Thursday, 28 April 2016

Huduma Ya Treni Ya Abiria Kutoka Dar Kwenda Bara Kuanza Tena Jumapili Mei Mosi, 2016

By: Unknown On: 23:51
  • Share The Gag
  • Treni ya kwanza ya abiria ya Deluxe  kutoka Dar es Salaam kwenda bara itaondoka saa 2 asubuhi siku Jumapili Mei Mosi, 2016 kuelekea Kigoma.

    Kuanza kwa safari hiyo kunatokana na kutengemaa kwa eneo korofi baina ya  stesheni za  Kilosa mkoani  Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma. 

    Kwa mujibu wa taarifa ya Wakuu wa Idara za uendeshaji wa kampuni ya Reli Tanzania (TRL) iliyotolewa  Aprili  26, 2016 baada ya ukaguzi wa kina wa  eneo la Gulwe, imesema  sasa eneo hilo  linapitika  na kwamba tuta limeiamarika na kuwezesha treni zote za abiria na mizigo kupita kwa usalama kabisa.

    Mara ya mwisho huduma za treni za abiria ya kawaida zilihamishiwa Dodoma mnamo Aprili 07, 2016.

    Ratiba za safari treni ya kawaida kutoka Dar es salaam kuelekea Mwanza na Kigoma  ni kila siku ya Jumanne na Ijumaa saa 11 jioni ambayo imepangwa kuanza Jumanne Mei 3, 2016.Wakati treni ya  Deluxe inaondoka Dar es salaam kila Jumapili saa 2.00 asubuhi.

    Na kutoka Mwanza na Kigoma treni ya kawaida inatoka huko kila siku ya Alhamisi na Jumapili saa 11.00 jioni kwa Kigoma na saa 12 jioni kwa Mwanza. Treni ya DELUXE  nayo inatoka  Kigoma au Mwanza kila siku ya Jumanne saa 2.00 asubuhi.

    Wasafiri wote wanaombwa kufanya mipango  ya safari (booking) katika stesheni zetu husika na sio vinginevyo.
    Aidha taarifa za uhakika kuhusiana na taratibu  za safari zetu za treni za abiria  na  mizigo  zinapatikana  katika vituo vyetu vyote vya TRL.

    Uongozi wa kampuni  ya TRL  unawaomba radhi  wateja wake na wananchi kwa ujumla kwa usumbufu wowote uliojitokeza katika kipindi chote  hicho ambacho huduma zetu zilipokuwa zinaanzia na kuishia Dodoma badala ya Dar es salaam kama ilivyo kawaida.

    Aidha Kampuni inashukuru jitihada za  Serikali pamoja na taasisi zake kadhaa   kufanikisha kurejesha hali ya miundombinu  ya reli  katika hali yake ya kawaida.

    Imetolewa na Afisi ya Uhusiano:
    Kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
    Ndugu Masanja Kungu Kadogosa
    Aprili 28, 2016
    DAR ES SALAAM
    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    CHADEMA Yatangaza Kutoshiriki Kura ya Maoni ya Katiba Mpya

    By: Unknown On: 23:47
  • Share The Gag

  • DK. Vincent Mashinji Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema), amesema kuwa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi ndiyo msingi imara pekee unaoweza kuweka mifumo na taasisi kwa ajili ya maendeleo ya kweli yatakayogusa maslahi ya Watanzania wote badala ya nchi kuongozwa na kauli za viongozi.

    Kutokana na umuhimu huo wa kuzingatia maoni ya wananchi yanayobeba matakwa yao katika mchakato wa Katiba Mpya, amesema kuwa Chadema hakitashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa ambayo ilipitishwa na Bunge Maalum la Katiba baada ya kubadili na kuondoa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya.

    Badala yake, Chadema kitaendelea kuweka agenda ya kupigania Katiba Mpya na bora katika vipaumbele vyake, kwa sababu itatibu vidonda na kumaliza makovu yaliyoko katika jamii kutokana na matatizo mbalimbali kama vile ukosefu wa haki, migogoro ya ardhi, wananchi kukosa huduma za msingi za kijamii zikiwemo elimu, maji na afya.

    Dkt. Mashinji aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipoukaribisha ujumbe wa Chama cha Centre Party cha Norway uliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam kutia saini makubaliano ya ushirikiano kati ya vyama hivyo kwenye Mradi wa Elimu ya Demokrasia awamu ya pili unaofanyika Wilaya ya Mtwara Vijijini.

    Dkt. Mashinji pia amekishukuru chama hicho kwa kusaidia kutoa elimu ya uraia kwa Watanzania hususani maeneo ya vijijini katika mradi ambao unahusisha vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi ndani ya Bunge, huku akisisitiza kuwa Chadema kiko tayari kwa ushirikiano unaozingatia maslahi na matakwa ya wananchi hasa katika kukuza uelewa wa kudai haki, demokrasia na uongozi bora ndani ya nchi.

    “Suala la Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi kama ilivyowasilishwa kwenye rasimu ya pili na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ni agenda muhimu kwa Watanzania wapenda nchi yao na sisi ni kipaumbele kwa mwaka huu na kuendelea hadi hapo nchi yetu itakapopata Katiba Mpya ya Wananchi.

    “Jana na leo tumewasikia baadhi ya viongozi wa serikali wakisema kuwa wanajiandaa kuitisha kura ya maoni…hatutashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunajua Watanzania wengi wanataka Katiba Mpya iliyotokana na maoni yao, si ile iliyochakachuliwa bungeni.

    “Katiba Mpya iliweka masuala kuhusu haki za wananchi, kuimarisha misingi na kuweka mifumo ya demokrasia na uongozi bora, walau kwa kuanzia. Hatuwezi kusema sasa tutatumia mikakati gani kuwahamasisha Watanzania kuidai Katiba Mpya…tutajua namna ya kuvuka tukishafika mtoni,” Alisema

    Aidha, Katibu Mkuu Dkt. Mashinji alisisitiza kuwa suala la nchi kuwa na misingi na mifumo imara ya demokrasia na uongozi bora ni muhimu kwa Tanzania, katika wakati ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi mkubwa wa nishati ya gesi na mafuta, akisema vinginevyo ni hatari iwapo taifa lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, litaendelea kuwa na wananchi waliokata tamaa kutokana na mfumo mbovu uliopo.

    Kwa upande wake ujumbe huo uliokuwa ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Centre Party, Knut Olsen, ulisema kuwa chama hicho kinashukuru kwa mradi huo kuingia katika hatua ya pili kuanzia mwaka 2016-2019 huku hatua ya kwanza ikiwa na mafanikio makubwa katika jamii ya wananchi wa maeneo ya pembezoni.

    “Kama unavyojua, mradi huu kupitia TCD unahusisha vyama vyote vyenye uwakilishi ndani ya bunge, na lengo letu ni kuwajengea uwezo viongozi wa vyama hasa wanawake na vijana katika ngazi ya jamii kwenye vitongoji, vijiji, kata na bunge ili waweze kushiriki mchakato wa maamuzi. Tunatarajia kuendelea kupata ushirikiano katika hatua ya pili,” alisema Inger Bigum, ambaye ni Meneja wa Mradi hapa nchini.

    Wengine waliokuwa katika ujumbe huo wa Centre Party ni pamoja na Vijana Sara Hamre Katibu Mkuu wa, Katibu Mkuu wa Wanawake, Eline Stokstad-Oslan na Kristin Madsen Katibu Mkuu wa Wazee.
    Mradi huo wa Elimu ya Demokrasia katika Wilaya ya Mtwara Vijijini unaohusisha vyama vyenye uwakilishi bungeni kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) chini ya ufadhili wa chama hicho, katika awamu ya kwanza ulihusisha kata za Msangamkuu, Nanyamba, Ziwani na Mbembaleo na katika sasa awamu ya pili utakuwa katika kata za Mkunwa, Tangazo, Mayanga na Madimbwa.
    Credit; Mpekuzi Blog

    Naibu Spika Achafua Hali ya Hewa Bungeni Baada ya Kumwita Mbunge BWEGE

    By: Unknown On: 23:45
  • Share The Gag

  • Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, jana alizua kizaazaa baada ya kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said Bungara kuwa ni bwege, akimtaka aache kuonyesha hali hiyo.

    Kwa mujibu wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford) la mwaka 2004, neno bwege linamaanisha “mtu mjinga, mpumbavu, bozi, fala gulagula”.

    Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege.

    Bila ya kuruhusiwa, mmoja alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”

    Hata hivyo, wabunge hao wa upinzani hawakushinikiza Dk Tulia kufuta kauliz yake, lakini baadaye wakiwa nje ya ukumbi waliponda kitendo hicho cha kiongozi huyo wa Bunge ambaye aligombea uspika kwa tiketi ya CCM kabla ya kujitoa na muda mfupi baadaye kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na hivyo kupata sifa ya kugombea nafasi hiyo ya naibu spika.

    Dk Ackson aliamsha tafrani hiyo saa 5:48 asubuhi baada ya Bungara, ambaye ni maarufu kwa jina la Bwege, kusimama bila kufuata kanuni za Bunge, kupinga maelezo ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye juu ya uamuzi wa Serikali kusitisha shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni nchini.

    “Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati mjadala ukianza kuwa mkali.

    Mjadala huo uliendelea bila ya wapinzani kuhamaki, lakini baada ya Nape kutoa taarifa akieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha studio za Bunge ulifanywa na Bunge la Kumi ambalo yeye hakuwamo, ndipo wapinzani walipokumbusha kauli hiyo ya naibu spika.

    “Bunge linaonyeshwa asubuhi na kurudiwa kuonyeshwa usiku na kuna wanahabari hapa Dodoma wana kamera zao na wanaripoti bunge hili. Tusitumie bunge hili kupotosha,” alisema Nape kabla ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kuingilia kati.

    Msigwa: Hii ni taarifa au hotuba? 
    Spika: Msigwa jifunze kusikiliza kwanza, unaipokea taarifa yake ama vipi?

    Msigwa: Taarifa yake naikataa kwa sababu anasema uongo. Leo na wewe umemuita mtu bwege. Kuna mtu kule Arusha alimuita Rais Magufuli bwege na akapelekwa mahakamani. Na wewe tutakupeleka mahakamani.

    Mkazi huyo wa Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani takribani wiki mbili zilizopita akikabiliwa na shtaka la kumuita Rais kuwa ni bwege.

    Msigwa alisema Bunge “nalo ni jipu” kwa kuwa haliwezi kuishauri Serikali kutokana na kufanya maamuzi bila ya kushirikisha makamishna wake, akitoa mfano wa chombo hicho kurejesha Sh6 bilioni serikalini ambazo zilibanwa kwenye matumizi yaliyoelezewa kuwa hayakuwa muhimu.

    Baada ya Msigwa kumaliza kuchangia, alifuatia mbunge wa viti maalumu (Chadema), Tunza Malapo ambaye aliungana kauli na Msigwa na kumponda Nape na uamuzi wa Serikali.

    Wakati Malapo akiendelea kuchangia, alisimama Khatibu kutoa taarifa.

    “Kwa taarifa yako wewe Malapo aliyelishauri Bunge kutorushwa live ni Nape vuvuzela,” alisema.

    “Kwani kuanzisha studio za Bunge maana yake ni Bunge kutorushwa moja kwa moja?”

    Wakizungumzia tukio hilo la asubuhi, mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa alisema Dk Tulia alighafilika wakati akitoa kauli hiyo baada ya kurushiwa maneno mara kwa mara na wabunge wa upinzani, tena bila kufuata kanuni na taratibu za kibunge.

    “Kwanza mtu mwenyewe (Bungara) huwa anapenda kuitwa bwege sasa kama ukiamua kumuita bwege utakuwa umekosea?” alihoji.

    Alisema mara nyingi huibuka mvutano bungeni kwa sababu baadhi ya wabunge hawataki kuzingatia kanuni za chombo hicho cha kutun ga sheria.

    Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Antony Komu alisema: “Kauli iliyotolewa na Naibu Spika inaonyesha wazi kuwa ni kiongozi anayekiuka misingi, taratibu na kanuni za Bunge. Tazama anatukana watu tu bila kujali jambo lolote, hii si sawa kabisa.”

    Alisema Bunge linapaswa kuongozwa kwa haki na si kama ilivyo sasa ambayo inawafanya wabunge wa CCM waonekane kuwa na haki zaidi ya upinzani.

    “Mfano (mbunge wa Tarime Vijijini-Chadema, John) Heche aliomba mwongozo akanyimwa ila Dk Kigwangalla akapewa,” alisema.

    Kwa takribani wiki moja Bunge lilikuwa limepoa kutokana na wabunge wa vyama vya upinzani kususia kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini jana walishiriki kwenye mjadala wa wizara ya Ofisi ya Rais na kurejesha uhai kwenye chombo hicho.

    Katika hoja zao jana, wabunge hao walijikita zaidi kuponda Serikali ya Awamu ya Tano kuwa inakiuka kanuni za utawala bora na kupinga uamuzi wake wa kusitisha matangazo ya Bunge, jambo lililomlazimu Nape kusimama mara kwa mara kutetea uamuzi wa Serikali, huku Dk Ackson akitoa ufafanuzi wa kanuni za Bunge.

    Mara zote ambazo Nape na Dk Ackson walikuwa wakitoa ufafanuzi wao, walizomewa na wabunge hao wa upinzani huku mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji akimfananisha Nape na “vuvuzela” kwa maelezo kuwa ndiye aliyeishauri Serikali kusitisha matangazo hayo. 
    Akichangia mjadala huo, Mchungaji Msigwa alisema utawala bora na unaozingatia sheria hauanzi na bajeti, bali huanza na utawala bora.

    “Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, dhana nzima ya utawala bora haionekani. Utawala bora ni kuongoza nchi kwa ufanisi, tija na kwa uwazi, uadilifu, uwajibikaji na ushirikishwaji wa watu kwa kufuata utawala wa sheria,” alisema.

    Alisema ni ajabu Ofisi ya Rais-Utawara Bora kuomba bajeti ya Sh800 bilioni wakati nchi haina utawala bora. Alirejea kauli ya kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuwa Serikali inaongozwa bila ya maamuzi yake kuwekwa kwenye Gazeti la Serikali.

    “Walikuwa wanafanya kazi kama sisi tu mawaziri vivuli wa upinzani.Wanatoa maagizo wakati hawapo kisheria. Huu si utawala bora,” alisema Mchungaji Msigwa.

    Alisema licha ya jambo hilo kubainika wazi Bunge lilikaa kimya huku akidai kuwa hata baadhi ya mawaziri walikuwa wanajua jambo hilo, na kwamba wanapokuwa nao katika mgahawa wa Bunge, wamekuwa wakiponda na kuukosoa utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli.

    “Mawaziri mnakuwa kama vinyonga. Kwenye chai mnasema ukweli, mkija bungeni mnakaa kimya.Huwa tunawarekodi na mkibisha tutataja mmoja mmoja humu ndani,“ alisema Msigwa huku akimtaja Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla kuwa ni mmoja wa mawaziri hao baada ya waziri huyo kusimama kuomba mwongozo, kupinga kauli ya mbunge huyo.

    Dk Kigwangalla alitumia kanuni 68 (7) na 63 (1) kuomba mwongozo, akimtaka Mchungaji Msigwa athibitishe kauli yake kwa kuwataja kwa majina mawaziri wanaopingana na uongozi wa Serikali.

    Dk Ackson naye alitoa ufafanuzi akinukuu kifungu cha 63 (1) (2), kinachomtaka mbunge kuthibitisha jambo analolisema hapohapo ama apewe muda na kwamba atatoa maelezo ya kuwataka Dk Kigwangalla na Mchungaji Msigwa kuwasilisha ushahidi wao.

    Msigwa: Mbona Kigwangalla unajihisi mwenye hatia? 
    Dk Ackson: Msigwa unaongea na kiti usibishane na mbunge.

    Msigwa: Mheshimiwa Spika wakati wa kuchangia tunakuwa na taarifa sio mwongozo ila nashangaa huyu (Dk Kigwangalla) kaomba mwongozo kapewa. Ila tunaendelea tu ila kiti bado kinayumba.

    Dk Ackson: Mbunge anaweza kukosea na wengi tu hukosea. Ametaja kanuni zinazohusu utaratibu naomba tusiendelee kujibizana.

    Akiendelea na mjadala huo Mchungaji Msigwa alisema Bunge la Tisa na la Kumi yaliendeshwa kwa uwazi mkubwa tofauti na Bunge la Kumi na Moja, kwamba hata utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne ulikuwa haubani demokrasia na kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.

    “Bunge ni mkutano wa wazi wa wananchi wote, lakini Serikali hii inaanza kuminya na kuweka siri. Huu si mkutano wa unyago, tunaongelea matumizi ya fedha za Watanzania,” alisema.

    “Serikali inayokandamiza uwazi ni Serikali iliyojaa uoga na inayoficha madudu. Mnasimama na kusema mnakusanya fedha za kuvunja rekodi sasa mnaficha nini kuwaonyesha Watanzania hiki mnachokifanya?”

    Huku akiipongeza Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mchungaji Msigwa alisema pamoja na udhaifu wake, ilikuwa haizuii watu kuzungumza na kusema ukweli.

    “Nyinyi mmekuja na ‘hapa kazi tu’, lakini hamtaki kukosolewa. Wakati tunamkosoa Kikwete wabunge wa CCM mlikaa kimya na kutuzomea, leo mnaufyata na inaonekana hata Dk Magufuli akidondosha kijiko, mtasimama na kupiga makofi kwa sababu ya uoga wenu,” alisema Mchungaji Msigwa na kuwataka wabunge kuhoji mambo kwa maslahi ya wananchi. 
    <a href='http://mpekuzihosting.com/ads/www/delivery/ck.php?n=a5fa0220&cb=INSERT_RANDOM_NUMBER_HERE' target='_blank'><img alt='' border='0' src='http://mpekuzihosting.com/ads/www/delivery/avw.php?zoneid=3&cb=INSERT_RANDOM_NUMBER_HERE&n=a5fa0220'/></a> ;
    ==

    Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

    Rais Magufuli amtumbua Mkurugenzi Mkuu TIC

    By: Unknown On: 23:41
  • Share The Gag

  • Rais Dk John Magufuli.

    RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Juliet Kairuki kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutochukua mshahara wake tangu alipoteuliwa mwaka 2013.
    Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, Dk Magufuli ametengua uteuzi huo rasmi kuanzia Aprili 24, mwaka huu. Profesa Mkenda alisema pamoja na mambo mengine, hatua hiyo imechukuliwa na Dk Magufuli baada ya kupata taarifa kuwa mkurugenzi huyo alikuwa hachukui mshahara wa serikali tangu alipoajiriwa, jambo lililozua maswali.

    Aidha, kwa mujibu wa Profesa Mkenda, endapo Kairuki atakuwa tayari kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Awamu ya Tano, atapangiwa kazi nyingine. Alisema kutokana na hatua hiyo, tayari mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya umeanza mara moja.
    “Wakati mchakato huo ukiendelea kwa sasa Clifford Tandali atakaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho,” alisisitiza Katibu Mkuu huyo. Kairuki anakuwa Mkurugenzi wa pili wa mashirika ya umma kutenguliwa uteuzi wake baada ya Rais Magufuli juzi kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Ally Simba.

    Kairuki ni mtaalamu wa Sheria na masuala ya ubia kati ya Serikali na wawekezaji, na aliteuliwa kushika wadhifa huo Aprili 12, 2013 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kutoka katika Chama cha Mabenki Afrika Kusini akiwa ni Meneja Mkuu wa Idara ya Benki na Huduma za Fedha.

    Chanzo habariLeo.

    DC Wa Kinondoni Ally Hapi Aanza Mapambano Dhidi Ya Watumishi Hewa, Abaini 89 Waliolipwa Zadi Ya Sh Bilioni 1.331

    By: Unknown On: 23:36
  • Share The Gag

  • Mkuu  wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema idadi ya watumishi hewa katika wilaya hiyo, imeongezeka hadi kufikia 89 wakiwa wamesababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja.

    Aidha, Hapi amebaini uwepo wa watumishi vivuli 81 katika kada ya ualimu na hivyo kutoa siku saba kwa maofisa utumishi wa wilaya hiyo, kuhakiki watumishi vivuli ili kubaini idadi yao na hasara waliyosababisha.

    Hapi aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, na kueleza kuwa awali wakati akiingia katika ofisi yake wiki iliyopita alikuta kuna watumishi hewa 34 waliokuwa wamesababisha hasara ya Sh milioni 512.

    Alisema baada ya kufanya uhakiki zaidi walibainika watumishi hewa wengine 55 walioisababishia serikali hasara ya Sh milioni 619 na hivyo kufanya jumla ya hasara kuwa Sh 1,131,754,081.

    “Bado uhakiki wa kina unaendelea ili kuhakikisha tunamaliza hili tatizo la watumishi hewa katika wilaya ya Kinondoni, awali walikuwa 34 lakini sasa wameongezeka 55 na kufikia 89,” alisema Hapi.

    Akifafanua kuhusu watumishi vivuli, Hapi alisema watumishi hao ni wale ambao walihamishwa bila kufuata taratibu na hivyo kuendelea kupokea mshahara wa kazi yake ya awali badala ya kazi yake mpya.

    Alisema walibaini kuwepo kwa walimu katika idara ya elimu ya msingi 42 ambao baada ya kufuatilia hawakuonekana katika shule yoyote ya wilaya hiyo.

    “Kwa hiyo hili nalo ni tatizo kuna walimu wengine wanapokea mshahara mkubwa, lakini mtu alishahamishwa lakini anaendelea kupokea mshahara wa zamani ambao haufanyii kazi,” alisema.

    Katika hatua nyingine, Hapi aliwataka wafanyabiashara ndogo ndogo walioko katika maeneo yasiyoruhusiwa kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa baada ya siku saba alizotoa kukamilika.

    Alisema agizo hilo alilitoa ikiwa ni sehemu ya kuweka Manispaa ya Kinondoni katika hali ya usafi ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya Rais John Magufuli ya usafi wa kudumu.
    ==

    Credit; Mpekuzi

    Mmarekani ahukumiwa kufungwa na kazi ngumu Korea

    By: Unknown On: 23:32
  • Share The Gag
  • Kim alipatikana na makosa ya kufanya ujasusi
    Raia wa Marekani amefungwa jela miaka 10 na kazi ngumu nchini Korea Kaskazini baada ya kupatikana na makosa ya kufanya ujasusi, shirika la habari la Uchina la Xinhua limeripoti.
    Kim Dong-chul, raia wa Marekani aliyezaliwa Korea Kusini, alikamatwa mwezi Oktoba mwaka jana.
    Kim aliwasilishwa kwa wanahabari mjini Pyongyang mwezi jana na akaoneshwa akikiri makosa, na kusema kwamba alilipwa na Korea Kusini kufanya ujasusi.
    Mwezi Machi, mwanafunzi mwingine Mmarekani alifungwa jela miaka 15 kwa kujaribu kuiba bango la propaganda.
    Alipatikana na makosa ya "uhalifu dhidi ya dola”.
    Kim amefungwa jela katika kipindi ambacho uhusiano baina ya Korea Kaskazini na Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi nyingine za Magharibi umedorora.

    Majuzi, Pyongyang imefanya msururu wa majaribio ya kurusha makombora baada ya kufanyia majaribio bomu ya nyuklia mwezi Januari, majaribio yote yakivunja vikwazo zilivyowekwa na UN.
    Pyongyang ilijaribu kurusha makombora mawili ya masafa ya wastani Alhamisi lakini yalilipuka na kuanguka baharini muda mfupi baada ya kurushwa.
    Hatua hiyo ilipelekea kuitishwa kwa mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
    Chanzo habariLeo.

    Mafuriko yaua watano, yaathiri 13,000 Morogoro

    By: Unknown On: 23:24
  • Share The Gag
  • Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Kebwe Steven Kebwe.

    WATU watano wamefariki dunia na wengine 13,933 kutoka kaya 3,095 wameathiriwa baada ya kutokea kwa mafuriko makubwa ya mvua zilizonyesha maeneo mbalimbali ya wilaya za Kilosa, Kilombero, Morogoro na Wilaya mpya ya Malinyi mkoani Morogoro.
    Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya awali ya mafuriko yaliyotokea mkoani humo kutokana na mvua zilizonyesha Aprili 23 na 24, mwaka huu.
    Dk Kebwe alisema mbali na kusababisha vifo vya watu watano, pia mvua hizo zimesababisha madhara makubwa kwa wananchi kwa kuharibu mali, mazao mashambani na miundombinu ya barabara na hivyo kusababisha maeneo mengi kutopitika.
    Alisema kutokana na mafuriko hayo, kaya 3,095 zenye wakazi 13,933 zimeathiriwa ikiwemo kubomoa jumla ya nyumba 315 na kuharibu mashamba hekta 12,073 kutoka katika wilaya za Kilosa, Kilombero, Morogoro na Malinyi.

    Alizitaja wilaya ambazo mafuriko ya mvua yalisababisha vifo ni Kilombero kwa watu watatu wakiwemo wanafunzi wawili wa shule za msingi waliokuwa wakivuka mto Lumemo na mmoja wakati akivuka mto eneo la Kisawasawa.
    Kwa wilaya ya Morogoro, watu wawili walifariki dunia Aprili 23, mwaka huu akiwemo mwanamume dereva wa gari la kukodishwa ambaye ni mkazi wa Ngerengere aliyezama alipokuwa akivuka mto Ngerengere.
    Mbali na huyo, pia mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 10 alizama maji kwenye mto Mvuha baada ya gema la mto kukatika. Mtoto huyo alikuwa amekaa pembezoni wakati mama yake akiosha vyombo karibu na mto huo.
    Dk Kebwe alitaja madhara mengine kutokana na mafuriko kwa wilaya hizo ni Kilosa katika vijiji vitano kaya 1,238 zenye idadi ya watu 4,765 zimekumbwa na athari za mafuriko ikiwamo kuharibu nyumba 1,120 na kubomoa 144.
    Halmashauri ya wilaya ya Morogoro, ilikumbwa na janga hilo Aprili 23, mwaka huu katika vijiji 14 kutoka kata za Serembala, Mvuha, Tununguo na Mkulazi ambako wakazi 8,795 walio katika kaya 1,759 waliathiriwa na mafuriko.

    Kwa wilaya ya Malinyi kutokana na mvua zilizoanza kunyesha Aprili 10 hadi 26, mwaka huu, zimeharibu vibaya barabara nyingi ikiwemo ya Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo kilometa 94.
    Pia alitaja athari nyingine zilizosababishwa na mafuriko hayo ni kufungwa kwa Shule ya Msingi Ngombo kuanzia Aprili 12, mwaka huu hadi sasa kutokana na kuzingirwa na maji. Dk Kebwe pia alisema katika wilaya hiyo, jumla ya hekta 6,000 za mpunga, mahindi na ufuta zimesombwa na maji katika vijiji vya Usangule, Ngoheranga na Biro.

    “Wilaya ya Ulanga, Gairo na Mvomero pamoja na kupata mafuriko, lakini hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza mpaka sasa,” alisema Dk Kebwe. Alisema Morogoro ni kati ya mikoa 10 iliyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuwa itakuwa na mvua nyingi katika kipindi hicho na kutokana na mafuriko hayo, hali ya barabara si ya kuridhisha katika maeneo mengi baada ya kuharibiwa na mvua.

    Aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia kwa kutoa vyakula na misaada mingine ya kibinadamu kwa ajili ya kuwapatia wale walioathiriwa wakiwemo na wananchi wenye mapenzi mema. Alisema tayari Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kutoa dawa za kutosha kukabili magonjwa ya mlipuko.

    Chanzo HabariLeo.


    Marekani yaitaka Urusi kushinikiza Syria

    By: Unknown On: 23:20
  • Share The Gag
  • Marekani imeitaka Urusi kuishinikiza Syria kusitisha kuvamia raia na badala yake kuzingatia makubaliano ya kusitisha mapigano.
    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ametoa kauli hiyo baada ya hospitali moja iliyopo kwenye eneo la waasi kushambuliwa kwa ndege huko mjini Allepo, ambapo madaktari na watoto wameuawa.
    Amesema Marekani imeshtushwa na shambulizi hilo ambalo limefanywa kwa kukusudiwa.
    Zaidi ya watu sitini wameuawa mjini Aleppo lakini kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita katika maeneo yanayohodhiwa na serikali pamoja na waasi.

    Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesema hali ni ya kusikitisha.
    Msemaji wa ikulu ya Marekani Josh Earnest amezungumzia kuongezeka kwa vurugu hizo.
    '' Tunalaani vikali wimbo jipya la mashambulizi ya anga ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu sitini katika mji wa Aleppo katika kipindi cha saa ishirini na nne pekee.
    Tumeshangazwa zaidi na shambulizi la anga lilipofanywa katika hospitali iliyopo mjini Aleppo ambalo limeuwa takriban wagonjwa kumi na nne na madaktari watatu- akiwemo pamoja na daktari pekee wa watoto katika mji huo''.

    Maeneo ya mji wa Aleppo yamekabiliwa na mashambulizi mapya kutoka serikalini.
    Wanaharakati wametoa picha za video zinazoonyesha waokoaji wanavyotafuta watu waliosalimika katika tukio hilo.

    Chanzo HabariLeo.

    Serikali Yashauriwa Kuwa na Hisa Kwenye Kampuni za Madini ili Kujua Mapato halisi Yanayoingizwa na Wawekezaji wa Kigen

    By: Unknown On: 23:14
  • Share The Gag
  • Serikali imeshauriwa kuwa na sehemu ya umiliki katika kampuni zinazochimba madini na gesi ili kujua mapato halisi yanayoingizwa na wawekezaji wa kigeni. 
    Aidha, imeshauriwa kuzilazimisha kampuni hizo kurejesha nchini asilimia 60 ya mauzo yake, ili kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, pamoja na kuimarisha Shilingi ya Tanzania.

    Ushauri huo ulitolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyestaafu, Ludovick Utouh pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji wa Uwazi katika mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (EITI), Jaji mstaafu Mark Bomani, wakati wa uzinduzi wa ripoti za kamati za mwaka 2013 na 2014 uliofanyika jana Dar es Salaam.

    Akizindua ripoti hizo, Utouh alisema, Tanzania haijafaidika na rasilimali za madini, jambo lililosababishwa na kujiondoa kufanya biashara, hivyo kuzipa mwanya kampuni za kigeni kuendesha biashara bila uwazi kuhusu mapato zinazoyapata kutokana na mauzo ya madini.

    “ Serikali iliangalie jambo hili na kulirekebisha, Serikali ya Botswana ina hisa kwenye migodi hiyo, hivyo wanakuwa na mwakilishi kwenye bodi jambo ambalo linakuwa rahisi kufuatilia mapato yanayopatikana, lakini sisi hapa tulijiondoa kwa madai kuwa Serikali haifanyi tena biashara,” alisema Utouh.

    Alisema, Serikali ikifanya hivyo itaweza kupata mapato mengi zaidi kuliko ilivyo sasa, ambapo imejiondoa kabisa katika umiliki wa migodi ilhali rasilimali hizo ni za Watanzania.
     “Wawekezaji wanakuja na fedha na utaalamu, lakini sisi cha kwetu ni rasilimali, ni lazima tugawane nao na tuwe na mwakilishi kwenye bodi, badala ya kusubiri mrabaha unaotokana na faida anayopata mwekezaji. Huu utaratibu wa kuwaachia kila kitu sio mzuri,” alisema Utouh.

    Naye Jaji Bomani alisema, Serikali inatakiwa kuzilazimisha kampuni zinazochimba madini nchini kurejesha asilimia 60 ya mauzo yake ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni. Alisema, kwa kufanya hivyo, Shilingi ya Tanzania itaimarika.

    Alisema, hatua hiyo ikichukuliwa, sekta ya madini itakuwa imetoa mchango wake kwa pato la Serikali, licha ya kuwepo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo. 
    Alitaja moja ya changamoto hizo kuwa ni kupanua wigo wa wachimba madini kama vile wachimbaji wa kati na ambao pato lao linazidi Sh milioni 200, kwa mwaka ambao, alisema wanastahili kutoa mchango kwa pato la Serikali.

    Alisema mpaka sasa ni kampuni kubwa tu zinahusika, lakini akasema umefika wakati wachimbaji wa kati nao waingizwe kwenye utaratibu huo. 
    Alipendekeza kuwa umefika wakati sekta ya madini ipanuliwe hadi kwenye uchimbaji wa makaa kuiwezesha nchi kufaidika zaidi na shughuli za rasilimali hiyo, ambayo inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa nchi.

    EITI ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa mwaka 2002 na nchi mbalimbali zenye sekta ya madini. Linafanya ufuatiliaji juu ya sekta ya madini na gesi na kuona kama kuna uwazi katika biashara yake.

    Tanzania ilijiunga na shirika hilo mwaka 2009. Kazi kubwa ya kamati iliyoundwa kushughulikia shughuli hizo hapa nchini ilikuwa ni kukusanya taarifa juu ya malipo ambayo kampuni za madini zilikuwa zinalipa serikali ya Tanzania na kuzilinganisha na mapato ambayo yalikuwa yamepokelewa serikalini na kutoa taarifa kila mwaka.
    Credit; Mpekuzi Blog 

    Spika apangua tena Kamati za Bunge

    By: Unknown On: 23:11
  • Share The Gag

  • Spika wa Bunge, Job Ndugai. 
    SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amepangua tena Kamati za Kudumu za Bunge huku akiagiza Ofisi ya Katibu wa Bunge kuratibu uchaguzi wa kamati sita. Kwa mujibu wa Waraka Na 04/2016 wa Mabadiliko ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge uliotolewa jana hapa, Spika pia amefanya mabadiliko ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge.

    Spika Ndugai alisema Ibara ya 96 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imelipa uhalali Bunge kuunda Kamati za Bunge za namna mbalimbali kadri itakavyoona inafaa kwa ajili ya utekelezaji bora wa madaraka yake.

    Alisema pia kwa mamlaka aliyopewa chini ya Kanuni ya 116 (3) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili 2016, amelazimika kufanya mabadiliko ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge.
    Spika alisema sababu kubwa iliyomfanya kufanya mabadiliko hayo ni kuhakikisha kuwa kila mbunge ikiwa ni pamoja na wabunge wanne wapya walioapishwa Aprili 19, anakuwa mjumbe kwenye kamati mojawapo ya Bunge.
    Alisema aidha mabadiliko hayo ni kwa ajili ya kuhakikisha pia kuwa kwa kadri inavyowezekana, muundo wa Kamati za Kuduma za Bunge unazingatia aina za wabunge (jinsia, pande za Muungano na vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni), ujuzi maalumu, idadi ya wajumbe kwa kila kamati na matakwa ya wabunge wenyewe.

    Aliwataja wabunge walioapishwa kuwa ni Shamsi Vuai Nahodha na wabunge wa Viti Maalumu, Ritha Kabati (CCM), Oliver Semuguruka (CCM) na Lucy Owenya (Chadema). Wabunge waliobadilishwa ni Neema Mgaya kutoka Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwenda Huduma na Maendeleo ya Jamii, Bernadeta Mushashu kutoka Ardhi, Maliasili na Utalii kwenda Huduma na Maendeleo ya Jamii na Kunti Majala kutoka Ardhi, Maliasili na Utalii kwenda Kilimo, Mifugo na Maji.
    Wengine ni Ussi Salum Pondeza kutoka Nishati na Madini kwenda Katiba na Sheria, Richard Ndassa kutoka Katiba na Sheria kwenda Ardhi, Maliasili na Mazingira, Sebastian Kapufi kutoka Utawala na Serikali za Mitaa kwenda Ardhi, Maliasili na Utalii.

    Mabadiliko hayo pia yanawahusu Atupele Mwakibete kutoka Sheria Ndogo kwenda Ardhi, Maliasili na Utalii, Omar Kigoda kutoka Miundombinu kwenda Ardhi, Maliasili na Utalii, Dk Godwin Mollel kutoka Katiba na Sheria kwenda Ardhi, Maliasili na Utalii, Dk Raphael Chegeni kutoka Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwenda Viwanda, Biashara na Mazingira, Ibrahim Hassanali Raza kutoka Utawala na Serikali za Mitaa kwenda Viwanda, Biashara na Mazingira na Abdulaziz Abood kutoka Hesabu za Serikali za Mitaa kwenda Viwanda, Biashara na Mazingira.

    Wengine ni Emmanuel John kutoka Utawala na Serikali za Mitaa kwenda Kilimo, Mifugo na Maji, Jacqueline Msongozi kutoka Huduma na Maendeleo ya Jamii kwenda Hesabu za Serikali za Mitaa, Josephine Genzabuke aliyetoka Huduma na Maendeleo ya Jamii kwenda Hesabu za Serikali na Suleiman Sadick kutoka Huduma za Maendeleo ya Jamii kwenda Viwanda, Biashara na Mazingira.
    Kwa upande wa wabunge walioapishwa na kupangiwa kamati ni Nahodha aliyepangiwa Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Owenya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kabati Miundombinu na Semuguruka Kilimo, Mifugo na Maji.

    Chanzo habariLeo.

    Facebook yapata faida kubwa

    By: Unknown On: 00:20
  • Share The Gag
  • Facebook yapata faida kubwa
    Facebook imeripoti ongezeko la faida kwa asilimia 195 katika robo ya kwanza ya mwaka huku kampuni hiyo ikiendelea kupata mapato ya matangazo mapya.
    IIiripoti mapato ya dola bilioni 1.5 katika kipindi cha kati ya mwezi Januari na Machi ikilinganishwa na mapato ya dola milioni 512 mwaka uliopita.
    Mbali na kuwapatia wenye matangazo huduma mpya kama vile video, Facebook iliimarisha mauzo yake kutokana na huduma zilizopo.
    Facebook pia imependekeza mpango mpya wa hisa ambao utampatia fursa mwanzilishi wake Mark Zuckerberg kuuza hisa zake bila kupoteza udhibiti wa kampuni hiyo.
    Mark Zuckerberg Kampuni hiyo imesema kwamba hatua hiyo itampa moyo bwana Zuckerberg kusalia katika uongozi wa facebook.
    Thamani ya hisa za facebook ilipanda hadi asilimia 9 baada ya kufanya biashara.

    Chanzo Habarileo.

    Kipindupindu chaua watu 45 Zanzibar

    By: Unknown On: 00:14
  • Share The Gag
  • Visiwa vya Zanzibar ni maarufu sana kwa utalii
    Watu zaidi ya 45 wamefariki kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu visiwani Zanzibar katika kipindi cha miezi miwili, shirika la habari la AP limeripoti.
    Shirika hilo la habari limemnukuu afisa wa afya visiwani humo anayesema vifo hivyo vimetokea mwezi Machin a Aprili.
    Muhammed Dahoma, ambaye ni mkurugenzi wa anayeangazia kuzuia maradhi katika wizara ya afya, anasema watu karibu 3,000 wamelazwa hospitalini baada ya kuugua.
    Ameongeza kuwa serikali ya Zanzibar imechukua hatua kukabiliana na mlipuko huo.
    Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kupiga marufuku uuzaji wa chakula na juisi maeneo ya wazi.
    Taarifa kutoka visiwani humo zinasema serikali pia imeamuru kufungwa kwa shule zote kwa muda usiojulikana.
    Waziri wa elimu Riziki Pembe Juma, amenukuliwa na shirika la habari la Uchina la Xinhua, akisema uamuzi huo umetolewa baada ya kubainika kwamba wanafunzi ni miongoni mwa watu walioathiriwa zaidi na ugonjwa huo.
    “Tumejaribu kudhibiti hali, lakini kwa maslahi ya watoto wetu, watakuwa salama zaidi wakisalia nyumbani,” amesema kupitia taarifa, kwa mujibu wa Xinhua.
    Ameongeza kuwa baadhi ya shule zimeathirika zaidi kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
    Kisiwa cha Unguja ndicho kilichoathirika zaidi ambapo watu 20 wamefariki na 400 kuambukiwa tangu Januari mwaka huu.
    Waziri wa afya Mahmoud Thabit Kombo aliambia gazeti la serikali la Daily News wiki jana kwamba ikizingatiwa kwamba Zanzibar ni visiwa vidogo na watu si wengi sana “kipindupindu sasa ni tishio kubwa”.
    Mlipuko wa kipindupindu ulianza mwaka jana.
    Kufikia Oktoba, visa 140 vya maambukizi vilikuwa vimeripotiwa katika visiwa hivyo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

    Chanzo BBC swahili.

    Wednesday, 27 April 2016

    Watakaolipa mishahara HEWA kuburuzwa Mahakamani

    By: Unknown On: 22:49
  • Share The Gag
  • Serikali imesema vigogo wa juu katika utumishi wa umma, watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha ulipaji wa mishahara hewa, watafunguliwa kesi ya jinai.

    Aidha, imesema ifikapo Julai mosi, mwaka huu Halmashauri zote nchini ziwe zimefunga na kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato yake ya ndani na zimetakiwa kusitisha ukusanyaji kwa njia ya mawakala.

    Katika hatua nyingine imesema hadi kufikia Machi, 2016, watumishi 90 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na wengine kufikishwa mahakamani kwa kukiuka taratibu na sheria za kazi wakiwemo wakurugenzi watendaji (DED) wa halmashauri watano ambao wamevuliwa madaraka.

    Hayo yalisemwa kwa wakati tofauti na mawaziri wawili katika Ofisi ya Rais, walipowasilisha hotuba za bajeti kwa ofisi zao kwa mwaka ujao wa fedha bungeni mjini Dodoma jana. 
    Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki akiwasilisha hotuba ya ofisi hiyo, alisema kuanzia sasa kiongozi wa serikali wakiwemo wa ngazi za juu watakaobainika kuhusika kwa njia moja au nyingine katika kufanikisha ulipaji wa mishahara hewa watafunguliwa kesi za jinai.

    Waziri huyo alisema uchumi imara na endelevu katika nchi yoyote unahitaji uwepo wa utumishi wa umma uliotukuka unaozingatia utawala bora, utawala wa sheria, maadili na mifumo thabiti ya usimamizi na utekelezaji.

    Alisema mipango na bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa ofisi hiyo imezingatia dhamana hiyo ambayo imebeba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuleta mabadiliko makubwa katika utumishi wa umma kwa kuimarisha uwajibikaji na uadilifu.

    Alisema utekelezaji wa dhamira hiyo utasaidia kujenga utumishi wa umma uliotukuka kwa kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka, kuondokana na ukiukwaji wa maadili ya uongozi na utumishi wa umma, kuondokana na ucheleweshaji wa maamuzi, kutosimamiwa kwa uwazi na kutowajibika kwa viongozi na watumishi.

    “Ni lazima tuwe na viongozi wa umma wanaozingatia maadili yao ya kazi na ndio maana tunasisitiza kuwa viongozi wote watakaobainika kuhusika na ulipaji au kusaidia kulipa watumishi hewa mishahara, tutawafungulia kesi za jinai,” alisema Kairuki.

    Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene akiwasilisha hotuba ya bajeti yake, alisema katika mwaka wa fedha unaomalizika, watumishi 78 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa walichukuliwa hatua za kinidhamu na kijinai.

    Alisema kati ya watumishi hao, ma-DED watano wamevuliwa madaraka na kupangiwa kazi nyingine na wakurugenzi watatu wamefunguliwa kesi mahakamani na kesi hizo bado zinaendelea.
    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Madiwani wa Chadema Wilayani Hai Wasusa Kuhudhuria Kikao cha Mkuu wa Mkoa Said Meck Sadiki

    By: Unknown On: 22:42
  • Share The Gag
  • Madiwani  wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Helga Mchomvu, wamesusa kuhudhuria kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki wakati akizungumza na viongozi wa vitongoji, vijiji, kata, viongozi wa taasisi za serikali na dini.

    Sadiki alifika wilayani Hai jana, ikiwa ni moja ya ziara zake katika wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kuzungumza na viongozi mbalimbali wanaowakilisha wananchi, pamoja na kusikiliza kero zinazozikabili wilaya hizo.

    Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Usharika wa Hai Mjini, madiwani hao ambao wote ni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hawakuonekana hata mmoja huku eneo walilokuwa wameandaliwa likibaki na viti vilivyo wazi.

    Awali, Mkuu wa Mkoa alipowasili ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kwa lengo la kupokea taarifa ya wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mchomvu aliwasili kwa kuchelewa na muda ulipofika wa kuelekea ukumbini, alitokomea kusikojulikana.

    Hali hiyo ilimshangaza Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa ambaye alisema siasa ziliisha baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, lakini inashangaza kwenye masuala ya maendeleo ya wananchi bado viongozi wanaendelea kuziendekeza.

    Byakanwa alisema, licha ya madiwani wote 17 wanaounda Baraza la Madiwani Wilaya ya Hai kuwa ni wa Chadema, bado wanasimamia na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho chama kilichopewa ridhaa na Watanzania kuongoza kwa awamu nyingine ya tano.

    “Ni jambo la kushangaza kuona viongozi waliochaguliwa na wananchi wanashindwa kuwakilisha wananchi wao katika kupeleka na kuzisemea kero zao mbalimbali zinazowakabili, na badala yake wamekuwa wakisusa vikao vya kupanga maendeleo. Kwa siasa hizi wananchi hawawezi kupata maendeleo,” alisema Byakanwa.

    Akiwasilisha taarifa za kutofika kwa madiwani hao, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Hai, Rosemary Kuringe alisema, amewasiliana na madiwani wake na kuelezwa kuwa hawakupata taarifa za ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa.

    Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na viongozi mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Saidi Mderu alikiri kutoa taarifa kwa madiwani wote katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani kilichofanyika Aprili 22, mwaka huu.

    “Kwa suala hili la viongozi hawa kususa, namwachia Mungu, niliwapa taarifa madiwani wote tena nilisisitiza, cha kushangaza wakati Mkuu wa Mkoa amewasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri alifika akiwa amechelewa lakini wakati tumekuja kwenye ukumbi hatukumuona,” alisema Mderu.
    Mkuu wa Wilaya ya Hai ,Gelasius Byakanwa akizungumza katika kikao hicho.
    Mkurugenzi wa Halmshauri ya wilaya ya Hai,Said Mderu akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa katika kikao hicho.
    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Bandari Ya Dar es Salaam Kuunganisha Singapore Na Afrika Mashariki

    By: Unknown On: 22:37
  • Share The Gag

  • Waziri wa Biashara na Viwanda wa Singapore, Dk. Koh Poh Koon, amesema wamepanga kutumia bandari ya Dar es Salaam kuwa kiunganishi cha biashara kati ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

    Dk. Koon ameyasema hayo jana(Jumatano, Aprili 27, 2016), wakati alipomtembelea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma, na kwamba  Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kwenda kufanya kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa bandari za Tanzania.

    Dk. Koon ambaye ameambatana na wafanyabiashara wakubwa wapatao 40, amemweleza Waziri Mkuu kwamba kampuni ya Hyflux ya Singapore imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalum la uchumi (Special Economic Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda vya kati (light industries), maeneo ya biashara na nyumba za makazi zipatazo 37,000.

    “Jiwe la msingi la mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na Waziri wa Biashara,Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage,” alisema.

    Mbali na ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, Dk Koon amweleza Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia Tanzania kujenga uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na uendeshaji wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta.

    “Hadi sasa makampuni ya Singapore yaliyowekeza nchini ni pamoja na Pavillion Energy ambayo imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 1.2 katika sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant) kitakachojengwa mikoa ya Kusini kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka Ulaya na Marekani”.

    Amesema kampuni ya PIL ya Singapore inatarajia kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa makampuni ya gesi.

    Amesema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo pamoja na kuweka mikakati ya kuinua uchumi na kupanua wigo wa biashara.

    Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa ameishukuru Serikali ya Singapore kwa uwekezaji unaofanywa na makampuni yake nchini na kwa misaada ya kiufundi ambayo wameitoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.

    Ili kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi, Waziri Mkuu ameyakaribisha makampuni mengine ya Singapore kuja nchini kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na  kuanzisha viwanda, mahoteli, kilimo na nishati.

    Amemuahidi Dk. Koon kwamba Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini Mkataba wa Kuvutia na kulinda uwekezaji baina ya nchi mbili (Bilateral Investment Protection and Promotion Agreement) na Mkataba wa Kuepuka kutoza ushuru mara mbili (Double Taxation Avoidance Agreement) ili kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Singapore. 

    Waziri Mkuu, Majaliwa amewataka Watanzania kutumia fursa ya ushirikiano kati ya Singapore na Tanzania kuanzisha biashara mpya zitakazowanufaisha wote.

    Waziri Mkuu amesema Singapore ina uwezo mkubwa kibiashara pamoja na uzoefu wa siku nyingi kwenye uendeshaji wa bandari hivyo Tanzania itapata nafasi ya kujifunza namna ya uendeshaji katika sekta hizo.

    Amesema Tanzania imefungua milango ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Singapore kuja kuwekeza katika sekta za viwanda, usafiri wa anga na kwenye Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ).
    ==

      Credit;Mpekuzi Blog