Waziri Mkuu Kasim Majaliwa akionesha usinga na mkuki ambavyo alipewa na wazee wa Kisukuma wa
Busega katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Lamadi, juzi. Wazee
hao pia walimbatiza jina la Massanja.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa alisema Tanzania inaweza kujitegemea kwa
zaidi ya asilimia 80 katika bajeti yake kutokana na vyanzo vyake vya
ndani. Amesema kutokana na rasilimali zilizopo, Tanzania inaweza kukidhi
bajeti yake kwa asilimia 80 bila kutegemea msaada kutoka nje na kwamba
suala la kukabiliana na ufisadi na ukwepaji kodi ni endelevu.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo juzi mjini Lamadi wakati akihutubia
maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika siku ya kwanza ya
ziara yake ya siku sita mkoani Simiyu. “Tanzania inaweza kujitegemea kwa
asilimia 80 kwa mapato yake kutokana na rasilimali na vyanzo vyake vya
ndani.
Hili linawezekana. Ndio maana tumeamua kubanana,” alieleza Waziri
Mkuu. Alisema ndio maana wameamua kupambana na ufisadi na ukwepaji kodi
kwa nia ya kuhakikisha wanapata fedha za kuwatumikia Watanzania kwa
fedha za ndani kupitia mapato yake.
Alisema hata uamuzi wa kupitisha fedha zote katika Mfuko Mkuu wa
Serikali ulikuwa na nia ya kutambua mapato yake yote ili fedha hizo
zikasaidie kuleta maendeleo ikiwamo kuisimamia Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ili kubana mianya yote ya ukwepaji kodi.
Alisema hali hiyo imesaidia kwani mapato yameongezeka kutoka Sh
bilioni 1.3 Desemba mwaka jana, Sh bilioni 1.5 Januari mwaka huu na
mwezi uliopita, alisema ana hakika zitavuka zaidi.
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali ndio maana inagharimia mambo
yake mengi likiwamo suala la elimu bure, na kwamba licha ya kuwapo kwa
changamoto mbalimbali, watahakikisha Watanzania wanapata huduma
mbalimbali zilizoboreshwa.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum akiwasilisha bungeni
mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka
wa fedha 2015/16, Juni mwaka jana, alisema jitihada za kuongeza mapato
zimelenga kuisaidia Serikali kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali
kwa fedha za wahisani.
Alisema kiwango cha utegemezi kimepungua kutoka asilimia 24 mwaka
2004/05 hadi asilimia 17 mwaka 2010/11. Alisema pia kwamba utegemezi huo
umekuwa ukipungua mwaka hadi mwaka. Mwaka 2015/16 ilitarajiwa upungue
kwa asilimia 6.4.
Kuhusu suala la mipaka kati ya hifadhi na vijiji, Waziri Mkuu alisema
amekwishaagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia suala hilo na
kuhakikisha wanaliangalia limalizike kwa busara.
Lakini ameagiza wananchi hasa katika wilaya za Busega na Bariadi
kutoingia tena katika hifadhi ambako inadaiwa wanapokonywa ng’ombe wao
na askari wa Wanyamapori kwa kutozwa Sh milioni tano hadi 10.
Amewaonya askari hao wa Wanyamapori kuacha tabia hiyo na kwamba
mwananchi yeyote mwenye taarifa za askari anayeshiriki vitendo hivyo,
kupeleka jina lake kwa vyombo husika.
Chanzo HabariLeo.
Thursday, 3 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment