3.0 Tarehe 01 Aprili,
2016 Kamati ilifanya kikao kilichowajumuisha Mhe. Jenista Mhagama (MB), Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu; Mhe. Harrison Mwakyembe (MB), Waziri wa Katiba na Sheria; Mhe. Mhandisi
Edwin A. Ngonyani (MB), Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi; Mhe.
Anthony Peter Mavunde (MB), Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana na
Ajira; Mwakilishi wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mwakilishi wa
Waziri, Wizara ya Mambo ya Ndani.
Katika kikao hicho, iliazimiwa kuwa Kamati,
kwa kushirikisha wawakilishi wa pande zote, itoe taarifa kwa umma juu ya hatua
zilizochukuliwa na mwelekeo uliopo.
4.0 Hivyo, Kamati inapenda
kutoa taarifa kwa wadau wote wa sekta ya
usafirishaji na wananchi kwa ujumla kwamba,
kufuatia hoja za vikao mbalimbali vya Kamati
ya Kudumu na Kamati Ndogo
vilivyofanyika kati tarehe 12/5/2015 na 01/04/2016, hatua zifuatazo zimechukuliwa:
4.1 Kuhusu kuendelea kutumia mizani ya Kibaha ili kupunguza
muda unaotumiwa na mabasi katika mizani ya Vigwaza; Serikali ilifunga Mzani
wa Kibaha kutokana na sababu za msingi. Hatua za kuimarisha huduma na kuondoa
tatizo la msongamano kwenye mzani wa Vigwaza zimechukuliwa. Hivyo, hoja hii imefungwa
na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.2 Kuhusu kushughulikia malalamiko ya wadau juu ya matuta ya
barabarani; Serikali
imeanza taratibu za kuyaboresha matuta ili yasilete madhara na inaangalia
uwezekano wa kuyaondoa matuta yote katika barabara kuu na kuweka alama za
vivuko (Zebra) kama inavyoelekezwa na Sheria. Utekelezaji unaendelea na hoja
hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.3 Kuhusu kutoa elimu juu ya matumizi ya mizani inayowezesha
gari kupimwa katika mwendo; Hoja imezingatiwa; elimu imeshaanza na
inaendelea kutolewa kwa njia mbalimbali za mawasiliano kwa umma, ikiwamo mabango
yaliyopo eneo la Vigwaza, vipeperushi kwa Madereva, vipindi vya TV na Redio. Hivyo,
hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.4 Kuhusu kuanzisha utaratibu wa kupima magari bila gharama
katika eneo la bandarini kabla ya safari ili kuwawezesha wasafirishaji
kuzingatia Sheria kwa kutozidisha uzito; Fedha kwa ajili ya kazi hii zimetengwa
katika Mwaka wa Fedha 2015/16, Usanifu umekamilika na taratibu za kumpata
mkandarasi wa ujenzi zinaendelea. Hivyo, hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele
ya Kamati kwa sasa.
4.5 Kuhusu kutoa taarifa ya maandishi kwa umma kuhusu maamuzi
ya kutohitaji vibali kwa ajili ya kuondoa magari mabovu na yaliyopata ajali
njiani; Maelekezo
yametolewa kwa TANROADS ili vibali visihitajike wakati wa hali ya dharura. Iwapo
ajali imetokea au gari limeharibika na kufunga barabara, magari husika yaondolewe
na kuyaweka mahali ambapo hayataleta usumbufu kwa watumiaji wengine. Hatua
baada ya hapo ni lazima zizingatie taratibu na matakwa ya Sheria. Upatikanaji
wa vibali hivyo utarahisishwa zaidi baada ya kuzindua utaratibu wa kupata
vibali kwa mtandao (e-permit). Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wameagizwa
kuleta taarifa ya utekelezaji katika kikao kijacho.
4.6 Kuhusu kufanya ukaguzi wa barabara ili kubaini ubovu na
mahitaji ya alama katika maeneo mbalimbali na kuyafanyia kazi; Hoja imezingatiwa na
kutekelezwa. Ukaguzi unaendelea kufanyika na alama za barabarani zinawekwa
sehemu stahili. Hivyo, kwa kuwa utekelezaji wa hoja hii ni endelevu, Kamati
imeagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi iendelee kutoa taarifa katika
kila kikao, kuhusu maeneo yaliyokarabatiwa na yaliyobaki.
4.7 Kuhusu wadau kutoa taarifa kuhusu maeneo yanayopaswa kuwa
na alama za barabarani; Wadau wamewasilisha taarifa kuhusu mahitaji ya alama za
barabarani zinazostahili kwenye maeneo ya Mlima Sekenke, Iguguno Shamba na Mkoa
wote wa Singida; na pia kona zote za Iyovi mkoani Morogoro.
Utafiti
umefanywa na Wizara ya Ujenzi na kubaini kwamba, jumla ya alama 156 za
barabarani zinahitajika kwa mkoa wa Singida. Kwa awamu ya kwanza jumla ya alama
80 zimewekwa kwenye maeneo husika. Utekelezaji unaendelea na Wizara hiyo
imeelekezwa kutoa taarifa ya maendeleo katika vikao vijavyo.
4.8 Kuhusu kukamilisha ubadilishaji wa aina ya malighafi
(materials) itumikayo katika kutengeneza alama za barabarani ili kuzuia kuibiwa
kwa alama hizo kwa ajili ya chuma chakavu; Hatua za kubadilisha mali ghafi na
kuweka alama za zege kulingana na mahitaji ya eneo husika unaendelea. Hatua za
utekelezaji wa zoezi hili zimeanza na pia ni endelevu.
4.9 Kuhusu kufanya marejeo (review) ya Sheria na Kanuni ili
malipo katika mizani yafanywe pia kwa fedha za Kitanzania; Kamati imeagiza TANROADS
kwamba, kwa kuwa ukarabati wa barabara zinazoharibiwa kwa kuzidisha uzito
hufanyika kwa dola, malipo ya faini yaendelee kufanywa kwa dola kama
inavyoelekezwa na Sheria au kwa fedha za kitanzania kwa kuzingatia viwango
halisi vya ubadilishaji fedha vinavyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania wakati wa
malipo hayo. Hivyo, hoja hii ya kutaka kurekebisha Sheria imefungwa na
kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.10 Kuhusu wamiliki wa daladala na Jeshi la Polisi kukutane
ili kujadili na kukubaliana utaratibu wa utakaotumika katika kufanya ukaguzi wa
kawaida wa daladala na kuteua maeneo maalum kwa ajili ya kaguzi hizo; Kikao kati ya Jeshi
la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na Wamiliki wa Daladala na
kuwashirikisha pia madereva, kilifanyika tarehe 05/06/2015. Utaratibu
umekubalika na maeneo ya kufanyia kaguzi yamebainishwa. Hoja imefungwa, lakini
Jeshi la Polisi limeagizwa kuendelea kushirikisha wadau mara kwa mara na kuwasilisha
taarifa katika kikao kijacho juu ya utekelezaji wa zoezi la ukaguzi kama
ilivyokubaliwa.
4.11 Kuhusu kuimarisha usimamizi wa Sheria na matumizi ya
ratiba na batli; Maelekezo
yametolewa kwa Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa (RTO’s) na usimamizi
umeimarishwa. Hatua za utekelezaji zinaendelea na hoja hii imefungwa na
kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.12 Kuhusu kutoa elimu kwa umma kuhusu utoaji wa taarifa za
vitendo vya rushwa vinavyohusisha askari wa usalama barabarani; Elimu juu ya kutoa
taarifa za rushwa inaendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari kama Redio na
Televisheni. Vipeperushi kuhusu rushwa vimeandaliwa na kusambazwa. Uelimishaji
umma unaendelea kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano kwa umma. Hatua za
utekelezaji ni endelevu na Jeshi la Polisi limeagizwa kuendelea kushirikisha
wadau ili kuweka mikakati ya kupata taarifa za vitendo vya rushwa.
4.13 Kuhusu kufuatilia kukamilishwa kwa Kanuni zitakazo
wezesha malipo ya faini kufanywa kwa njia ya mtandao; Kanuni zimekamilishwa
na Mfumo umeanza kutumika kwa majaribio katika mkoa wa Dar es salaam. Hatua za
utekelezaji zitaendelea kwa mikoa yote. Jeshi la Polisi limeagizwa kufanya
vikao vya ushirikishaji wadau mara kwa mara. Hoja hii imefungwa na kuondolewa
mbele ya Kamati kwa sasa.
4.14 Kuhusu kuainisha masuala yatakayozingatiwa katika ziara
ya mafunzo kwa wajumbe wa Kamati katika nchi jirani; Rasimu ya masuala ya
kuzingatiwa bado inafanyiwa kazi. Kamati imeagiza Sekretarieti ifuatilie maoni
kutoka TATOA na kushirikisha Vyama vingine vya wamiliki. Hatua za utekelezaji ni
endelevu.
4.15 Kuhusu kushirikiana na Halmashauri ili kuteua vituo kwa
ajili ya pikipiki hasa katika mkoa wa Kigoma; SUMATRA imeanza
utekelezaji kwa kutuma mtaalam mkoani Kigoma kwa ajili ya kusimamia zoezi la
kuainisha vituo vya pikipiki na bajaji katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji. Hatua
za utekelezaji ni endelevu. Kamati imeagiza utekelezaji uendelee na hoja hii
imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.16 Kuhusu kufuatilia kukamilishwa kwa Kanuni
zinazotenganisha makosa ya madereva na wamiliki zilizowasilishwa kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Ufuatiliaji umefanywa katika Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Rasimu ya Kanuni hizo imeboreshwa na kuwasilishwa
tena kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua za mwisho kabla ya kutolewa na
kuanza kutumika. Kamati imeagiza Kanuni hizo kukamiliswa haraka, taarifa
itolewe na mawasilisho yafanywe katika kikao kijacho. Hoja hii imefungwa na
kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.17 Kuhusu kufanya utafiti wa mahitaji ya huduma za
usafirishaji katika njia kuu; Utafiti umefanywa kwa kushirikisha Chama cha
Wamiliki wa Mabasi (TABOA) katika njia za Dar-Mbeya, Dar-Mwanza na Dar-Arusha;
na taarifa inakamilishwa. Kamati imeagiza SUMATRA kuwasilisha taarifa ya
matokeo ya utafiti katika kikao kijacho. Hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele
ya Kamati kwa sasa.
4.18 Kuhusu kufanya utafiti wa mahitaji ya huduma za
usafirishaji katika njia zinazohudumiwa na Daladala katika Jiji la Dar es
Salaam; Utafiti
utafanywa katika robo ya mwisho wa mwaka wa fedha wa 2015/2016. Hatua za
utekelezaji zinaendelea na hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa
sasa.
4.19 Kuhusu kutoa leseni za usafirishaji kwa maombi mapya kwa
ratiba za magari ya kuanzia saa 1.30 asubuhi na kuendelea; Utekelezaji umeanza
kwa magari ya abiria yanayoomba leseni kwa mara ya kwanza. Hatua za utekelezaji
wa zoezi hili ni endelevu. Kamati imeagiza wadau kuwasilisha hoja mpya katika
kikao kijacho, kama zipo, kuhusiana na suala hili. Hoja hii imefungwa na
kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.20 Kuhusu kuwasilisha mapendekezo kwa mwakilishi wa Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji juu ya sekta zinazoweza kuendeshwa na wazawa
kwa ufanisi ili kuzingatiwa katika mchakato wa kutengeneza Sera ya usafirishaji
kwa ajili ya wawekezaji wa ndani (Local Content Policy); Serikali imeanza
kulifanyia kazi suala hili kwa pamoja na sekta nyinginezo chini ya uratibu wa
OWM-Uwezeshaji. Hatua za utekelezaji ni endelevu.
4.21 Kuhusu kufuatilia matumizi ya pikipiki, bajaji na magari
aina ya Probox (michomoko) katika Mikoa ya Iringa na Kigoma; Ufuatiliaji umefanywa
na SUMATRA. Vikao vya mashauriano na wadau vinaendelea. Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi imetoa maelekezo juu ya utatuzi wa suala hili. Kamati
imeagiza SUMATRA kutoa taarifa kwa umma juu ya hatua zake na kutoa mrejesho
katika kikao kijacho juu ya utekelezaji wa maelekezo ya Wizara. Hoja hii
imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.22 Kuhusu kuanzishwa kwa jukwaa (forum) la wadau wa
usafirishaji kwa barabara; SUMATRA inaandaa mpango wa namna ya kuanzisha jukwaa hili
katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2015/2016. Hatua za utekelezaji
zimeanza na zinaendelea.
4.23 Kuhusu wadau kushirikishwa katika kuelewa utaratibu wa
ukokotoaji nauli kwa mujibu wa Kanuni; Wadau wameshirikishwa katika utafiti wa hali
ya mahitaji ya huduma za usafirishaji (occupancy ratio) katika njia kuu za
mabasi ya mikoani ambao upo katika hatua za mwisho za kukamilishwa taarifa.
Ushirikishwaji zaidi utafanyika kupitia mafunzo ya ukokotoaji yatakayofanyika
ndani ya Robo ya Mwisho wa Mwaka wa fedha 2015/2016. Hatua za utekelezaji zitaendelea
kwa daladala.
4.24 Kuhusu kuharakisha ununuzi wa mitambo ya TBS ya ukaguzi
wa ubora wa matairi na vipuri; Utaratibu wa ununuzi wa mitambo unaendelea na
bajeti imetengwa kwa mwaka 2015/2016. Hatua za utekelezaji zimeanza na
zinaendelea.
4.25 Kuhusu kutoa elimu kwa umma juu ya utambuzi wa bidhaa
zisizo na ubora na hatua za kuchukua, hususani kuhusu matairi ya magari na
vipuri; TBS
imekuwa ikitoa elimu kwa njia mbalimbali za mawasiliano kwa umma. Hatua za
utekelezaji zimeanza na zoezi hili ni endelevu. Kamati imeagiza Mkurugenzi wa
TBS awasilishe taarifa katika kikao kijacho juu ya hatua na mikakati ya ukaguzi
hapa nchini na katika nchi ambazo TBS haina vituo/wakala wake wa ukaguzi na
namna ya kuzuia Tanzania kuwa dampo la bidhaa zisizo na viwango.
4.26 Kuhusu kushirikisha sekta binafsi ikiwemo TATOA ili
kuwekeza katika vifaa vya ukaguzi wa ubora wa matairi na vipuri; Jukumu la ukaguzi wa
viwango vya ubora wakati wa uingizaji bidhaa ni la serikali kupitia TBS. Hata
hivyo, watumiaji binafsi hawakatazwi kuwekeza katika kufanya uhakiki wa bidhaa
zao baada ya uingizaji huo. Hatua za utekelezaji ni endelevu.
4.27 Kuhusu agizo la Kamati kuwa tarehe 20 Agosti 2015, Kamati
itembelee mizani ya Vigwaza ili kupata hali halisi ya kero zinazolalamikiwa na
madereva na kuona namna ya kuzishughulikia; Kamati ilitembelea Mizani ya Vigwaza
tarehe 20/08/2015 kama ilivyoagizwa na mapendekezo ya maboresho yalitolewa
kupitia vikao vya Kamati. Uboreshaji umefanywa na hali ya huduma za mzani huo
inaridhisha. Agizo limetekelezwa na kukamilika; na hivyo hoja inafungwa na kuondolewa
mbele ya Kamati kwa sasa.
4.28 Kuhusu Sekretariati kutuma taarifa za mialiko ya vikao na
kusambaza Muhtasari mapema ili wajumbe waweze kujiandaa na vikao vijavyo; Maagizo yamezingatiwa
na kutekelezwa, kulingana na hali halisi inayojitokeza. Usimamizi wa suala hili
utaimarishwa. Hoja imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.29 Kuhusu Mamlaka husika (EWURA na WMA) kuwasilisha Mada
kuhusu changamoto na taratibu za upakiaji, usafirishaji na upakuaji wa mafuta; Mada ziliwasilishwa
na maelezo ya kitaalam kutolewa na wawakilishi wa EWURA, WMA na kampuni ya PUMA
katika kikao cha Kamati cha tarehe 11 Machi, 2016.
Kamati imeagiza EWURA na WMA
zifanye utafiti na kutoa taarifa ndani ya siku 60 kuhusu kasoro (shoti)
zinazolalamikiwa na wadau, hususani nchini Zambia. Wizara husika ziwasilishe
taarifa katika kikao kijacho.
4.30 Kuhusu Serikali kutoa ufafanuzi juu ya matumizi ya Mfumo
wa Kukata Nukta katika Leseni za Udereva; Ufafanuzi ni kwamba Mfumo wa ukataji
nukta katika leseni za udereva bado haujaanza kutumika. Pindi ukiwa tayari
taarifa itatolewa kwa umma.
Mfumo huo utatumika kwa kila mtu anayeendesha gari
kwa sekta zote, ikijumuisha madereva wa magari binafsi. Hivyo, wadau wameombwa
kupata uelewa sahihi kupitia ufafanuzi unaotolewa na Jeshi la Polisi mara kwa
mara kupitia vyombo vya habari, badala ya taarifa potofu zinazozagaa mitaani.
Hatua za utekelezaji wa hoja hii ni endelevu.
4.31 Kuhusu kukamilisha marekebisho na kuwasilisha mkataba wa
ajira ya madereva ulioboreshwa katika vikao vya Kamati; Mkataba ulioboreshwa
umekamilishwa na kuanza kutumika tarehe 01 Julai, 2015. Wadau walipatiwa nakala
ya mikataba na vitambulisho ili waanze kutumia katika sehemu zao za kazi.
Ukaguzi
ulibaini jumla ya mikataba 11, 133 ilitolewa kwa madereva hadi kufikia Desemba,
2015. Hata hivyo, zoezi la ukaguzi wa mikataba lilisitishwa kwa maombi ya
wawakilishi wa wafanyakazi kwamba, lisubiri kukamilika kwa majadiliano na
muafaka wa viwango vya posho ili vijumuishwe kwenye mikataba hiyo.
Hata hivyo, kwa
sasa ukaguzi utaendelea kwa mujibu wa Sheria baada ya wadau kuafikiana hivyo. Utekelezaji
wa hoja umekamilishwa na imeondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.31.1 Kuhusu Serikali kutoa tamko la kuweka viwango vya posho
kwa madereva; Vikao
vya majadiliano ya wadau yamekamilishwa na kuafikiwa kwamba majadiliano juu ya
suala la posho kwa madereva yafanywe kwa mujibu wa Sheria. Hivyo, Kamati imeagiza Vyama vya Wafanyakazi vitekeleze wajibu
wake kisheria kwa kufanya majadiliano na Vyama vya Waajiri au Mwajiri mmoja
mmoja katika maeneo yao ya kazi.
Kufanikisha
majadiliano hayo, Vyama vya Wafanyakazi ni lazima viandikishe wanachama kwa
asilimia zaidi ya hamsini ya wafanyakazi waliopo sehemu ya kazi ili vipate
uhalali wa kuwawakilisha katika majadiliano na mwajiri husika. Wafanyakazi nao
wajiunge na Vyama kwa mujibu wa Sheria za Kazi na kuzingatia taratibu za
kisheria ili waweze kudai haki, kufanya majadiliano na kupata haki ya kushiriki
migomo kwa utaratibu halali iwapo hakutakuwa na muafaka.
Kwa
upande mwingine, Waajiri wameagizwa pia kuzingatia Sheria kwa kuruhusu Vyama
vya Wafanyakazi kufanya shughuli zao katika maeneo yao ya kazi na kufanya
majadiliano kisheria ili kudumisha mahusiano mema baina yao, kukuza tija na
ufanisi.
Kamati
imeagiza Idara ya Kazi na SUMATRA kuimarisha kaguzi katika kampuni za
usafirishaji na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka
taratibu zilizowekwa juu ya masuala haya; ikiwemo kuchukua hatua dhidi ya
waajiri wasiolipa mishahara wafanyakazi wao au wanaolipa chini ya kima cha
chini cha kisheria, kuwashtaki wanaoghushi mikataba na kufuta leseni kwa wanaokiuka
masharti ya leseni hizo.
Kamati
imeagiza pia, Vyama vya Wafanyakazi viwasilishe mbele ya Kamati, orodha ya wamiliki
na madereva wanaokiuka Sheria ili mamlaka husika ziwachukulie hatua stahiki. Majina
hayo yatolewe kwa njia za siri kupitia mawasiliano na Afisa Kazi waliyetambulishwa.
Hivyo,
hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.32 Kuhusu kuhamasisha madereva kujiunga na Vyama vya Wafanyakazi
vilivyopo; Serikali
imewezesha kuundwa kwa vyama viwili vya wafanyakazi madereva ambavyo ni Chama
cha Wafanyakazi Madereva wa Malori Tanzania (CHAWAMATA) kilichosajiliwa tarehe
28/5/2015 na Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU) kilichosajiliwa
tarehe 25/6/2015. Uwepo wa Vyama hivyo,
pamoja na vile vilivyokuwepo awali, vya TAROTWU na COTWU (T), utawawezesha
Madereva kushiriki ipasavyo katika
majadiliano ya pamoja na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kwa lengo la
kuboresha maslahi na haki za madereva.
Vyama
hivi sasa vinawajibika kisheria kufuata taratibu za majadiliano sehemu za kazi
na kuzingatia matakwa ya Sheria na Katiba zao. Vyama husika vimelekezwa kufika
katika maeneo ya kazi na kutangaza sera zao kwa njia mbalimbali ili kuvutia
wanachama wapya na kuwa na nguvu za kisheria kuwawakilisha na kutetea maslahi
ya madereva.
Hivyo,
hoja hii imekamilishwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.33 Kuhusu Kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali kuhusu Sheria
za Kazi, haki na wajibu wa mfanyakazi na mwajiri; Mafunzo yalitolewa
kwa wajumbe wa Kamati, wajumbe wa TATOA na TABOA kwa nyakati tofauti kuanzia
tarehe 18 Mei, 2015. Uelimishaji umeendelea kufanywa kwa njia ya vyombo vya
habari na ushauri kwa wadau husika kulingana na mahitaji. Utekelezaji ni endelevu
na hoja hii inaondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.34 Kuhusu Serikali kutoa Tamko la kuongeza mishahara ya
madareva; Baada
ya kupata ufafanuzi wa kisheria, wadau waliafikiana kuwa suala la nyongeza ya
mshahara liachwe lishughulikiwe na Bodi za Mshahara kwa mujibu wa Sheria.
Uundaji wa Bodi za Mshahara za Kitaifa umeanza na upo katika hatua za mwisho.
Bodi hizo ndizo zitakazofanya utafiti kwa mujibu wa Sheria na kuboresha Kima
cha Chini cha Mshahara, Vigezo, Hali na Masharti ya Ajira kwa wafanyakazi wa Sekta
ya Umma na Binafsi. Madereva wanawakilishwa katika Bodi na watapata fursa ya
kutoa maoni yao yafanyiwe kazi huko na kukamilishwa mwanzoni mwa mwaka wa fedha
2016/17.
Hivyo,
hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.35 Kuhusu Serikali kufanya marekebisho ya Sheria za Kazi na
kuboresha kanuni ili kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mikataba na maslahi
ya madereva; Marekebisho
ya Sheria za Kazi, Na. 6 na 7 za mwaka 2004 yalikamilishwa na kupitishwa na
Bunge mwezi Julai, 2015.
Kanuni za Sheria za Kazi, Na. 6 na 7 za mwaka 2004
nazo zimeboreshwa na zinatarajiwa kukamilishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kabla ya kutiwa saini na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi na
ajira hivi karibuni. Aidha, hatua zinaendelea kufanya marekebisho mapya katika
Sheria za Kazi ili kuongeza nguvu za Maafisa Kazi kutoa adhabu za papo kwa papo
kwa wakiukaji.
Jambo hili litasaidia kutolewa kwa mikataba ya ajira na
uzingatiaji Sheria na taratibu za kutoa haki nyingine kwa wafanyakazi wote
wakiwemo madereva. Uwezekano unaangaliwa ili adhabu za papo kwa papo ziweze pia
kutolewa kwa wafanyakazi watakaobainika kutishia au kuitisha migomo kinyume cha
Sheria.
Hivyo,
hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
5.0
Hitimisho:
Serikali inatoa wito kwa
wamiliki wa vyombo vya usafirishaji,
viongozi wa vyama vya wafanyakazi madereva na madereva wote nchini kuzingatia
na kutekeleza makubaliano yaliyokwishafikiwa hadi sasa.
Pamoja
na juhudi za Serikali kutatua mgogoro wa ajira ya madereva nchini, kumekuwepo matishio
ya mara kwa mara ya kuitishwa migomo kwa madereva. Kamati inawakumbusha
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Madereva wote kuzingatia taratibu
za kisheria katika kufanya migomo mahali pa kazi, kama zilivyoainishwa katika
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na. 6 ya mwaka 2004. Kufanya migomo
kinyume cha utaratibu ni kuvunja Sheria na hatua stahiki zitachukuliwa kwa wale
wote watakaoitisha na kushiriki katika migomo hiyo.
Aidha,
Serikali itaendelea kutoa elimu na
kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa na hatua za kisheria zitaanza
kuchulikwa dhidi ya wale watakaokiuka utekelezaji wa makubaliano hayo na
matakwa ya Sheria kwa ujumla. Taarifa kwa umma zitaendelea kutolewa juu ya
hatua za utekelezaji.
IMETOLEWA NA:
Eric F. Shitindi
MWENYEKITI WA KAMATI
04/04/2016
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment