Friday, 1 April 2016

Tagged Under:

Kitilya, wenzake wawili kortini

By: Unknown On: 23:17
  • Share The Gag
  • Kamishina Msaidizi msitaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya (wa pili kushoto), Shose Sinare (wa pili kulia) na Sioi Sumari (kushoto) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana.

    SAKATA la rushwa ya Dola za Marekani milioni 600, linalohusisha Benki ya Standard ya London Uingereza, jana lilichukua sura mpya baada ya kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, akikabiliwa na mashitaka mbalimbali, ikiwemo utakatishaji wa fedha.

    Washitakiwa wengine waliounganishwa katika kesi hiyo ni pamoja na mrembo wa zamani wa Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa benki hiyo, Sioi Graham Solomon. Mashitaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali na kutakatisha fedha, ni pamoja kutumia nyaraka za kughushi na za uongo kujipatia isivyo halali Dola za Marekani milioni 6, sawa na Sh bilioni 12 za Tanzania.
    Mbele ya Hakimu Mwandamizi, Emilius Mchauru washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na kurudishwa rumande mpaka Aprili 8 mwaka huu, wakati mahakama itakapokutana kusikiliza shauri kuhusu dhamana yao. Upande wa utetezi, ukiwakilishwa na mawakili Dk Ringo Tenga na Semu Anney, waliomba mahakama itoe dhamana kwa wateja wao.

    Hata hivyo, upande wa Mashitaka ukiwakilishwa na wanasheria waandamizi wa Serikali; Oswald Tibabyekomya na Christopher Msigwa pamoja na Mwanasheria wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Stanley Luwoga walipinga dhamana hiyo kwa madai kuwa kesi za utakatishaji fedha hazina dhamana.
    Awali upande wa mashitaka uliieleza mahakama kwamba, katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013, katika Jiji la Dar es Salaam, washitakiwa hao watatu walipanga pamoja kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani hapo, kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.

    Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic Tanzania Limited yaliyopo wilayani Kinondoni, mshitakiwa Sinare akiwa na nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya Benki ya Standard ikiwa na tarehe ya Agosti 2, 2012.
    Kwa mujibu wa madai hayo, Sinare alieleza katika maombi hayo kuwa Benki ya Standard ya London kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania, watatoa mkopo unaofikia Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa gharama ya asilimia 2.4 ya mkopo huo, wakati akijua kuwa gharama hiyo si kweli.

    Mahakama ilielezwa kuwa Agosti 13, 2012, mrembo huyo wa zamani wa Tanzania, aliwasilisha taarifa hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha iliyopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam. Imedai kuwa Septemba 20, 2012 katika Benki ya Stanbic, Sinare alitengeneza barua ya uongo ya kuelezea mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550, ikieleza kuwa Benki ya Standard PLC kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic, zitatoa mkopo huo kwa Serikali kama wakikubaliwa.

    Upande huo wa mashitaka uliendelea kudai kuwa, Sinare aliwasilisha barua hiyo ya uongo katika Wizara ya Fedha kwa lengo hilo hilo. Kwa mujibu wa madai hayo, Novemba 5, 2012 katika Benki ya Stanbic jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote watatu, wakiwa na nia ovu, walitengeneza makubaliano ya uongo kwa lengo la kuonesha kuwa benki imeipa kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA) Limited, kazi ya kushughulikia mkopo huo.

    Lengo la washitakiwa hao kwa mujibu wa madai hayo, lilikuwa kufanikisha mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania, ambapo EGMA alitarajiwa kuonekana kuwa muongozaji wa mazungumzo ya kupata mkopo huo. Upande huo wa mashitaka ulidai kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam, Kitilya, Sinare na Sioi, wakiwa na lengo ovu walifanikiwa kupata Dola za Marekani milioni 6, sawa na Sh bilioni 12, wakidai kuwa fedha hizo ni malipo ya kazi iliyofanywa na EGMA Limited.

    Utakatishaji fedha Watatu hao pia wameshitakiwa kwa utakatishaji fedha unaodaiwa kufanyika kati ya Machi 13 na Septemba mwaka jana. Wanadaiwa kushiriki kutakatisha Dola za Marekani milioni sita kwa kuzihamisha kwenda katika akaunti tofauti, kuzitoa katika akauti hizo na kuziweka katika akauti zingine tofauti zinazomilikiwa na EGMA Limited katika Benki ya Stanbic Tanzania Limited na Benki ya KCB Limited.

    Mahakama imeelezwa kuwa hivi karibuni Benki ya Standard imelipa Dola za Marekani milioni 33 baada ya kukiri kushindwa kuzuia rushwa katika suala hilo. Mbunge kortini Katika hatua nyingine, Takukuru jana ilimfikisha Mahakamani Mbunge wa Sumwe, Richard Ndassa (pichani), ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Mtaji na Uwekezaji kwa kosa la kushawishi na kuomba rushwa ya Sh milioni 30, kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15 (i)(a) na (2).

    Taarifa ya Takukuru kwa vyombo vya habari, imedai kuwa Mbunge huyo akiwa mjumbe wa Kamati hiyo, alimwomba rushwa hiyo Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Felchesmi Mramba ili amsaidie kuwashawishi wajumbe wengine wa Kamati Mtaji na Uwekezaji kupitisha bila kipingamizi taarifa ya Tanesco kwa mwaka 2015/16.
    Mbunge huyo amefunguliwa kesi namba 118/2016 na alisomewa mashitaka hayo na Wakili wa Takukuru, Dennis Lekayo akishirikiana na Emmanuel Jacob katika Mahakama ya Kisutu mbele ya. Hakimu Emirius Mchauro.
    Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kupata mdhamini mmoja na kulipa Sh milioni 10 na uchunguzi wa shauri hilo bado unaendelea huku kesi ikitarajiwa kutajwa tena Aprili 18, 2016.

    Chanzo HabariLeo.


    0 comments:

    Post a Comment