Siku moja baada ya Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing kusema kuwa nchi yake inaamini kuwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar hivi karibuni ulikuwa huru na haki, chama cha CUF kimejitokeza na kupinga kauli hiyo kikieleza ni ukandamizaji wa demokrasia.
Chama hicho
kimeionya China kuacha siasa na kufumbia macho ukiukwaji wa demokrasia
nchini kwa masilahi yao na kuitumia Tanzania kujinufaisha na rasilimali
zilizopo bila kujali amani itakapovunjika hapo baadaye.
Juzi, Dk
Youqing alipokuwa anazungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alimhakikishia kuwa nchi
yake itaendelea kutoa misaada kwa Tanzania hata baada ya Shirika la
Marekani la Maendeleo ya Milenia (MCC) kusitisha misaada.
Mkurugenzi
wa Mambo ya Nje wa CUF, Abdalah Mtolea alisema China inahalalisha
uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar kwa sababu ya masilahi yao ya
kiuchumi kwa taifa lao na raia wa China waliopo nchini.
“CUF
tunaelewa kwamba kwa nchi yoyote inayofahamu demokrasia, uhuru na haki
ni nini, hawezi kusema uchaguzi wa marudio Zanzibar ulikuwa huru na
haki,” alisema.
Alisema chama kikongwe kinachotawala China CCP
na CCM vimekuwa na uswahiba wa muda mrefu jambo linaloifanya nchi hiyo
kutoaana mambo mbalimbali ya ukiukwaji wa demokrasia na haki za binadamu
wakihofia kuharibu uhusiano wao.
Alisema Serikali ya Tanzania
inapaswa kuwa makini na uhusiano na misaada inayotolewa na nchi hiyo ili
kubaini ina malengo gani yaliyofichika kwa Taifa letu.
Mtolea ambaye pia ni
Mbunge wa Temeke alisema China imeamua kuunga mkono kukandamizwa kwa
demokrasia nchini Tanzania ili kujikomba kwa Serikali ya CCM waendelee
kupata hisani zaidi kwa masilahi ya taifa lao.
Alisema: “China
inapata tenda kubwa za ujenzi nchini Tanzania mfano ujenzi wa barabara
ambazo nyingine zishaanza kuharibika, madaraja na majengo makubwa
nchini.
"Hata mradi wa kusafirisha gesi, kana kwamba hiyo
haitoshi, kumekuwa na ongezeko la Wachina wakifanya biashara
zinazofanywa na Watanzania huku wengine wakiishi nchini bila vibali."
Katika
mazungumzo yake na Waziri Makamba, Balozi Youqing alisema China ina
mipango mingi ya ushirikiano na Tanzania, ikiwamo kwenye sekta ya umeme
na itaendelea kutoa ushirikiano kupitia kampuni zake.
Kwa upande
wake, Makamba alimshukuru Balozi Youqing pamoja na Serikali ya China
kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.
“Ujumbe na
salamu ulizotoa leo umetupa faraja Watanzania. Urafiki baina ya nchi
zetu, na baina ya vyama vyetu vya CCM na CCP, ni wa muda mrefu, ni wa
majira yote na umejengwa kwenye misingi ya kuheshimiana na hauna budi
kuendelezwa”, alisema Makamba.
Pia Waziri Makamba na Balozi
Youqing walikubaliana kutembelea Pemba na Unguja kwa pamoja ili kukagua
na kutengeneza miradi ya maendeleo kati ya China na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment