Jaribio la kutaka kumuondoa madarakani Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma
limegonga mwamba baada ya idadi ya kura zilizohitajika bungeni
kushindwa kutimia.
Wabunge walitaka kumng’oa Rais Zuma kufuatia
uamuzi wa Mahakama ya Rufani uliotolewa Alhamisi wiki iliyopita kuwa
kiongozi huyo alikiuka sheria kwa kutumia mabilioni ya fedha za umma
kukarabati makazi yake binafsi.
Upigaji kura ndani ya Bunge
ulihitaji theluthi mbili ya wajumbe ili kumng’oa kiongozi huyo. Chama
tawala cha African National Congress (ANC) kina idadi kubwa ya wabunge.
Katika
uamuzi wake, Mahakama ya Rufani iliamua kwamba Rais Zuma alikiuka
katiba kwa kushindwa kurejesha sehemu ya Sh2.4 bilioni za umma
alizotumia kukarabati makazi hayo yaliyopo eneo la Nkandla katika Mkoa
wa Kwa Zulu-Natal.
Rais Zuma alitumia fedha hizo kujenga bwawa la kuogelea, mabanda ya kuku na ng’ombe na chumba maalumu cha burudani.
Ripoti
iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Thuli
Madonsela mwaka 2014 ilifichua kuwa familia ya kiongozi huyo ilitumia
fedha hizo kinyume cha sheria. Thuli alimtaka rais kurejesha sehemu ya
fedha hizo.
Ijumaa iliyopita, Rais Zuma aliomba msamaha kupitia luninga
ya serikali, huku akisema amesikitishwa na kusononeshwa na sakata hilo.
Zuma alisema atarejesha sehemu ya fedha anazodaiwa kuzitumia kama
ilivyoagizwa na mahakama.
Hoja ya kutaka kumng’oa Rais Zuma
iliwasilishwa bungeni na chama kikuu cha upinzani cha Democratic
Alliance (DA). Viongozi wa upinzani walidai kuwa uongozi wake unafanya
kinyume na ule wa Mwasisi wa Taifa hilo, Nelson Mandela.
“Jacob
Zuma ni maradhi ya kansa ndani ya mioyo ya raia wa Afrika Kusini. Hafai
kamwe kuongoza taifa,” ulisema upinzani uliokuwa ukijibu hotuba ya rais
ya Ijumaa.
Baada ya Mahakama ya Rufani kutoa uamuzi wake ,
Kiongozi wa Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema alisema
upinzani hautamruhusu Rais Zuma kulihutubia tena bunge.
“Kuanzia
leo hatutamruhusu rais kuhutubia Bunge kwani tutamnyamazisha kwa nguvu.
Tutamfurusha bungeni kwa kuwa kuanzia sasa yeye siyo Rais wa Afrika
Kusini,” alisema Malema.
Vigogo wa ANC waliomsaidia Hayati
Mandela kuingia madarakani mwaka wa 1994, wamemtaka Rais Zuma kujiuzulu
ili kukiondolea fedheha chama hicho.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment