Saturday, 27 February 2016

Sarakasi za umeya Dar zaendelea

By: Unknown On: 22:31
  • Share The Gag
  • Madiwani wanaounda Umoja Katiba ya wananci (UKAWA) wakivutana na polisi baada ya kutokea vurugu katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, zilizosababisha kuahirishwa kwa uchaguzi huo katika ukumbi wa Karimjee.

    VURUGU na fujo zimerindima jana katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, baada ya kuahirishwa tena kwa uchaguzi huo.
    Katika vurugu hizo, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Theresa Mmbando alifanyiwa fujo na wafuasi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), lakini polisi waliokuwa na mabomu pamoja na risasi, walidhibiti hali hiyo.
    Mmbando alijikuta akikabiliana na vurugu baada ya wafuasi hao wa Ukawa na viongozi wao, wakiwemo wabunge na madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujaribu kumvamia baada ya kutangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo.
    Katibu Tawala huyo alisema uchaguzi huo, unaahirishwa hadi zuio lililoandikwa tangu Februari 5 dhidi ya uchaguzi huo, lililokuwa limebandikwa mlangoni mwa ukumbi wa Karimjee, litakaposikilizwa.
    Kutokana na hali hiyo, askari Polisi walifika na magari ya Polisi (defender) kuangalia usalama, wakamtoa Mmbando kwa mlango mwingine ili kudhibiti vurugu hizo.
    Wanachama wa Ukawa, walihoji ni kwa nini Mmbando atangaze kuahirishwa kwa uchaguzi huo bila kubainisha ni nani aliweka zuio hilo.
    Pia walihoji kama zuio hilo lilitolewa muda mrefu, kwanini watangaze jana bila ya kuandika barua kwa vyama husika.
    Waliotoa hoja hizo ni pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na wanachama wengine wanaounda umoja huo.
    “Hatukubaliani na suala hili. Tunamuomba Rais atumie kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ katika masuala makubwa kama haya ya umeya na wala asifumbie macho,” alisema Mdee.


    Chanzo HabariLeo.


    Yanga yang’ara Afrika

    By: Unknown On: 22:28
  • Share The Gag
  • Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la pili lililofungwa na Thaban Kamusoko (wa pili kulia) kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius Uwanja wa Taifa, Dar es Salaa jana. Wengine kutoka kushoto ni Vicent Bossou, Deusi Kaseke.

    Yanga imeleta heshima kwa Watanzania baada ya jana kuifunga Cercle de Joachim ya Mauritius mabao 2-0 katika mchezo wa maruadiano Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kutokana na matokeo hayo Yanga imefuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 3-0, baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Mauritius wiki mbili zilizopita Yanga kushinda bao 1-0.
    Yanga itakumbana na mshindi wa mchezo kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland.
    Ilikuwa furaha kwa mashabiki wa Yanga walioingia jana kifua mbele ikiwa ni wiki moja baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya watani wao Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
    Hata hivyo Yanga licha ya ushindi huo, itabidi ijilaumu kutokana na kukosa nafasi nyingi za wazi, ambazo zingewawezesha kupata ushindi mnono.
    Lakini washambuliaji wake wakiongozwa na Amis Tambwe, Simon Msuva, Malimi Busungu na Paul Nonga kwa nyakati tofauti walishindwa kulenga lango la wapinzani wao.
    Washambuliaji hao kila walipokaribia lango la Yanga, ama walipiga michomo dhaifu iliyodakwa na kipa au walipiga nje ya lango.
    Yanga ilianza kupata bao la mapema dakika ya tatu mfugaji akiwa Amiss Tambwe kutokana na krosi ya Simon Msuva.
    Bao hilo liliwapa matumaini mashabiki wa Yanga kuona ushindi mnono, lakini kadri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo matumaini hayo yalipokuwa yakififia.
    Wageni walijitahidi kupanga mashambulizi dakika za mwanzo kipindi cha pili, lakini walijikuta wakipachikwa bao la pili dakika ya 56 mfungaji akiwa kiungo Thabani Kamusoko kwa shuti lilitokana na mpira wa adhabu wa Juma Abdul.
    Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondani, Vincent Bossou, Mbuyu Twite/Pato Ngonyani, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Malimi Busungu/Paul Nonga na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya.
    Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la pili lililofungwa na Thaban

    Chanzo HabariLeo.

    Mwanasheria Mkuu wa Serikali amuunga mkono Jecha

    By: Unknown On: 22:24
  • Share The Gag

  • MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju

    MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju amemuunga mkono Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kwa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na kusema hatua hiyo ni halali kutokana na sababu zilizotajwa.
    “Ukichukua kasoro zote na hii ya mgombea kujitangaza mshindi... ni tatizo kubwa, lazima mtaingia kwenye matatizo iwapo huyu kajitangazia ushindi halafu matokeo yamtangaze mshindi tofauti na huyo,” alisema Masaju.
    Akizungumza kwenye kipindi cha Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano, kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), juzi usiku, Mwanasheria huyo alisema ZEC iko huru kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na uamuzi uliofanywa na Mwenyekiti wa Tume hiyo ni kitendo halali.
    Masaju alisema kasoro zote zikichunguzwa, ikiwemo hiyo ya mgombea kujitangazia ushindi, kulikuwa na kila sababu ya kufuta matokeo hayo ili uchaguzi urudiwe.
    Alisema iwapo dosari hizo, zingeachwa bila kufanyiwa kazi, hata wagombea wasio na sifa ya kushinda katika uchaguzi huo, wangesema na wao ni washindi hivyo kungetokea machafuko ambayo yangeweza kuleta matatizo makubwa zaidi.
    Ila kwa hatua iliyochukuliwa na ZEC ni jambo sahihi la kurudisha amani na kupanga tarehe nyingine ya kurudia uchaguzi huo, ili kasoro hizo zirekebishwe na mshindi apatikane kwa haki na kuepuka machafuko.
    Masaju alisema awali Rais John Magufuli wakati akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe, alisema atashirikiana na Rais wa Zanzibar kumaliza suala la uchaguzi, ila hakusema ataingilia uhuru wa Tume.
    “Rais alipohutubia Bunge kwa mara ya kwanza aliahidi kushirikiana na Rais wa Zanzibar kumaliza suala la uchaguzi, ila hakusema ataingilia uhuru wa Tume na ndicho alichofanya, Zanzibar ina amani,” alisema Masaju.

    Chanzo HabariLeo.

    Waziri Mkuu Kutua Jijini Mwanza Kesho Kutwa

    By: Unknown On: 22:18
  • Share The Gag

  • WAKAZI wa Jiji la Mwanza na vitongoji vyake wametakiwa kujitokeza kwa wingi keshokutwa ili kumpokea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye anatarajiwa kuwasili jijini hapa akitokea jijini Dar es Salaam akielekea mkoani Simiyu.
     
    Hayo yameelezwa jana jijini hapa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Baraka Konisaga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, wakati alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Kamanga Feri wakati alipowaongoza kwenye shughuli ya kufanya usafi.
     
    “Niwataarifu kuwa Waziri Mkuu atawasili jijini Mwanza kwa mara ya kwanza siku ya Jumanne majira ya saa 7:00 mchana akitokea jijini Dar es Salaam… akishawasili hapa ataelekea mkoani Simiyu kikazi, nawaomba muiweke moyoni siku hiyo ya Jumanne na mjitokeze kwa wingi kumlaki kiongozi wetu mpendwa, ” alisema.
    Credit;Mpekuzi blog

    Ufisadi wa vitabu waathiri darasa la kwanza

    By: Unknown On: 22:17
  • Share The Gag
  • UFISADI uliofanyika katika uchapaji wa vitabu 2,807,600, vilivyo tayari kutumika kwa ajili ya darasa la kwanza nchi nzima, umesababisha wanafunzi hao, ambao mwaka huu udahili wao umeweka historia kwa idadi kubwa kuwahi kudahiliwa, kulazimika kutumia vitabu vya zamani.
    Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna Tarishi (pichani), alisema hayo jana alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam. Alifafanua kwamba kasoro kubwa, zilizobainika katika vitabu hivyo, ambavyo vilishafika katika ghala la Serikali, zimesababisha Serikali izuie visisambazwe.
    Kwa mujibu wa Tarishi, vitabu hivyo vya ‘Najifunza Kusoma Kitabu cha Kwanza’ na ‘Najifunza Kusoma Kitabu cha Pili’, vimechapwa na kampuni ya Yukos Enterprises, ambayo ni moja ya kampuni tatu zilizoshinda zabuni ya kazi hiyo iliyotangazwa Aprili mwaka jana.
    Lakini, alisema kasoro hizo zimesababisha Serikali kuagiza viondolewe katika ghala lake na udhibiti ufanyike visisambazwe mashuleni.
    Upungufu
    Kasoro zilizokutwa ni muingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa, picha moja kuwa na rangi tofauti, ukataji usiozingatia vipimo, baadhi ya vitabu kufungwa kwa pini moja katikati badala ya mbili, huku vingine vikikosa pini kabisa na vingine vikifungwa ubavuni.
    Kasoro nyingine ni vingine vimekutwa vimechakaa kabla ya matumizi, hasa kitabu cha ‘Najifunza Kusoma Darasa la Kwanza Kitabu cha Pili’; vingine vikiwa na mpangilio mbaya wa kurasa, ufifiaji wa maandishi huku picha katika baadhi ya vitabu na maandishi, vikishindwa kuonekana kabisa.
    Kasoro nyingine kwa mujibu wa Tarishi ni namba za kurasa kutoonekana kabisa, baadhi ya kurasa kujirudiarudia, baadhi ya kurasa kutotenganishwa, maandishi ya baadhi ya vitabu kugeuzwa mwelekeo, majalada kuwa zaidi ya moja na baadhi ya vitabu kukutwa vimedurufiwa (photocopy).
    Katibu Mkuu huyo alisema kasoro hizo, zilibainika baada ya ufuatiliaji kufanywa na Wizara katika bohari iliyokuwa ikipokea vitabu hivyo.
    “Kutokana na kasoro hizo, ni dhahiri mchapaji Yukos Enterprises Ltd hakuzingatia vigezo vilivyowekwa na kwa kufanya hivyo amekiuka makubaliano yaliyo katika mkataba alioingia na Taasisi ya Elimu Tanzania,” alisema Tarishi.
    Athari zake
    Kutokana na hali hiyo, Tarishi alisema wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka huu watapungukiwa vitabu vya kujifunza kusoma, kwa kuwa haviwezi kutumika. Hivyo aliagiza wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka huu, watumie vitabu vya zamani na walimu watatumia ‘Kitabu cha Kiongozi cha Mwalimu’ ambacho ni kipya.
    Kuhusu gharama iliyotumika, Tarishi alisema ni zaidi ya Sh bilioni mbili, lakini alibainisha kuwa mchapishaji alikuwa amelipwa asilimia 20 tu kwa kutumia dhamana ya benki.
    Majipu yatumbuliwa
    Kasoro hizo zimemlazimu Katibu Mkuu huyo kuagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), kuwasimamisha kazi vigogo wa taasisi hiyo, akiwemo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Vifaa vya Kielimu, Peter Bandio, Mwanasheria, Pili Magongo na Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Jackson Mwaigonela.
    Hatua hiyo imetakiwa kufuatia uchunguzi katika taasisi hiyo, kuhusu vipi wameshindwa kusimamia Sheria ya Manunuzi na kazi ya uchapaji wa vitabu.

    Chanzo HabariLeo.

    Sinema ujambazi wa kivita jijini Dar

    By: Unknown On: 22:14
  • Share The Gag
  • UJAMBAZI wa kutumia vifaa vya kivita umeibuka jijini Dar es Salaam, ukiwemo uliofanyika katika uporaji wa Benki ya Access juzi, ambako majambazi walitumia bunduki za kivita aina ya SMG na mabomu ya kurusha kwa mkono.
    Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema mbali na uvamizi huo, pia Polisi imebaini na kukamata askari bandia, waliokuwa na sare rasmi za Jeshi la Polisi zenye vyeo na redio call, zenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya askari Polisi.
    Akizungumzia matukio hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alisema atakutana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, ili Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi, waanzishe msako wa pamoja dhidi ya wahalifu hao.
    Uvamizi, mauaji Mbagala
    Akisimulia ujambazi uliofanyika katika Benki ya Access Tawi la Mbagala, Kamanda Sirro alisema majambazi hao walikuwa 12, wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki sita na walifika kwenye benki hiyo saa 8:30 mchana.
    Baada ya kufika, moja kwa moja waliingia kwenye chumba cha askari wanaolinda benki na kumpiga risasi kichwani askari mwenye namba H7739 Konstebo Harid na kufa papo hapo.
    Mbali na mauaji hayo, Kamanda Sirro alisema walimshambulia askari mwingine, Konstebo Shaban miguuni na kupora silaha zao na kuingia nazo ndani ya benki, ambako walimshambulia mlinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi na raia wengine wawili na kufa papo hapo, huku wengine watano wakijeruhiwa.
    Baada ya hapo kwa mujibu wa Kamanda Sirro, majambazi hao walikimbilia chumba kinachohifadhi fedha nyingi (strong room) na kukipiga risasi katika jitihada ya kutaka kuingia ndani, lakini hawakuweza kuvunja.
    Kutokana na ugumu wa kuvunja chumba hicho, Kamanda Sirro alisema haraka haraka wakahamia katika kaunta za watoa fedha na kupora fedha zilizokuwepo kati ya Sh milioni 20 mpaka Sh milioni 30 na kuondoka na silaha za polisi aina ya SMG mbili na ile yao moja pamoja na pikipiki zao.
    Polisi waua watatu
    Kamanda Sirro alisema taarifa zilisambazwa katika vikosi vya ulinzi, ambavyo vilijiimarisha.
    Alitaja Kikosi cha Mbwa na Farasi eneo la Mkuranga, ambao walijiandaa na majambazi hao walipofika kijiji cha Chui wilayani Mkuranga mkoani Pwani, walipambana na polisi na askari wakafanikiwa kuua majambazi watatu.
    Mbali na kuua watatu, silaha tatu zilikamatwa ambazo ndio zile SMG mbili za Polisi, walizochukua pamoja na ile yao moja, lakini wakakutwa pia na mabomu matatu ya kutupa kwa mkono yaliyotengenezwa Urusi.
    “Hawa majambazi walikuwa wamejiandaa, kwa maana walikuwa na mabomu ya kutupwa kwa mkono matatu aina ya RGD 01 ambayo ni mbinu ya kujilinda wanaposhambulia,” alisema Kamanda Sirro.
    Tisa watoroka
    Pamoja na kujiimarisha kwa polisi, majambazi tisa walikimbia wakaacha pikipiki zote sita za aina tofauti, ambazo ni Haojue mbili zenye namba MC 560 AED na MC 207 BAN, San LG yenye namba MC 784 BDJ, Boxer yenye namba MC 248 AXE na King Lion mbili zenye namba MC 653 BDQ na MC 853 BDR.
    Kamanda Siro alisema baada ya hapo, waliendelea kuwakimbiza majambazi hao hadi wakatokomea katika Msitu wa Kongowe, ambako juhudi za kuwatafuta zilianza mara moja.
    “Nawahakikishia wananchi mtandao wote wa ujambazi kwenye mabenki na maeneo mengine, tutausafisha wote kwa maana hawa wanafanya uhalifu maeneo ya Dar es Salaam na Pwani na wana ndugu zao, tutawakamata wote,” alisisitiza Kamanda Sirro.
    Alisema hawawezi kuona Watanzania wakiumia na kufa kwa tamaa za wachache, wenye kupenda utajiri wa haraka.
    JWTZ kazini
    Akizungumza kuhusu ujambazi huo, Waziri Kitwanga alisema Polisi inajipanga upya na atazungumza na Waziri mwenzake, Dk Mwinyi kuangalia jinsi ya majeshi hayo mawili, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), watakavyofanya kazi pamoja ya msako katika misitu yote inayozunguka mikoa ya Pwani, kuanzia Bagamoyo hadi Kisarawe.
    Alionya kama kuna kambi za uhalifu ndani ya misitu hiyo, zitasambaratishwa na kuomba raia wema watoe taarifa za uhalifu.
    “Tutafanya operesheni kubwa na tutaifanya haraka, tunaomba wananchi watoe ushirikiano hasa waendesha bodaboda kwa maana zinatumika sana kwenye matukio haya. Mtandao wa majambazi ufahamu kwamba vyombo vya usalama havijalala, tutawamaliza wote, tutatumia nguvu zetu zote kuwamaliza na tutafanikiwa,” alisisitiza Kitwanga.
    Kuhusu waendesha bodaboda, Kitwanga alisema ukaguzi wa kina unafanywa na kuwataka waendesha bodaboda hao wanaposimamishwa, wakubali na kutoa ushirikiano na wasione kama wanabughudhiwa, bali ni kuwakagua kwa sababu wahalifu hutumia vyombo hivyo zaidi kufanya matukio mabaya.
    Polisi feki
    Katika tukio jingine, Kamanda Sirro alisema polisi feki wanne wamekamatwa na wanashikilia kwa mahojiano, ili kubaini mtandao huo ambao unatumia sare za Polisi, redio za upepo na pingu kufanya matukio ya uhalifu.
    Alisema walipata taarifa kutoka kwa raia wema ya kuwepo kwa mtandao wa askari bandia, ambao hutumia sare za jeshi hilo kufanya matukio ya uhalifu, ndipo walipowakamata hao wanne. Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, polisi feki watatu walikamatwa Februari 24, asubuhi saa mbili eneo la Upanga karibu na Daraja la Selander.
    Alisema watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, walikiri kufanya matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja anayeishi Kinyerezi. Kamanda Siro alisema Polisi walimfuata mtuhumiwa huyo nyumbani kwake Kinyerezi na walipofanya upekuzi, walimkuta na sare halisi ya Polisi, redio ya upepo na pingu.
    Kamanda Sirro alisema baada ya uchunguzi, imebainika kwamba watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia sare na vifaa hivyo vya Polisi, kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi kwa kujiaminisha kuwa wao ni askari Polisi.
    Alisema watuhumiwa hao wamekiri kufanya matukio mbalimbali, ikiwemo kuweka vizuizi katika barabara za mikoani na kufanya uporaji.
    “Watuhumiwa hao wote wanahojiwa ili waeleze jinsi walivyopata sare na vifaa hivyo ya Polisi, wamekiri kufanya uhalifu maeneo mbalimbali, lakini wakati mwingine tunashindwa kukamata wahalifu kwa sababu redio call wanayotumia zinaingiliana na zetu, hivyo wanakuwa wamepata taarifa,” alisema Kamanda Sirro.
    Katika tukio lingine, Februari 18 mwaka huu, watuhumiwa watatu wa ujambazi, walikamatwa eneo la Kiwalani Kwa Mkude jijini Dar es Salaam wakiwa na bastola moja.

    Chanzo HabariLeo.

    Polisi Zanzibar Kuwahoji Watu 34 Wanaotumia Lugha ya Matusi Katika Mitandao ya Kijamii

    By: Unknown On: 22:12
  • Share The Gag

  • JESHI la Polisi Zanzibar limetoa tahadhari kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wanaitumia kwa kuwatukana viongozi wa kitaifa, huku likiwa na orodha ya watu 34 ambao wanatarajiwa kuhojiwa zaidi kutokana na matumizi mabaya ya mitandao hiyo.

    Kauli hiyo imetolewa juzi na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Salum Msangi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.

    Alisema hivi sasa baadhi ya watu wanaitumia mitandao hiyo kinyume na maadili jambo ambalo linaweza kusababisha chuki na uhasama na kwamba ni kinyume na maadili ya wananchi wa Unguja na Pemba.

    Msangi alisema jeshi hilo linakusudia kuwahoji watu 34 wanaotumia mitandao hiyo ya kijamii kwa kuhamasisha vurugu pamoja na kutoa lugha za matusi kwa viongozi wa Zanzibar, jambo ambalo ni kinyume na sheria pamoja na utamaduni wa wananchi wa Zanzibar.

    Alisema mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, kumejitokeza baadhi ya watu na vikundi mbalimbali vinavyotumia mitandao ya kijamii kwa kuandika maneno ya matusi au kutoa video za kuzungumza zenye lugha ya matusi kwa kuwatukana watu mbalimbali hasa viongozi wa kitaifa.

    “Tayari orodha ya watu hao imeshapatikana na hadi sasa Polisi inamshikilia kwa mahojiano na uchunguzi mtu mmoja ambaye anatuhumiwa kutoa moja ya video hizo zenye lugha ya matusi dhidi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein,” alisema.

    Aidha alisema kuwa uchunguzi wa kitaalamu na kisayansi unaendelea na ukishakamilika jalada litafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kulisoma na kulifikisha kwenye hatua zinazofuata.

    Msangi alitoa tahadhari kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwani kutumia lugha za matusi ni kosa lililoainishwa kisheria kwenye sheria ya kanuni ya adhabu, yoyote atakayetenda kitendo hicho atakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, bila ya kujali limetolewa mahali gani au wakati gani.

    Hata hivyo alisema kuwa wapo watu wanaodhani kuwa demokrasia ni uhuru wa kuwatukana viongozi, jambo ambalo sio sahihi na halikubaliki kisheria na kinyume na maadili ya wananchi wa Tanzania ambao wamejengwa na utamaduni wa kuheshimu watu.

    Msangi ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Polisi Zanzibar, alisema orodha ya watu wanaojiuhusisha na vitendo hivyo wanayo na wataendelea kukamatwa mmoja baada ya mwingine na kuchukuliwa hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria.

    Hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein alikemea tabia iliyojitokeza sasa ya matumizi mabaya ya mitandao.
    Credit; Mpekuzi blog

    Morogoro waomba Ulanga kuwa mkoa

    By: Unknown On: 22:10
  • Share The Gag

  • Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe

    WAJUMBE wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Morogoro (RCC) wamepitisha pendekezo la uanzishwaji mkoa mpya wa Ulanga, ambao utakuwa na wilaya tatu za Kilombero, Malinyi na Ulanga.
    Mkoa huo mpya, utatokana na kugawanywa mkoa mama wa Morogoro.
    Pendekezo hilo lilifikiwa baada ya kupitishwa na vikao vya ushauri vya halmashauri za wilaya (DCC) za mkoa wa Morogoro na kufikishwa kujadiliwa na kupitishwa katika kikao cha RCC, kilichofanyika juzi chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa, Dk Rajab Rutengwe.
    Kwa sasa mkoa wa Morogoro una wilaya saba za Morogoro, Kilosa, Mvomero, Gairo, Kilombero, Ulanga, Malinyi na una eneo la kilometa za mraba 73,039.
    Eneo hilo ni sawa na asilimia 7.7 ya eneo lote la Tanzania Bara.
    Katika kikao hicho cha RCC, Dk Rutengwe aliwaagiza watendaji wa serikali za wilaya, kukamilisha taratibu mbalimbali za kisheria na kuwashirikisha wananchi kabla ya kufikiwa hatua za mwisho za uwasilishaji rasmi wa pendekezo la kuanzishwa mkoa mpya kwa mamlaka zinazohusika.
    Alitumia pia kikao hicho, kuagiza maofisa mipango miji na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero kuandaa michoro ya mipango miji ya kisasa, itakayokidhi upatikanaji wa huduma zote muhimu za kiuchumi na kijamii.
    Awali, Mkuu wa Mkoa huyo aliliwasilisha pendekezo hilo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili kati ya Februari 22 na 23, mwaka huu mkoani Morogoro.
    Dk Rutengwe alisema mchakato huo, ulianza kufanyika tangu mwaka 2014 na sasa umefikia mahali pazuri, kwa kuwa suala hilo limefikishwa mezani kwake na kuwa limetokana na mazingira ya kijiografia na ukubwa wa mkoa huo, lengo likiwa ni kusogeza huduma za kijamii na kiutawala karibu na wananchi.

    Chanzo HabariLeo.

    Friday, 26 February 2016

    Orodha Ya Majina ya Wanafunzi wa St. Joseph Kampasi ya Songea Waliohamishiwa Vyuo Vingine Baada ya TCU Kukifuta Chuo Hicho

    By: Unknown On: 22:42
  • Share The Gag
  • http://www.tcu.go.tz/images/pdf/Students%20from%20SJUCAST%20&%20SJUCIT%20%20to%20other%20institutions_25_02_2016.pdf

    The Tanzania Commission for Universities (TCU) wishes to inform the general public and particularly students, who were undertaking their studies at St Joseph University College of Agricultural Sciences and Technology (SJCAST) and St Joseph University College of Information Technology (SJCIT) in Songea, that we have transferred the respective students to other universities. 

    These students are required to report to the receiving institutions upon the opening of the second semester.

    The dates for opening of the second semester for each receiving institution will soon be communicated through TCU website and websites of respective institutions.
     
    Meanwhile, TCU hereby releases the list of names of the transferred students, which contains receiving institutions and the programmes they have been transferred to.
     
    TCU would also like to inform respective students including those with Diplomas that there are names of some students, which are yet to be posted as we are continuing with the verification of their data. 

    These names shall be posted as soon as the verification exercise is completed.
     
    For further information or clarification please contact the Tanzania Commission for Universities through the following numbers;
     
    Landline: +255 (0) 222 772 657 
    Hotlines : +255 (0) 683 921 928
                    +255 (0) 675 077 673
     
    Credit; Mpekuzi blog

    Majambazi Dar es Salaam Yavamia Benki Ya Access....Yaua Mlinzi na Kupora Pesa, Polisi Wapambana Nayo na Kuyaua

    By: Unknown On: 22:36
  • Share The Gag

  • Majambazi  ambao  idadi  yao  haikufahamika  wakiwa  na  mabomu  na  bunduki  za  kisasa  jana  walivamia  Benki  ya  Access  tawi  la Mbagala  ambako  walipora  viroba vya   fedha, kuua  mlinzi  na  baadae wanne  kati  yao  waliuawa  na  jeshi  la  polisi.

    Watu  walioshuhudia  tukio  hilo  walisema  baada  ya  majambazi  hao  kufika  katika  benki  hiyo  kwa  bodaboda  nne  majira  ya saa  nane  mchana,yalimuua  mlinzi  wa  benki  hiyo, kusha  kubomoa  kwa  risasi  mlango  wa  vioo  na  kuingia  ndani  na  kuzua taharuki  kubwa

    Mashuhuda  hao  walisema, katika  tukio  hilo  lililodumu  kwa  karibu saa  moja,mmoja  wa  majambazi  hao  aliyekuwa  amevaa  kininja,alikuwa barabarani  akiamuru  magari  kupita  haraka  huku  akifyatua  risasi  hovyo.

    Ilielezwa  kuwa, jambazi  huyo  aliyeonekana  kuwa  na  uzoefu  wa  matumizi  ya  bunduki  alikuwa  akifyatua  risasi  kwa  kutumia  mkono  mmoja  na  ndiye  aliyewajeruhi  baadhi  ya  wapita  njia.

    Hivyo,wakati  uporaji  ukiendelea  na  jambazi  huyo  akiimarisha  ulinzi  barabarani  baadae  hakukuwa  na  magari  wala  pikipiki  zilizokuwa  zikipita.

    Mfanyabiashara  wa  duka  la  vifaa  vya  ujenzi  jirani  na  benki  hiyo,Ramadhani Tairo  alisema  baada  ya  jambazi  huyo  kuliona  gari  la  polisi  likielekea  eneo  la  tukio,alifyatua  risasi  na kulipiga  kabla  halijafika.Gari  hilo  lilipoteza  mwelekeo  na  kutumbukia  mtaroni.

    Tairo  alisema  mbali  na  jambazi  huyo  kulipiga  risasi  gari  la polisi  pia  alilirushia  bomu  la  mkono,lakini  liliangukia  barabarani  bila  kuripuka.Polisi  walifanikiwa  kulilipua  bomu  hilo  baadae  likiwa  halijasababisha  madhara  kwa wananchi  waliofika  kushuhudia  tukio  hilo.

    Mkazi  mwingine  wa  eneo  hilo,Rebecca  Maliva  alisema  majambazi  walioingia  ndani  ya  benki  hiyo  walioneka  wakitoka  na  viroba  vitatu vya  fedha  ambavyo  walivipakata kwenye  pikipiki  na  kuondoka  kwa  kasi  kuelekea  Mkuranga kupitia  barabara  ya  Kilwa.

    Rebecca  alisema  polisi  zaidi  walifika  kwenye  eneo  hilo  wengine  wakiwa  kwenye  pikipiki  na  kuanza  kuwafukuza  majambazi  hao  ambapo  walipofika  eneo  la  shule  ya  St. Marry's,walitupa  kiroba  kimoja  cha  fedha  ambacho  wananchi  waliokuwa    jirani  waligombania  na  kuchukua  fedha  zilizokuwemo  na   kisha  kila  mmoja  kukimbia  na  burungutu  la  noti.

    Baada  ya  nusu  saa  wakati  umati  ukiwa  bado  upo  kwenye  benki  hiyo,magari  ya  polisi  yalipita  katika eneo  hilo  yakitokea  eneo  la  Mkuranga  yakiwa  yamebeba  miili  ya  majambazi  yaliyouawa.

    Magari  hayo  yalikuwa  yakisindikizwa  na  vijana  wa  bodaboda  waliokuwa  wakishangilia  kazi  iliyofanywa  na  polisi.

    Kamanda  wa  p[olisi  kanda  maalum ya  Dar es Salaam, Simon Sirro  alizungumzia  kwa  ufupi  tukio  hilo n kwamba  majambazi  manne  yaliuawa  na  kukamata  silaha  tatu,lakini  hakutaka  kuingia  kwa  ndani  akisema  atatoa  taarifa  zaidi  leo
    Credit;Mpekuzi blog

    Meneja Vipindi wa kituo cha televisheni cha East Africa (EATV) Afikishwa Mahakamani Kwa Kuhifadhi Raia Wa Kigeni

    By: Unknown On: 22:35
  • Share The Gag

  • WATU wawili akiwemo Meneja Vipindi wa kituo cha televisheni cha East Africa (EATV), Lidya Igarabuza (37) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kuishi nchini bila kibali.

    Igarabuza ambaye ni mtanzania na raia wa Kenya, David Wachila (36), ambaye anadaiwa kuwa ni DJ wa muziki katika kituo hicho cha televisheni, walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkazi, Kwey Rusema.

    Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Khadija Masoud alidai kuwa Februari 25, mwaka huu katika maeneo ya Mikocheni A, Wachila akiwa raia wa Kenya, alikutwa akiishi nchini bila kibali jambo ambalo ni kinyume cha Sheria za Uhamiaji. Katika mashitaka yanayomkabili, Igarabuza anadaiwa kumhifadhi Wachila jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

    Inadaiwa Februari 25, mwaka huu huko maeneo ya Mikocheni, Igarabuza alikutwa amemhifadhi Wachila huku akijua jambo hilo ni kinyume cha sheria. Washitakiwa walikiri kutenda makosa hayo.

    Wakili Masoud aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali. Hakimu Rusema aliahirisha kesi hiyo hadi Machi Mosi, mwaka huu. Igarabuza aliachiwa kwa dhamana wakati mshitakiwa Wachila akirudishwa rumande kwa kukosa wadhamini.
     
    Credit; Mpekuzi blog

    CUF Kuandamana Kupinga Marudio Ya Uchaguzi Zanzibar

    By: Unknown On: 22:33
  • Share The Gag

  • CHAMA cha Wananchi (CUF) Bukoba kimejiandaa kufanya maandamano ya amani keshokutwa, kwa ajili ya kupinga kufanyika upya uchaguzi wa Zanzibar unaotarajiwa kuwa Machi mwaka huu.

    Kimeiomba pia serikali ya awamu ya tano, kuchukua uamuzi wa kumtambua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa urais Zanzibar na kuwa hakiko tayari kurudia uchaguzi huo tena.

    Akizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama hicho, Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Saverina Mwijage, alisisitiza kuwa kamwe chama hicho hakitakuwa tayari kurudia uchaguzi huo uliotangazwa na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa utafanyika Machi 20,kwa kile kinachodaiwa ni kufutwa uchaguzi wa Oktoba 25,mwaka jana.

    “Tumedhamiria kuandamana ili kumfikishia ujumbe wetu Rais John Magufuli kupitia kwa Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella lengo letu hasa ni kupinga uchaguzi wa Zanzibar. Hali ya Zanzibar kwa sasa haiko shwari, watu wanatishiwa maisha yao, wanaishi kwa hofu juu ya maisha,” alisisitiza.

    Mwijage ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF Taifa, alisema chama hicho kinatambua uchaguzi ulishakwisha na tume hiyo ilishatoa vyeti kwa walioshinda, kwa mantiki hiyo CUF inamtambua Maalim Seif kuwa alishinda katika uchaguzi huo.

    Alisema maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri na baadaye utakuwepo mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mayunga ulioko mjini Bukoba ili kuutangazia umma juu ya msimamo wa chama hicho na baada ya hapo watazunguka katika wilaya za Muleba, Missenyi na Karagwe.
    Credit; Mpekuzi blog

    Kila la heri Yanga

    By: Unknown On: 22:27
  • Share The Gag


  • WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa ngazi ya klabu, timu ya soka ya Yanga leo itashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikipeperusha bendera ya nchi.
    Yanga itakuwa kibaruani kuoneshana umwamba na timu ya Cercle de Joachim ya Mauritius katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika ugenini, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, hivyo leo inahitaji ushindi ama sare tu itakuwa imesonga mbele.
    Watanzania sote tunajua umuhimu wa mchezo huu, tunatambua namna gani nchi yetu itapata sifa kama Yanga itaibuka kidedea. Tunaitakia kila la heri Yanga, huku tukiamini watawapa mashabiki furaha na si karaha kwani ndoto yao ni kufika mafanikio makubwa zaidi.
    Ni vyema mashabiki sote bila kuangalia klabu gani wanayoipenda hapa nchini, tushirikiane kuitakia heri Yanga na kwa wale watakaopata fursa waende wakaishangilie na wengine waiombee dua tunaamini zitafika. Hakuna haja ya kuiona Yanga kama timu ya nchi nyingine, hivyo kuitakia mabaya kwa kisingizio chochote kile.
    Tuna kila sababu ya kuona mchezo wa leo una umuhimu mkubwa kwetu sisi Watanzania hasa kipindi hiki tunachohaha kujaribu kuinua soka letu. Kwa upande wa wachezaji wenyewe nao lazima wahakikishe wanapigana kufa au kupona ili ushindi upatikane.
    Tunaamini wachezaji wa Yanga wamejiandaa vya kutosha, wamepewa kila aina ya hamasa na pia wamelipwa vizuri ili wasiwe na malalamiko badala yake wawe na kazi moja tu ya kuhakikisha wanaleta ushindi.
    Tuweke akilini kuwa kwa vile wenzetu tuliwafunga kwao bao 1-0, hata wao wanaweza pia kutufunga kwetu, hivyo tusibweteke badala yake tuone kama nasi tuna deni kubwa. Tunasema wachezaji wa Yanga watambue umuhimu wa mchezo wa marudiano na nafasi yao ya kuzidi kuwatangaza kimataifa.
    Ni imani yetu kwamba benchi la ufundi la Yanga likiongozwa na Hans Pluijm litakuwa imara kuhakikisha wachezaji wanacheza kwa ushirikiano na uelewano dimbani. Kikubwa ni kwamba tunakutana na timu ambayo si mara ya kwanza kukutana nao, tumecheza nao kwao, tunawafahamu vizuri, lakini zaidi ni Waafrika wenzetu na tuliwafunga kwao.
    Wanaocheza uwanjani ni wachezaji 11 kila upande, hivyo hatudhani kama tuna haja ya kuingia tukiwa wanyonge, wala hatuna sababu ya kuhofia chochote. Tupo nyumbani tupate ushindi mnono.

    Chanzo HabariLeo.

    Mawaziri Wote Waliopewa Hadi Leo Jioni Kujaza Na Kurejesha Tamko La Mali Na Madeni, Hati Ya Uadilifu Wametekeleza Agizo La Rais Katika Muda Muafaka

    By: Unknown On: 22:20
  • Share The Gag
  • WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema agizo lilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli la kuwataka mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni wakamilishe kabla ya saa 12 leo jioni limetekelezwa.

    Waziri Mkuu amepokea barua kutoka kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji (Mst.) Salome Kaganda ikithibitisha kuwa mawaziri na naibu mawaziri wote wametekeleza agizo hilo.

    “Hadi kufikia saa 9.30 leo alasiri (Ijumaa, Februari 26, 2016) mawaziri wote walikuwa wamekamilisha fomu zao za kuzikabidhi katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,” alisema Waziri Mkuu.

    Rais Magufuli leo asubuhi alitoa maelekezo kwamba Mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni ifikapo leo Ijumaa tarehe 26 Februari, 2016 saa 12.00 jioni wawe wamejaza na kurejesha Fomu ya Tamko la Rasilimali na Madeni katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam. Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake.

    Mawaziri waliotakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi (OMR – Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba. 
     
    Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga ambaye alitakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako ambaye alitakiwa kutoa tamko la rasilmali na madeni.

    Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira), Mhe. Luhaga Mpina alitakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilmali na madeni pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.

    IMETOLEWA NA:
    OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
    S.  L. P. 3021,11410 DAR ES SALAAM.
    IJUMAA, FEBRUARI 26, 2016
    ==

    Credit;Mpekuzi blog

    Tanesco yataka kupandisha bei ya umeme

    By: Unknown On: 22:18
  • Share The Gag
  • SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limepeleka maombi kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuomba kupandisha bei ya nishati hiyo, kinyume na matakwa ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ya kushusha bei hiyo.
    Taarifa ya Ewura kwa umma iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa maombi hayo yamepokewa Jumatano ya wiki hii na kutaka wadau kujitokeza kujadili uhalali wa nyongeza hiyo siku mkutano huo utakapoitishwa.
    “Mamlaka inaanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau, ili kujua uhalali wa maombi ya nyongeza ya bei za huduma iliyoyapokea kutoka Tanesco,” imeeleza taarifa hiyo.
    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanesco iliwasilisha ombi husika kulingana na Sheria ya Umeme namba 131, inayoitaka Ewura kufanya mabadiliko ya bei zinazotozwa na mtoa huduma mara moja kila baada ya miaka mitatu.
    “Pendekezo la wastani wa badiliko la bei za umeme ni asilimia 1.1 kuanzia Aprili mosi 2016 na asilimia 7.9 kuanzia Januari mosi 2017,” limeeleza tangazo hilo.
    Mapendekezo hayo japo ya kisheria, lakini yanapingana na msimamo wa Waziri Muhongo, ambaye tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, alielezea kusudio lake la kutaka bei ya nishati hiyo ishushwe.
    Profesa Muhongo alikwenda mbali na kuagiza Tanesco, Ewura na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa bei ya umeme kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.
    Katika maagizo hayo, Profesa Muhongo alihoji kwa nini bei ya umeme isishuke, wakati gharama za uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta zimeshuka kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
    Kutokana na maombi hayo ya Tanesco, Ewura imewataka wadau wa nishati wanaopenda kutoa maoni yao kwa maandishi, kufanya hivyo kwa kutuma maoni yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, ghorofa ya saba jengo la LAPF Pensions Fund Tower, mkabala na Kijiji cha Makumbusho, Kijitonyama Dar es Salaam.
    Kwa watakaotuma kwa njia ya posta, wameombwa kufanya hivyo kwa kutumia Sanduku la Posta 72175, Dar es Salaam, Tanzania, simu namba (+255-22) 2123853-4; Fax namba (+255-22) 2123180; Barua pepe info@energyregulators.org au tovuti http://www. energyregulators. org.
    Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamlaka hiyo pia, itaitisha mikutano ya wazi ili kukusanya maoni kuhusu mapendekezo hayo kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwamo Baraza la Wawakilishi wa Watumiaji wa Huduma (CCC); Baraza la Ushauri la Serikali (GCC) pamoja na wananchi kwa ujumla.

    Chanzo HabariLeo.

    TCU yafuta kibali cha Chuo Kikuu St. Joseph Arusha

    By: Unknown On: 22:14
  • Share The Gag

  • Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya

    TUME ya Vyuo Vikuu (TCU), imefuta kibali kilichoanzisha Chuo Kikuu cha St Joseph tawi la Arusha na kuahidi kuhamishia wanafunzi 1,557 wa chuo hicho kwenda vyuo vingine.
    Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya alisema, hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo migogoro ya muda mrefu baina ya uongozi wa chuo hicho na wanafunzi.
    “TCU inapenda kuutaarifu umma kuwa imekifungia chuo hicho kwa kuwa hakina uwezo wa kutoa elimu ya juu na wanafunzi ndio waathirika wakuu,” alisema.
    Kutokana na hatua hiyo, Profesa Mgaya alisema wameanza kuhamisha wanafunzi na kuwapeleka kwenye vyuo vingine na kuwataka wanafunzi hao kuangalia mtandao wa TCU kubaini vyuo walivyopangiwa na kabla ya kuhamia vyuo hivyo, wakamilishe taratibu zote.
    Alisema, tume imekuwa ikifuatilia kwa karibu migogoro hiyo na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa uongozi wa chuo kurekebisha kasoro zinazosababisha migogoro chuoni hapo.
    Katika kutekeleza azma hiyo, tume iliunda jopo la wataalamu kufanya ukaguzi wa kina katika chuo kikuu hicho na ripoti ya ukaguzi huo iliwasilishwa Februari 22 mwaka huu.
    Baada ya kupokea ripoti hiyo na kuifanyia kazi, Profesa Mgaya alisema waliofikia uamuzi huo kwani uongozi wa chuo hicho, licha ya kushauriwa na TCU kurekebisha kasoro zilizopo, haukuchukua hatua husika.
    Wiki hii wanafunzi 1,548 wa chuo hicho waligoma kuingia darasani kwa siku tatu na kukodi mabasi matatu kwa nia ya kutaka kufika Dar es Salaam kumwona Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
    Lengo la safari yao hiyo ya Dar es Salaam, ilikuwa ni kujua hatma yao baada ya TCU, kufungia chuo hicho tawi la Songea.
    Hata hivyo, Profesa Mgaya aliwataka kuwa watulivu na kuahidi kuzungumzia hatma ya chuo hicho jana, baada ya tume hiyo kupitia mapendekezo ya wataalamu iliyoundwa mapema kwa ajili ya ukaguzi wa chuo hicho, tawi la Arusha.

    Chanzo HabariLeo.

    Nape atoa rungu kwa magazeti ya Serikali

    By: Unknown On: 22:11
  • Share The Gag
  • Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye akizungumza na  wafanyakazi wa Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers Ltd (TSN) inayochapisha magazeti ya Serikali ya Daily News, Sunday News, HabariLeo na SpotiLeo. Waziri alifanya ziara katika Ofisi TSN barabara ya Nandera jijini Dar es salaam.

    WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametaka magazeti ya Serikali kumsaidia Rais John Magufuli, kutumbua majipu kwa kuibua uozo serikalini.
    Akizungumza katika kikao cha wafanyakazi wa Kampuni ya Tanzania Standard (Newspapers) Ltd Dar es Salaam jana, inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na Spotileo, Nape ametaka magazeti hayo yasimung’unye maneno kwa kuandika ukweli; kwenye nyeusi yaandike nyeusi na kwenye nyeupe, yaandike nyeupe.
    Alisema vyombo vya habari vya Serikali vina wajibu wa kumsaidia Rais kutumbua majipu kwa kuandika habari bila woga, upendeleo wala kuomuonea mtu, ili kama kuna dosari ziko mahali ziibuliwe kwa lengo la kupata suluhu.
    “Unajua vyombo vya habari vinaaminika na vinasomwa na wengi na hasa wananchi wanapotaka ukweli wa jambo, wanaangalia kama limeandikwa, sasa kama jambo litaandikwa kwa kufichwa fichwa haitaisaidia Serikali, kama ni nyeusi sema nyeusi, kama ni nyeupe sema nyeupe na hiyo ndiyo suluhu,” alisisitiza Nape.
    Alisema majipu yanayoendelea kutumbuliwa na Rais, mengine yanaibuliwa na vyombo vya habari na ili kumsaidia na kusaidia Taifa, vyombo vya habari vya Serikali lazima viibue hayo, pia viaminiwe mpaka na watumishi wa Serikali, wavitumie kuibua uozo.
    Nape alisisitiza kwamba kuficha ukweli kwenye jambo ovu, ni kuendelea kuharibu hivyo kuibuliwa kwa maovu kutaisaidia Serikali na watendaji wake kuchukua hatua madhubuti. “Kuna hili jambo la baadhi ya watendaji kusema mfumo hautaki hili, hakuna cha mfumo ni maneno yao wanayatumia kama kichaka cha kufanya uchafu,” alisema Nape.
    Nape alitoa onyo kwa watendaji wa serikali kuacha tabia ya kuzuia habari zisitoke kwa maslahi yao na kutaka wenye pingamizi ya kutoka kwa habari, wawasiliane naye na si kuingilia chombo cha habari.
    Katika taarifa ya wafanyakazi wa TSN kwa Waziri huyo, walimuomba kuangalia changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na maslahi duni, uhaba wa vitendea kazi na baadhi ya viongozi kufanya uamuzi kwa kukiuka sheria na utaratibu.
    Akijibu hoja kuhusu Muundo wa Utumishi wa kampuni hiyo, ambao umelalamikiwa na wafanyakazi kuwa umepitwa na wakati na umekuwa na malalamiko mengi ya upendeleo, Nape alitoa mwezi mmoja kwa Menejimenti ya TSN, kulifanyia kazi na kulimaliza.
    “Sipendi kufukuza watu kazi, ila inapobidi itafanyika, natoa mwezi mmoja menejimenti na mtu wa utumishi kaeni, pitieni muundo huo... kwanza umeisha muda wake uletwe mpya na wafanyakazi walipwe malimbikizo ya nyongeza ya mishahara kwa muda wote ambao hawajaongezwa,” alisisitiza Nape.
    Kuhusu Mkataba wa Hali Bora kwa Wafanyakazi, Waziri Nape alitoa siku saba kwa Menejimenti ya TSN kupitia upya mkataba huo na kuhakikisha unazingatia maslahi ya watumishi.
    Akizungumzia dosari nyingine zilizopo katika kampuni, Nape alisema ukaguzi mkubwa wa hesabu za kampuni utafanywa na ripoti yake itatumika kuchukua hatua zaidi kwa wahusika.
    Akizungumzia miradi ya kampuni ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikizungumzwa bila kutekelezwa, Nape aliagiza mikabata yote ya miradi hiyo ipelekwe mezani kwake, ili ichunguzwe kuona wapi imekwama.
    Nape alisema ni vyema watendaji wanapokubaliana na wafanyakazi, utekelezaji ufanyike na wanapoona wameshindwa, ni vyema kurudi mezani kuwaeleza watumishi, badala ya kukaa kimya.
    “Tujenge utamaduni wa kuheshimu taratibu tunazojiwekea, kama mlikubaliana mambo, mkashindwa kutekeleza ni vyema mkarudi mezani kuzungumza na si kukaa kimya, jambo ambalo wafanyakazi wanatafsiri wanavyojua wao,” alisema Nape.
    Aliagiza menejimenti ya TSN, kuweka wazi kwa sifa na vigezo mambo yanayowahusu watumishi ikiwa ni pamoja na muundo wa utumishi, upandishwaji madaraja na mshahara ili watumishi wasinung’unike na kila mmoja ajue kesho yake baada ya kujiendeleza.
    Awali Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (Raawu) tawi la TSN, Oscar Mbuza, alimkabidhi Waziri Nape orodha ya mambo ambayo wafanyakazi wamekuwa wakiyadai kwa miaka mingi bila mafanikio na kusema ujio wa Waziri huyo utaleta suluhu, kwani morali ya watumishi kazini ilishuka.
    “Wafanyakazi pamoja na kuendelea kufanya kazi, lakini morali ya kazi imeshuka kwa kiwango kikubwa sana, hii ni kwa sababu ya maslahi duni ya wafanyakazi ya muda mrefu, ila ujio wako tunatumaini utaleta suluhu na watumishi watapata ari mpya ya kufanya kazi,” alisema Mbuza.


    Chanzo HabariLeo.

    Tuesday, 23 February 2016

    Barcelona yaicharaza Arsenal UEFA

    By: Unknown On: 23:29
  • Share The Gag
  • Barcelona yaiadhibu Arsenal kwa mabao 2-0
    Klabu ya soka ya Barcelona imefanikiwa kuchomoza na ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Arsenal katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Mtoano ya Timu 16 ya klabu bingwa barani ulaya (UEFA) mchezo uliopigwa uwanja wa Emirates. Mabao ya Barcelona katika mchezo huo yamefungwa na mchezaji Lionel Messi dakika ya 71 na Dakika ya 83 likiwa ni bao la pili lililofungwa kwa njia ya penati .
    Messi alifunga mabao yote mawili Katika mchezo mwingine Juventus wakiwa nyumbani dhidi ya Buyern Munich, mchezo huo umemalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu kufuatia sare ya kufungana mabao 2-2.
    Bayern Munich ndio walioanza kuzigusa nyavu za wapinzani kwa kuandika bao la kuongoza kupitia kwa mchezaji wao Thomas Muller dakika ya 43, muda mchache baadaye Arjen Robben akaandika bao la pili kwa buyen Munich katika dakika ya 55 kipindi cha pili.
    Kwa upande wao Juventus walizinduka na kuandika bao la kwanza kupitia kwa Paulo Dybala ikiwa ni dakika ya 63 kipindi cha pili, huku Stefano Sturaro akiandika bao la pili la kusawazisha dakika ya 76 na kuufanya mchezo umalizike kwa sare ya kufungana bao 2-2.
    Michuano hiyo itaendelea tena Jumatano kwa Mechi 2 Dynamo Kiev ikiikaribisha Man City huko Ukraine na PSV Eindhoven wao watakuwa Wenyeji huko Uholanzi dhidi ya Atletico Madrid.

    Chanzo BBC Swahili.

    Wagombea wa Republican washindania Nevada

    By: Unknown On: 22:57
  • Share The Gag
  • Trump amekuwa akiongoza kwenye kura za maoni
    Wagombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani wanakabiliana kwenye uchaguzi wa mchujo katika jimbo la Nevada katika kinyang’anyiro cha nne cha kuamua mgombea wa chama hicho.
    Mfanyabiashara Donald Trump, ambaye amekuwa akiongoza kwenye kura za maoni kitaifa, anaongoza pia kwenye kura za maoni jimbo hilo, na anatarajia kupata ushindi wa tatu mtawalia baada ya kushinda New Hampshire na South Carolina.
    Nevada, ambalo ni jimbo lisilo na mbabe na lenye watu wengi wa asili ya Amerika Kusini, ni muhimu sana katika uchaguzi.
    Upigaji kura kwa sasa unaendelea na kuna foleni ndefu vituoni.
    Kura ya maoni ya karibuni CNN/ORC imeonesha Trump ana uungwaji mkono 45% akifuatwa na Seneta Marco Rubio 19% naye Seneta Ted Cruz akiwa na 17%.
    Ingawa Nevada ina wajumbe wachache, inatarajiwa kuwa mtihani kwa Trump kutokana na matamshi yake dhidi ya wahamiaji ikizingatiwa kwamba ina watu wengi wa asili ya Amerika Kusini.
    Hillary Clinton alishinda kwenye jimbo hilo katika chama cha Democratic Jumamosi.
    Alimshinda mpinzani wake Bernie Sanders kwa kumpita kwa asilimia tano na wagombea hao wawili sasa wanaangazia jimbo la South Carolina lenye watu wengi weusi.
    Uchaguzi wa mchujo wa chama cha Republican katika jimbo la South Carolina utafanyika Jumamosi.
    Uchaguzi wa mchujo hutumiwa kuchagua wagombea wa vyama viwili vikuu kwenye uchaguzi mkuu wa urais ambao utafanyika mwezi Novemba.

    Chanzo BBC Swahili.

    Uhamiaji wasafishwa Dar na Kilimanjaro

    By: Unknown On: 22:38
  • Share The Gag

  • Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga
    WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ameagiza watumishi wa Idara ya Uhamiaji walioko katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na Kilimanjaro (KIA), wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini, wakiwemo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
    Katika maagizo ya waziri huyo, amesisitiza kuwa anataka kuwepo na mabadiliko makubwa katika vitengo mbalimbali vya idara ya uhamiaji ili kuboresha huduma na kuimarisha uadilifu katika vitengo hivyo.
    Aidha, utafiti uliofanywa hivi karibuni, umeonesha kuwa matatizo ya rushwa katika idara ya uhamiaji, yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka.
    Kitwanga alitoa maagizo hayo Dar es Salaam jana, alipozungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa idara ya uhamiaji na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara.
    Pamoja na watumishi hao wa Idara ya Uhamiaji wa viwanja hivyo vya ndege kutakiwa kuhamishwa, wengine walioagizwa na waziri huyo kuhamishwa ni kutoka Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
    Aidha, ameagiza pia kuwa Wakuu wote wa Vitengo vya Upelelezi vya wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam, Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo mengine, wakiwemo watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika vituo hivyo.
    “Hatua hii inayochukuliwa ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja ya Idara muhimu za Serikali,” alisisitiza Kitwanga.
    Alisema katika kuisafisha idara hiyo, uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa hakuna mtumishi anayeonewa wala kupendelewa, lengo likiwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wasiowajibika.
    Alisema kutokana na utafiti uliofanywa hivi karibuni, umeonesha kuwa matatizo ya rushwa katika Idara ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka.
    Aidha, alisema asilimia 15 inahusisha vitendea kazi, mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia 10 huduma mbovu na asilimia tano ukabila na upendeleo.
    Aliwataka viongozi na watumishi wote katika idara hiyo kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi na kuepuka vitendo vya kupokea rushwa na kusaidia wahamiaji haramu na wauza dawa za kulevya.

    Chanzo HabariLeo.

    Kampuni Ya Kichina Matatani Kwa Kutengeneza Vibao Vya Namba Za Magari Kinyume Cha Sheria

    By: Unknown On: 22:36
  • Share The Gag

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya msako wa kushtukiza katika kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development Ltd iliyoko Barabara ya Nyerere Dar es salaam baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema na kukamata vifaa pamoja na malighafi za kutengeneza na kutoa vibao vya namba za pikipiki kinyume na sheria.

    Katika msako huo uliofanyika tarehe 19 Februari 2016 katika kampuni hiyo, Maofisa wa TRA waliweza kukamata na kutaifisha vibao vyenye namba za pikipiki 2,500 na vibao 5,600 ambavyo havikuwa na namba. Pia maofisa wa TRA walikamata malighafi za rangi ya vibao katoni tatu, pamoja na mashine ya kupaka vibao rangi yenye uzito wa kilo 155.

    Mashine nyingine iliyokamatwa katika msako huo ni ya kutengeneza namba za magari yenye uzito wa kilo 902 ambayo imezuiwa isihamishwe kutoka katika kampuni hiyo pamoja na kompyuta mpakato ambayo imepelekwa katika maabara ya uchunguzi TRA kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

    Taarifa za kuwepo kwa utengenezaji wa vibao vya magari kinyume na taratibu na sheria zilitolewa na msamaria mwema ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni husika Donglinh Guo, Meneja wa Kiwanda Yong Qing Cheng na Meneja wa ghala Peng Zhan walikamatwa baada ya kutokea fujo wakati wa msako na kufikishwa katika kituo cha Polisi Changombe.

    Kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development LTd ndio waingizaji pekee wa pikipiki za Falcon tangu mwaka 2008 ambapo inatuhumiwa kutoa vibao vya namba za pikipiki kwa wateja wake kwa shilingi 5,000 kinyume na sheria.Uchunguzi wa thamani ya kodi iliyopotea bado unaendelea.
     
    Vibao vya magari na pikipiki hutolewa na kampuni ambazo zinatambuliwa na TRA baada ya kupewa idhini. Kampuni hizo ni Masasi Sign, Auto Zone, Sign Industry, Kiboko, Budda Auto works, Parkinson Ltd na Next Telecom.

    Ili kujiridhisha kuwa kadi za pikipiki zinazotolewa kwa wateja wa kampuni hiyo ni halali, TRA ilifanya uchunguzi na kugundua kuwa kadi hizo zinatolewa kihalali.

    TRA inawatahadharisha wananchi kufuata taratibu na sheria ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea endapo watagundulika kujihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria.
     
    Credit; Mpekuzi blog

    Ndege iliyowabeba watu 21 yatoweka Nepal

    By: Unknown On: 22:34
  • Share The Gag
  • Ndege ndogo iliyowabeba abiria 21 imetoweka ikiwa maeneo yenye milima nchini Nepal.
    Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Pokhara, magharibi mwa mji mkuu Kathmandu, kwenda Jomsom, eneo ambalo watu wengi wanaoenda kukwea milima ya Himalaya huanza safari yao ya kukwea milima hiyo.
    Hakuna viwanja vya ndege kati ya maeneo hayo mawili na inahofiwa kwamba ndege hiyo imeanguka.
    Ndege hiyo ni ya shirika la ndege la Tara Airlines.

    Chanzo BBC Swahili.

    Jengo la posta Dodoma lateketea kwa moto

    By: Unknown On: 22:31
  • Share The Gag

  • JENGO Posta lililopo katika eneo la sabasaba katika Manispaa ya Dodoma  jana limeteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa

    Akizungumzia kutekeleza kwa jengo hilo Meneja wa Posta Mkoa wa Dodoma, Magreth Mlyomi alisema mpaka sasa kuna hasara kubwa kutokana na kutekeleza jengo hilo sambamba na vifaa vyote vya ofisi.

    Mlyomi alisema licha ya kuwa hakuna mfanyakazi hata mmoja aliyepoteza maisha katika jengo hilo lakini mpaka sasa kuna vitendea kazi vingi vya ofisi pamoja na mizigo ya wateja imeteketea.

    “Kuna mizigo mingi pamoja na vifaa vya kazi vyote vimeteketezwa na moto na kwa taarifa nilizopata kulikuwa na mizigo ya watu, inaonesha kuwa chanzo cha moto ni umeme,” alieleza Meneja huyo.

    Akizungumzia kuhusu masuala ya miundombinu ya maeneo husika alisema ni mibovu na kutokana na changamoto hiyo suala hilo lipo katika mamlaka husika ya manispaa.

    Kwa upande wake katibu wa wafanyabiashara katika soko la Sabasaba katika Manispaa ya Dodoma, Gergod Lugusi alisema jana saa nne asubuhi kulitokea moto mkali ambao uliunguza jengo hilo.

    Alisema chanzo cha moto huo inasemakana kuwa ni tatizo la umeme na uongozi ulilazimika kutoa taarifa katika kikosi cha zima moto na bila kuchelewa walifika kwa wakati.

    Hata hivyo alisema licha ya kufika kwa wakati katika tukio bado kikosi hicho kilikutana na kikwazo kwa kutokana na miundombinu kuwa mibovu na migumu kupitika.
    Credit;Mpekuzi blog

    Utafiti zaidi wafanywa Brazil kuhusu Zika

    By: Unknown On: 22:27
  • Share The Gag
  • Wanasayansi wa Marekani wanachunguza uhusiano kati ya virusi vya Zika na hali ya watoto kuzaliwa na vichwa vidogo
    Wanasayansi kutoka kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa CDC nchini Marekani wameanza kufanya utafiti nchini Brazil ili kujua uhusiano kati ya Virusi vya Zika na watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo.
    Timu za wanasayansi zimekuwepo katika jimbo la Paraeeba, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, jimbo ambalo limeathirika zaidi na Virusi.
    Timu nane zinazoundwa na cdc na mawakala wa maswala ya afya walienda kwenye maeneo yaliyoathirika na kuchukua sampuli ya damu na kuwahoji wamama walioathirika na wamama ambao watoto wao walizaliwa wakiwa na vichwa vidogo.
    Katika kipindi cha majuma yajayo, watakusanya taarifa kutoka kwa mamia ya wamama katika jimbo la Paraeeba, jimbo la pili lililoathirika zaidi.
    Katika Ripoti ya siku ya jumanne Wizara ya Afya ya Brazil imethibitisha watoto 587 wana vichwa vidogo asilimia 75 zaidi ya wiki iliyopita huku maelfu ya watoto wanachunguzwa.
    Baada ya kutangazwa hali ya taadhari ya kiafya, Rais wa Shirika la Afya duniani, Margaret Chan aliwasili Brasilia kufuatilia hali ilivyo.
    Akiwa huko alikutana Rais wa Brazil,Dilma Roussef siku ya jumanne na kusema kuwa anafurahishwa na namna Serikali inavyoshughulikia tatizo hilo na kutaka jamii isaidiwe kupambana na mbu anayeeneza virusi vya Zika

    Chanzo BBC Swahili.

    Nkurunziza atuma salamu, asema Burundi ni shwari

    By: Unknown On: 22:23
  • Share The Gag

  • Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

    RAIS Pierre Nkurunziza wa Burundi amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa hali ya Burundi ni shwari na kwamba tangu juzi nchi hiyo imepokea ugeni mkubwa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na inatarajia kupokea marais watano kutoka nchi za Umoja wa Afrika kesho.
    Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, ujumbe wa Rais Nkurunziza umewasilishwa na Mjumbe Maalumu ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki wa Burundi, Leontina Nzeyimana Ikulu Dar es Salaam jana, alipokutana na Rais Magufuli na kufanya naye mazungumzo.
    Pamoja na kumpa taarifa kuwa Burundi inaendelea vizuri, Nzeyimana pia alimueleza Rais Magufuli kuwa Burundi ipo tayari kupokea nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kwa Rwanda, ikiwa ni kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaoelekeza kuwa nchi inayofuata kutoa Katibu Mkuu baada ya Katibu Mkuu wa sasa kumaliza muda wake, ni Burundi.
    Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu wanaowakilisha nchi zao nchini.
    Balozi wa Uholanzi nchini, Jaap Frederiks aliwasilisha salamu za Mfalme wa Uholanzi, Mtukufu Willem- Alexander ambaye amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa alizoonesha katika mwanzo wa utawala wake katika kusimamia uadilifu serikalini na katika biashara na pia kuisaidia Mahakama.
    Alisema Uholanzi inaamini kuwa maeneo hayo ndio yamekuwa yakileta vikwazo vya maendeleo, biashara na uwekezaji, na alimhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo kama ilivyofanya katika miaka 45 iliyopita huku akitaja baadhi ya maeneo ya ushirikiano kuwa ni kilimo na nishati.
    Balozi wa India nchini, Sandeep Arya aliwasilisha salamu za Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ambaye pamoja na kuitaja Tanzania kuwa lango muhimu katika mpango wake wa ushirikiano na Afrika, alimhakikishia kuwa India itaendeleza uhusiano wake na Tanzania hususani katika biashara na uwekezaji ikiwemo kuunga mkono mpango wa ujenzi wa viwanda Tanzania.
    Kwa upande wake, Rais Magufuli aliwahakikishia mabalozi hawa kuwa serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na nchi hizo.

    Chanzo HabariLeo.

    Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Akana Kutoa Amri ya Kufuta Matokeo ya Uchaguzi Zanzibar

    By: Unknown On: 22:21
  • Share The Gag


  • MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amesema hajahusika kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar kwa kumpigia simu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

    Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Chama ya Kibaha Mjini mkoani Pwani na kusema maneno hayo ni ya uongo, hayana ukweli wowote na watu hawapaswi kutoa shutuma hizo juu yake.

    Rais huyo wa Awamu ya Nne alisema maneno hayo hayana kichwa wala miguu wala hajawahi kumpigia simu Jecha kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwani tume hiyo inajitegemea.

    “Wasitoe lawama zisizohusika, wapuuzeni sikuwahi kufanya hivyo hata kwa Damian Lubuva wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania hivyo nashangaa watu wanavyosema kuwa nimehusika kufutwa uchaguzi huo,” alisema Kikwete.

    “Tume ya Zanzibar ni tume huru na inajitegemea kwani ina mambo yake hata Dk Ali Mohamed Shein (Rais wa Zanzibar) hana uwezo wa kuingilia na kuahirisha uchaguzi huo, watu hao wasipake watu matope wasio husika kwani kila mtu ana nafasi yake,” alifafanua Kikwete.

    Alisema kikubwa kinachotakiwa ni kuwaombea Wazanzibari wafanye uchaguzi wao mkuu wa marudio kwa amani na utulivu ili wapate viongozi wao wa kuiongoza Zanzibar na wawaombee wagombea wa CCM washinde.

    Aidha, alisema chama hicho kinapaswa kuwaadhibu watu waliokihujumu chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwa kutomwonea mwanachama, bali watende haki na si kwa kwa uonevu.

    Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao alisema Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka ameonesha njia ya kiongozi kutumia fursa kuboresha mazingira ya utendaji kazi Awali, Koka ambaye ndiye aliyejenga ofisi hiyo yenye thamani ya Sh milioni 100, alisema aliamua kujitolea kujenga ofisi hiyo kwa lengo la kukisaidia chama kiendeshe shughuli zake.

    Koka alisema aliamua kujenga kama kumbukumbu kwa wanaKibaha ili iwe kielelezo cha uongozi wake kama mbunge wa Jimbo hilo kwa ajili ya kufanya shughuli za chama badala ya kufanyia sehemu zisizo na hadhi yao.
    Credit;Mpekuzi blog