Raisi John Magufuli.
MSAKO ulioanzishwa na Rais John Magufuli wa kutokomeza tatizo la
wafanyakazi hewa katika utumishi wa umma, umeendelea kuibua mazito,
ambapo mkoani Kilimanjaro, Benki ya CRDB imejikuta ikitoa mkopo kwa
waliokuwa wafanyakazi hewa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Helga Mchomvu aliyasema
hayo akidai kuwa, yamegundulika baada ya Serikali kuunda kamati za
uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh milioni 500 katika
halmashauri hiyo.
Kabla ya kuibuka kwa kisa hicho kinachoonesha namna wafanyakazi hewa
alivyokuwa wakiibia nchi, hivi karibuni mkoani Singida, Mhasibu wa
Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Imani Nyamangaro, alipandishwa
kizimbani akidaiwa kujilipa mishahara ya wastaafu 57, yenye thamani ya
Sh milioni 29.4.
Mbali na mhasibu huyo, Rais Magufuli alipokuwa mapumziko kijijini
kwake Mlimani, katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, alieleza kisa
kingine kilichoshitua jamii kuwa katika Mamlaka ya Mapato (TRA),
kulikuwa na mtumishi mmoja ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17.
Benki ya CRDB Hai
Akizungumza jana, Mchomvu alidai kuwa watumishi watatu wa halmashauri
hiyo; wawili wa Idara ya Utumishi na mmoja Mchumi, walikopa katika
Benki ya CRDB Sh milioni 35.2, kwa kutumia majina ya wafanyakazi hewa.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mkuu Idara ya Utumishi na Utawala,
Gudila Mashele, Ofisa Utumishi Daraja la Kwanza, Faraja Ndatu na Mchumi
Daraja la Pili, Isaiah Bayege. Kutokana na tuhuma hiyo iliyoibuliwa na
kamati hizo za uchunguzi, Mchomvu alisema Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Wilaya ya Hai, limewafukuza kazi watumishi hao.
Muda, dawa feki Mbali na tuhuma ya kujipatia mkopo kwa kutumia majina
ya wafanyakazi hewa, Mchomvu alisema kuna watumishi wengine wamefukuzwa
kazi kwa tuhuma za wizi wa fedha za muda wa kazi wa ziada wa madaktari
na wauguzi katika Hospitali ya Machame wilayani hapa, huku mwingine
akifukuzwa kwa kununua dawa hewa za hospitali hiyo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mhasibu Daraja la Kwanza, Edwin
Kalokola na Mhasibu Msaidizi, Valentina Elisha, wanaodaiwa kuiba Sh
milioni 24.4 za muda wa kazi wa ziada wa madaktari na wauguzi katika
hospitali hiyo.
Mbali na wahasibu hao, yupo pia dereva Derick Urassa, aliyefukuzwa
kwa tuhuma za kushiriki katika ununuzi wa dawa hewa katika hospitali
hiyo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 32.7. Walioshushwa cheo
Alisema wapo pia watumishi walioshushwa vyeo kutokana na tuhuma
mbalimbali, ikiwemo kughushi nyaraka na kuidhinisha malipo bila idhini
ya mwajiri.
Miongoni mwao ni pamoja na Ofisa Muuguzi Msaidizi Daraja la Kwanza,
Agness Chami na Katibu wa Afya Daraja la Kwanza, Gilbert Mashamba.
Wengine ni wahasibu waandamizi wawili, Kasisim Herpa na John Bogohe
na Mhasibu Daraja la Kwanza, Christopher Manzi, ambao wanatuhumiwa
kuidhinisha malipo mbalimbali ya Sh milioni 488.2, bila kuwa na idhini
kinyume na taratibu za kazi.
Walivyobambwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Saidi Mderu
alisema tuhuma hizo ziligunduliwa na Mkaguzi wa Ndani wa halmashauri
hiyo, Michael Mosha na kufanyiwa kazi na tume hizo zilizoongozwa na
Katibu Tawala Msaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, Grace
Makiluli.
Baada ya kubainika kwa tuhuma hizo, Mderu alisema baraza hilo
lilimpongeza mkaguzi huyo kwa kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa kwa kuwa
angeweza kudanganyika kutumia fedha hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa, amepongeza baraza hilo kwa
hatua hizo na kueleza kuwa kazi kubwa ya madiwani ni kusimamia mali na
rasilimali za Serikali, ili wananchi wapate huduma bora za Serikali yao
ya Awamu ya Tano ambayo ina dhamira ya kuwahudumia.
Chanzo HabariLEO
Saturday, 23 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment