Veronica Romwald na Esther Mnyika, Dar es Salaam
SERIKALI imeombwa kudhibiti uingizwaji na utengenezaji wa bidhaa za
tumbaku nchini kwa sababu utafiti unaonyesha asilimia 32 ya saratani
zote zinasababishwa na zao hilo.
Pia imetakiwa kuchukua hatua kali ya kudhibiti kasi ya ongezeko la
vijana wanaovuta bidhaa hizo, wakichochewa zaidi na uingizwaji wa
tumbaku aina ya shisha na sigara za umeme.
Rai hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji
wa Chama cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Tanzania (TTCF), Lutgard
Kagaruki, wakati alipokuwa akitoa mada kwenye semina ya siku moja ya
waandishi wa habari, iliyolenga kuwajengea uelewa juu ya namna tumbaku
inavyochangia ongezeko la ugonjwa huo.
“Tumbaku huua wavutaji milioni sita kwa mwaka duniani, huku wengine 600,000 wasiovuta wakivutishwa moshi wa tumbaku,” alisema.
Alisema tumbaku inachangia kwa kiasi kikubwa matatizo ya upungufu wa
nguvu za kiume, huku Serikali ikitumia kiasi kikubwa cha fedha takribani
dola za Marekani milioni 4 kwa mwaka kugharamia matibabu.
“Hii ni kwa mujibu wa utafiti tulioufanya katika Taasisi ya Saratani
ya Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) mwaka 2009 na
hapo hatukwenda maeneo ya vijijini, hivyo huenda hali ikawa mbaya
zaidi,” alisema.
Alisema ni vyema Serikali ikatunga sheria kwa ajili ya kusimamia
udhibiti wa bidhaa hiyo kama ambavyo ilikubali mkataba wa kimataifa wa
kudhibiti matumizi ya tumbaku.
“Tanzania iliridhia mkataba tangu 2007. Haina budi kutekeleza
kikamilifu kwa kutunga sheria madhubuti ya kudhibiti matumizi ya tumbaku
inayoendana na matakwa ya mkataba wenyewe,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage,
alisema idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka ambapo hadi sasa imefikia
asilimia 100.
“Takwimu zetu zinaonyesha mwaka 2000 hadi 2005 tulikuwa tunapokea
wagonjwa wapya 2,400 hadi 2,500 kwa mwaka, idadi imeongezeka hadi
kufikia wagonjwa wapya 5,500 mwaka 2015,” alisema.
Alisema hali hiyo inachangiwa zaidi na mfumo wa maisha ya sasa ambapo
watu wengi wamekuwa hawazingatii ulaji bora, matumizi ya pombe, uvutaji
wa sigara, kutokufanya mazoezi na mambo mengineyo.
Chanzo Mtanzania.
Thursday, 4 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment