Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki |
AGIZO la Rais John Magufuli la kuwataka viongozi sehemu za kazi kuondoa watumishi hewa, limesaidia watumishi hewa 4,317 wa Serikali Kuu kufutwa baada ya kufanya uhakiki katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Machi mosi hadi Aprili 4, mwaka huu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki alisema jana kuwa idadi hiyo inafanya watumishi hewa ambao wameshatambuliwa kwenye mfumo wa malipo wa serikali kuanzia Januari mwaka huu hadi juzi kufikia 7,795 na walishalipwa Sh bilioni 7.6 tangu waache kuwa watumishi wa umma.
Kairuki alisema mishahara hewa ni tatizo kubwa na linatokana na baadhi ya maofisa utumishi wa idara na taasisi za Serikali kutokuwa waaminifu.
“Hili ni eneo ambalo tunatumia asilimia 51 ya makusanyo ya TRA kwa ajili ya mishahara ni lazima tatizo hili tuliondoe,” alisema Kairuki.
Alifafanua kuhusu watumishi hao kuwa kati ya watumishi hewa 4,317, waliobainika ndani ya mwezi mmoja, watumishi 3,033 waligundulika mara tu baada ya Rais John Magufuli kutoa tamko Machi 15.
Alisema baadhi ya watumishi hao walishafariki, wengine walishastaafu na wengine ni majina bandia yaliingizwa na wajanja ili wawe wanachukua mishahara yao.
Alisema kutokana na hali hiyo, ofisi yake imeagiza maofisa tawala wote wa idara za serikali kufanya uhakiki na kujua huyo mtumishi hewa kituo chake cha kazi kilikuwa kipi, kazi alizokuwa anafanya, tarehe ya kuajiriwa, kufa au kustaafu ama kufukuzwa kazi.
“Kasi hii ya kuondoa watumishi ambao utumishi wao umekoma, haijawahi kufikiwa kipindi cha nyuma ikionesha kuwa agizo la Rais limepata mwitikio mkubwa kwani kuanzia Aprili Mosi hadi juzi yaani ndani ya siku nne watumishi zaidi ya 1,284 walifutwa kwenye mfumo wa malipo ya serikali,” alisema Kairuki.
Waziri huyo alisema watumishi hao ni tofauti na watumishi 1,830 waliogundulika kwenye mikoa mbalimbali baada ya Rais kuwaagiza wakuu wapya wa mikoa kwenda kushughulikia tatizo hilo katika maeneo yao ya kazi.
Hata hivyo, alisema taarifa hizo za watumishi hewa wa kutoka mikoani zina kasoro nyingi, ikiwemo kutokuwepo majina ya watumishi walioondolewa katika mfumo wa malipo na pia dosari nyingine ni kutokuwepo kwa namba ya hundi ya mtumishi.
Alisema pamoja na kugundulika kwa watumishi hao hewa, ofisi yake imewaagiza waajiri wote wawe wamewasilisha taarifa zao wiki hii ili kuwezesha kujua kwa usahihi watumishi wangapi hewa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Alisema watumishi hao hewa wamefahamika kwa urahisi kutokana na serikali kutumia mfumo wa kisasa wa kufanyia malipo ya mishahara ujulikanao kama Lawson 9, alisema umejengwa katika hali ya kumwezesha mwajiri kumuondoa moja kwa moja katika orodha ya malipo mtumishi hewa bila kuidhinishwa na Utumishi.
Alisisitiza kuwa mwenye jukumu la kumuondoa mtumishi aliyefikia ukomo wa ajira ni mwajiri husika na siyo Wizara ya Utumishi.
“Hata hawa watumishi 4,317 wameondolewa katika orodha ya malipo kuanzia Machi Mosi mwaka huu hadi Aprili 4 bila kupata idhini ya Wizara ya Utumishi baada ya maofisa utumishi kufundishwa namna ya kutumia mfumo wa Lawson 9,” alifafanua waziri huyo wa Utumishi na Utawala Bora.
Alisema kutokana na uhakiki wa watumishi hewa unaoendelea kufanyika katika ofisi mbalimbali za umma, ameagiza wizara na idara zote kufunga mfumo wa malipo ya mishahara Aprili 12 badala ya tarehe tano ili kuhakikisha watumishi wote ambao hawastahili kuwepo kwenye orodha ya malipo ya mishahara wanafutwa.
“Baada ya tarehe hiyo ofisi yangu itafanya ukaguzi kwenye taasisi na mamlaka mbalimbali ili kuhakikisha kwamba wale wote ambao hawawajibiki au kutimiza wajibu wao katika eneo hili la usimamizi wa rasilimali watu wanachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema Kairuki.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment