Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu akimuapisha Kamishna wa Polisi, CP Nsato Marijani baada ya kupandishwa cheo na Rais. |
POLISI imesema ina taarifa juu ya kuibuka kwa makundi ya kihalifu nchini na imejipanga kukabili wahusika. Aidha, Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, amehadharisha askari na watendaji wa jeshi hilo, aliowataja kuwa wasaliti na kusema watakaobainika watafukuzwa na si kuhamishwa vituo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu mikakati ya jeshi katika mapambano ya uhalifu nchini, Marijani amewataka wananchi kuwa watulivu , kutotaharuki kwa kile alichosisitiza kuwa nchi iko salama wakati Polisi ikiendelea kujipanga kukabili vikundi husika.
Kamishna Marijani alisema makundi ya uhalifu yanayoibuka nchini yamekuwa kero . Alisema juhudi za makusudi zinafanywa kuyadhibiti kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
“Hatuwezi kuweka mikakati yetu hadharani ya kukabiliana na vikundi vya uhalifu vilivyoibuka hivi sasa, ila wafahamu kwamba tutawadhibiti kikamilifu,” alisema Kamishna Marijani. Alisema hakuna haja ya wananchi kuwa na hofu bali wawe watulivu na kuendelea kufanya shughuli zao za uzalishaji mali, kwa sababu vyombo vya usalama vipo na vitahakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao unalindwa .
Alisisitiza kwamba, ni vyema kwa raia wanapoona tabia au mienendo yenye mashaka ya watu, watoe taarifa Polisi. Polisi wasaliti Akizungumzia suala la nidhamu kwa askari na watendaji wa jeshi hilo, Kamishna Marijani alisema watendaji wengi wa jeshi hilo wana nidhamu na wanafanya kazi kwa weledi.
Hata hivyo, alisema wapo wachache wanaochafua jeshi hilo. Alisema watakapobainika, hawatawavumilia wala kuwahamisha vituo vya kazi, bali watafukuzwa. “Watendaji wetu wengi wana nidhamu, ila wapo wachache wanaotuchafua, kuanzia sasa hatutawahamisha vituo vya kazi, tutawafukuza, kama walizoea huko nyuma , sio zama hizi, wajue kila zama zina vitabu vyake”, alisisitiza .
Alisema hatua hiyo wataitekeleza bila uoga wala kificho . Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kuhusu taarifa za watumishi wa jeshi hilo wasio na maadili ili hatua zichukuliwe.
Hivi karibuni, kumejitokeza matukio kadhaa ya uhalifu hususan jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa matukio hayo, ni uvamizi wa benki ya DCB katika eneo la Chanika, wilayani Ilala. Uvamizi mwingine ulifanyika Benki ya Access , Tawi la Mbagala.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment