Thursday, 28 April 2016

Tagged Under:

DC Wa Kinondoni Ally Hapi Aanza Mapambano Dhidi Ya Watumishi Hewa, Abaini 89 Waliolipwa Zadi Ya Sh Bilioni 1.331

By: Unknown On: 23:36
  • Share The Gag

  • Mkuu  wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema idadi ya watumishi hewa katika wilaya hiyo, imeongezeka hadi kufikia 89 wakiwa wamesababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja.

    Aidha, Hapi amebaini uwepo wa watumishi vivuli 81 katika kada ya ualimu na hivyo kutoa siku saba kwa maofisa utumishi wa wilaya hiyo, kuhakiki watumishi vivuli ili kubaini idadi yao na hasara waliyosababisha.

    Hapi aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, na kueleza kuwa awali wakati akiingia katika ofisi yake wiki iliyopita alikuta kuna watumishi hewa 34 waliokuwa wamesababisha hasara ya Sh milioni 512.

    Alisema baada ya kufanya uhakiki zaidi walibainika watumishi hewa wengine 55 walioisababishia serikali hasara ya Sh milioni 619 na hivyo kufanya jumla ya hasara kuwa Sh 1,131,754,081.

    “Bado uhakiki wa kina unaendelea ili kuhakikisha tunamaliza hili tatizo la watumishi hewa katika wilaya ya Kinondoni, awali walikuwa 34 lakini sasa wameongezeka 55 na kufikia 89,” alisema Hapi.

    Akifafanua kuhusu watumishi vivuli, Hapi alisema watumishi hao ni wale ambao walihamishwa bila kufuata taratibu na hivyo kuendelea kupokea mshahara wa kazi yake ya awali badala ya kazi yake mpya.

    Alisema walibaini kuwepo kwa walimu katika idara ya elimu ya msingi 42 ambao baada ya kufuatilia hawakuonekana katika shule yoyote ya wilaya hiyo.

    “Kwa hiyo hili nalo ni tatizo kuna walimu wengine wanapokea mshahara mkubwa, lakini mtu alishahamishwa lakini anaendelea kupokea mshahara wa zamani ambao haufanyii kazi,” alisema.

    Katika hatua nyingine, Hapi aliwataka wafanyabiashara ndogo ndogo walioko katika maeneo yasiyoruhusiwa kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa baada ya siku saba alizotoa kukamilika.

    Alisema agizo hilo alilitoa ikiwa ni sehemu ya kuweka Manispaa ya Kinondoni katika hali ya usafi ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya Rais John Magufuli ya usafi wa kudumu.
    ==

    Credit; Mpekuzi

    0 comments:

    Post a Comment