CHAMA
cha ACT-Wazalendo Wilaya ya Shinyanga Mjini kimetamba kuwa kwenye
uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ndicho kitakuwa mpinzani mkubwa wa CCM
badala ya Chadema.
Katibu
wa ACT-Wazalendo, Wilaya ya Shinyanga, Melkyoli Sebastian alisema hayo
baada ya kumuingiza kwenye chama hicho, kada wa Chadema, Ibrahimu
Mbogoma.
Mbogoma alikuwa mwenyekiti wa baraza la wazee kata ya Masekelo manispaa ya Shinyanga.
Sebastian
alisema chama chao kimeanza kuaminiwa na wananchi kutokana na sera zake
za kiujamaa ambazo zimelenga kumkomboa mwananchi wa hali ya chini bila
ya kubagua dini, kabila wala rangi.
Alisema
kutokana na sera hizo, ndiyo maana wanachama wa Chadema wameanza
kujiunga na chama chao baada ya kusoma alama za nyakati.
“Kujiunga
kwa kada huyo aliyekuwa Chadema ni salamu tosha kuwa Chadema inaelekea
kufa kiupinzani, nina imani wapo wanachama wengi wa vyama vya upinzani
watakuja kujiunga na ACT Wazalendo.
"Sisi tunawakaribisha waje kwa wingi ili tukijenge chama kuelekea Ikulu 2020,” alisema Sebastian.
Akieleza
sababu za kuhama Chadema, Mbogoma, alisema ameamua hivyo kutokana na
kuchoshwa na migogoro ndani ya Chadema pamoja na kuongozwa na viongozi
wasiojua majukumu yao.
Mbogoma
alisema tangu alipojiunga na Chadema mwaka 2010 hajaona mafanikio
yoyote licha ya kushika nyadhifa mbalimbali. Alisema amekuwa akikumbana
na migogoro ya mara kwa mara. Alisema anaamini ACT-Wazalendo ndicho
kitaipindua CCM.
Katibu
wa Chadema wilaya ya Shinyanga Mjini, George Kitalama alisema alikuwa
hajapata taarifa rasmi za kiofisi za kuhama kwa mwanachama wake huyo.
Hata hivyo, alisema kila mtu ana haki ya kwenda kujiunga kwenye chama anachokitaka kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment