Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe |
SIKU moja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), kudai kuna uvunjifu wa sheria katika uhamishaji wa fedha zilizoidhinishwa na Bunge, Tume ya Mipango imetoa ufafanuzi na kusema hakuna sheria iliyovunjwa.
Aidha, Mbowe na wabunge wa kambi ya upinzani wametakiwa kwenda kuisoma upya Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 ili waielewe badala ya kuupotosha umma.
Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kuzinduliwa kwa Kitabu cha Muongozo kuhusu wa Usimamizi Rasilimali za Umma, Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Mipango, Florence Mwanry alisema madai yaliyotolewa juzi na Mbowe bungeni si ya kweli.
“Wabunge ndio walipitisha wenyewe Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015, ambayo inafafanua kuhusu uhamishaji wa fedha kutoka kifungu kimoja kwenda kingine, hivyo uhamisho wa fedha uliofanywa uko sahihi na hakuna sheria iliyovunja, wakaisome vizuri,” alisema Mwanry.
Mbowe akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kususa Bunge, alitoa mfano wa bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa na Bunge kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2015/16, iliyokuwa ya Sh bilioni 883.8, ambapo kati ya fedha hizo, fedha za ndani zilikuwa ni Sh bilioni 191.6.
Alisema inashangaza kuwa hadi kufikia Machi 2016, Wizara ilikuwa imeshapokea kutoka Hazina Sh bilioni 607.4, ambazo ni fedha za ndani, tofauti na ilivyopangwa kuwa fedha za ndani ni Sh bilioni 191.6. Mbowe alidai kuwa hiyo inaonesha kuwa kuna ongezeko la fedha zilizotolewa na Hazina hadi kufikia Machi 2016, ikilinganishwa na fedha zilizoidhinishwa na Bunge.
Akitoa ufafanuzi, Mwanry ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Mipango, alisema Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015, inamruhusu Ofisa Masuhuli kuhamisha fedha kutoka kifungu kimoja kwenda kingine, ili mradi asivuke asilimia saba ya bajeti nzima.
Kadhalika, kwa upande wa Waziri, alisema sheria hiyo inampa uwezo wa kufanya uhamisho wa fedha kutoka kifungu kimoja kwenda kingine ili mradi asizidi asilimia 10 ya bajeti na katika uhamisho uliofanywa na wizara tajwa, mambo hayo yamezingatiwa.
“Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ni wizara yenye madeni mengi ya wakandarasi na ni moja ya wizara zinazotumia fedha nyingi kwenye masuala ya miundombinu, sasa ni lazima madeni hao yalipwe na Serikali haiwezi kuacha kuyalipa kwa sababu kadri yanavyobaki, ndivyo riba inavyoongezeka,” alisema Mwanry.
Alisema pamoja na uhamisho uliofanywa ndani ya wizara hiyo, bado fedha zilizohamishwa ziko ndani ya kiwango kinachotakiwa kisheria na bado ni kiwango kidogo ambacho hakijavunja sheria.
Chanzo habariLeo.
0 comments:
Post a Comment