Kamati ya Miundombinu imeitaka Serikali kuchunguza kwa kina na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote aliyehusika na kufungwa mita za mafuta zilizopo Bandari ya Dar es Salaam, bila kufanya kazi kwa miaka mitano.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Dk Norman Sigala alisema kuna haja ya Serikali
kujiridhisha kwa umakini lengo la kufungwa kwa mita hizo na sababu ya
kufungwa kwake, kisha ichukue hatua.
“Kamati
yetu inatambua wajibu wake ikiwamo kuielekeza Serikali, kuishauri na
kuikosoa bila uoga tulitembelea tukaona zile mashine moja ya mafuta ya
dizeli tayari ilifungwa na inaendelea kufanya kazi, sasa hiyo nyingine
Serikali inapaswa kwenda ndani zaidi kiuchunguzi na kuchukua hatua kali
kwa yeyote aliyehusika,” alisema.
Februari
12, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya ghafla kwenye Kitengo
cha Upimaji Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam na kukuta mita
zimejaa kutu baada ya kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano.
Kutokana
na hali hiyo, alimpa saa nne Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA),
Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga
mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita.
Akizungumzia
kiwango cha fedha za bajeti ya Sh4 trilioni iliyotengwa kwa ajili ya
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, alisema kamati yake
inaridhishwa na kiwango hicho.
Hata
hivyo, alisema Serikali inapaswa kuongeza upembuzi katika uteuzi wa
watendaji wa idara na taasisi zake, ili kuepusha vitendo vya ufisadi
ambavyo vimekuwa vikigharimu fedha nyingi kutafunwa ama kupotea katika
mazingira ya kutatanisha, hivyo kukwamisha juhudi za maendeleo.
“Serikali
ifanye uteuzi vyema wa watendaji wake kigezo cha uadilifu na uwezo wa
kazi kiangaliwe kwa makini, huwezi kuzuia rushwa mahali ambapo kiongozi
si mwadilifu, kamati inaishauri Serikali nafasi hizo zisitolewe kama zawadi,” alisema.
Alisema
wameridhishwa na utendaji wa baadhi ya viongozi wanaokaimu nafasi za
ukurugenzi wa taasisi hivyo na wameishauri Serikali pia iwathibitishe
watu hao ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi vizuri zaidi.
Akizungumza
kuhusu bajeti, Dk Sigala alisema kamati yake imeridhishwa na mipango ya
Serikali iliyoweka kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 kwa wizara hiyo inayolenga kuboresha miundombinu muhimu.
“Serikali
imetenga mafungu ya fedha kwa ajili ya kuboresha reli, barabara,
viwanja vya ndege pamoja na kununua ndege nne, na kwa kuanzia imetenga
Sh250 bilioni kununulia mbili za kuanzia katika mwaka huu wa fedha,” alisema.
Alisema
hata hivyo katika kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Bandari wameishauri
Serikali kupunguza baadhi ya gharama ambazo zinakuwa zinatozwa na
mamlaka hiyo, nia ikiwa ni kuwezesha wavutia wafanyabiashara na kumudu
ushindani na bandari za nchi nyingine.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment