*Aeleza asipobadilika timu itaondolewa mapema kimataifa
NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Dar es Salaam (DRFA), Joseph Kanakamfumu, amemshauri Kocha Mkuu wa timu
ya Yanga, Hans van der Pluijm kubadili mfumo wa timu yake mapema ili
kupata uhakika wa ushindi kila mchezo katika Ligi Kuu Tanzania Bara na
Michuano ya Kimataifa.
Ushauri huo kwa Pluijm umekuja baada ya timu hiyo kuanza kupokea
kichapo cha bao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili dhidi ya
Coastal Union na sare ya 2-2 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya.
Kanakamfumu aliweka wazi kama asipobadilika na kukubali kubadili
mfumo anaotumia, atakuwa kwenye wakati mgumu au kuondolewa mapema kwenye
michuano ya Klabu Bingwa Afrika licha ya kuwa na timu nzuri.
Akizungumza na MTANZANIA, Kanakamfumu alisema kocha huyo atakuwa na
wakati mgumu kupata ushindi katika kila mchezo atakaocheza endapo
ataendelea kutumia mfumo wa 4-2-3.
Alisema mabadiliko atakayokubali kuyafanya yataisaidia timu hiyo
kufanya vizuri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika inayotarajiwa
kuanza Februari 13 mwaka huu siku chache kuanzia sasa.
“Bado Yanga ni timu ya kawaida ingawa imefanya usajili mkubwa
ukilinganisha na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu, hivyo wana wajibu
wa kufanya marekebisho kabla ya kuanza michezo migumu ya Klabu Bingwa
Afrika,” alisema Kanakamfumu.
“Pluijm amezoeleka kuichezesha Yanga kwenye ligi mfumo ambao unatumia
sana washambuliaji kuliko viungo, hali ambayo inamgharimu katika baadhi
ya michezo.
“Mfumo huo ndio ulisababisha timu hiyo kufungwa na Coastal Union wiki
iliyopita, wakati anaweza kuchezesha mfumo wa 4-4-2 ambao ulimpa
ushindi katika mchezo dhidi ya Simba katika mzunguko wa kwanza,”
alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Polisi Dodoma, alisema endapo kocha huyo
hatoweza kubadilika anaweza kupata matokeo mabaya zaidi kwenye michezo
ijayo.
“Tangu Nadir Harub (Cannavaro) awe majeruhi safu ya ulinzi imepoteza
umakini kitu ambacho kinafanya kuwe dhaifu eneo la nyuma kutokana na
uchache wa viungo.
“Unapochezesha mfumo huo ni muhimu kuwa na mshambuliaji mwenye
kiwango kizuri cha ufungaji, ili kufanya upatikanaji wa mabao uwe
mwepesi, lakini ikiwa tofauti litakuwa jambo la kubahatisha kama
anavyofanya Pluijm,” alisema.
Aliongeza kwamba, ni nadra kwa kocha yeyote duniani kuchezesha mfumo
ambao unatoa fursa chache za utengenezaji wa pasi za mwisho ambazo
zinatumika kupata mabao.
“Kabla ya Haruna Niyonzima kurudi dimbani, awali Pluijm alikuwa
akiwatumia Thaban Kamusoko kama namba nane huku Mbuyu Twite akiwa namba
sita, idadi ambayo ni ndogo ya viungo ukilinganisha na washambuliaji,”
alisema.
Alieleza kuna wakati timu hiyo inalazimika kucheza mipira mirefu
kutokana na udhaifu wa mfumo unaotumika ambao unaowanyima wachezaji
kuchezea mpira wa burudani.
Chanzo Mtanzania.
Thursday, 4 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment