Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
SERIKALI imetangaza kuboresha hospitali za rufaa, maalumu, za kanda
na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambayo sasa itaanza kutoa
huduma ya kupandikiza figo. Aidha, itajenga jengo maalumu la kulaza
viongozi wa kitaifa na watu mashuhuri.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alisema hayo bungeni mjini hapa jana alipokuwa akiwasilisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Alibainisha kuwa maboresho hayo kwa upande wa MNH ni pamoja na
kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu
(ICU) kutoka 21 hadi vitanda 75.
Pia itanunua vifaa tiba vya upasuaji na kuongeza vyumba vya upasuaji
kutoka 13 vya sasa hadi 18, itapanua huduma za kusafisha figo kwa
kuongeza vitanda kutoka 15 hadi vitanda 50 na kuanza kusafisha figo kwa
wagonjwa wenye Virusi Vya Ukimwi na virusi vya ini.
“Muhimbili itaanzisha huduma mpya ya upandikizaji figo na
upandikizaji wa ‘cochlea’ kwa wagonjwa ambao ni viziwi…itajenga jengo la
kisasa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa binafsi na viongozi wa
kitaifa na watu mashuhuri litakalokuwa na vitanda 170 na kuongeza mapato
kutoka shilingi bilioni 2.6 za sasa hadi shilingi bilioni tano kwa
mwezi,” alisema Ummy.
Alisema Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) katika mwaka wa fedha
2016/2017, itaongeza nafasi ya wagonjwa wanaolazwa kutoka vitanda 150
hadi 340 ambapo katika chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi
maalumu (ICU) vitaongezeka kutoka vinane hadi 32.
“Serikali itanunua mashine mpya za uchunguzi ikiwa ni pamoja na MRI,
CT scan na Xray za dijitali. MOI itatoa mafunzo na upasuaji wa marejeo
kwa nyonga na goti,” alifafanua.
Kwa upande wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo mwaka wa fedha
2015/2016 ilihudumia wagonjwa 24,570 wa nje na waliolazwa 2,134,
alisema katika mwaka ujao wa fedha wizara itaijengea uwezo taasisi hiyo
kwa kuweka vifaa ili chumba cha upasuaji cha tatu kianze kufanya kazi.
Waziri huyo alisema huduma za kibingwa za mkoba (outreach services)
zitatolewa katika hospitali za Temeke, Amana, Mwananyamala (zote za Dar
es Salaam), Tumbi mkoani Pwani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro.
Kwa upande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, alisema katika mwaka
wa fedha 2016/2017 itapatiwa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu
ikiwa ni pamoja na PET/CT scan, Linac na MRI.
Pia itatoa huduma za mkoba hasa katika maeneo yatakayoonekana kuwa na
idadi kubwa ya wagonjwa wenye saratani. “Wizara itaimarisha upatikanaji
wa dawa kwa wagonjwa wa saratani ambapo asilimia 13 ya fedha za dawa
zitatumika kununua dawa za saratani ili kupunguza mzigo kwa wagonjwa
hasa wa kipato cha chini,” alisema.
Kuhusu Hospitali ya Mirembe, alisema mafunzo yatatolewa kwa watumishi
ili kukidhi mahitaji ya kutoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya
na kwa Hospitali ya Bugando kutafungwa CT scan simulator kwa ajili ya
kupanga matibabu na mashine mbili za Varian & Elekta linac kwa ajili
ya matibabu ya saratani.
Hiyo itasaidia matibabu ya mionzi kutolewa Mwanza badala ya wagonjwa
kwenda Dar es Salaam. Ummy alisema katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC
itafungua wodi mpya za wagonjwa walioungua kwa moto na kemikali na
kuanzisha Kitengo cha ICU kwa ajili ya watoto na kununua vifaa vya
uchunguzi vya CT Scan, MRI pamoja na vifaa kwa ajili ya jengo jipya la
huduma za dharura.
Katika hatua nyingine, waziri amesema serikali imebaini vituo vya
afya 73 kati ya 5,235 vilivyopo nchini ndivyo vyenye hadhi ya kuwa vituo
vya afya. Waziri akizungumzia tathmini ya vituo vya afya 5,235, alisema
kati yake vituo 2,016 sawa na asilimia 38.51 vimepata nyota 0, vituo
2,583 vimepata nyota moja, vituo 561 vimepata nyota mbili.
Nyota hizo zote kuanzia sifuri hadi mbili maana yake havistahili kuwa
vituo vya afya. Ni vituo 68 vilivyopata nyota tatu na vituo vitano
vimepata nyota nne yaani ndiyo vyenye sifa ya kuwa vituo vya afya.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha asilimia 80 ya vituo
vilivyofanyiwa tathmini vinapata nyota tatu na zaidi ifikapo Juni mwaka
2018. Alisema wizara inaangalia uwezekano wa kurekebisha sheria ili
kufuta matangazo ya tiba asili na tiba mbadala.
Alisisitiza kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha matangazo
yote ya tiba asili na tiba mbadala yanayotolewa kwenye vyombo vya habari
yameidhinishwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Alisema Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Magonjwa wa Binadamu (NIMR)
kwa kushirikiana na kikundi cha kudhibiti Ukimwi Tanga (TAWG) itafanya
majaribio juu ya ubora na usalama wa dawa ya asili aina ya Tashack ya
tiba ya Ukimwi ambayo imeboreshwa na kutengenezwa kiwandani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu
utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo iliyoomba kuidhinishiwa Sh
845,112,920,056, Peter Serukamba ameomba serikali kufanyia uchunguzi
ongezeko la gharama kwa baadhi ya maeneo kwa zaidi ya mara 10 katika
ujenzi wa jengo la ghorofa saba la MOI kwa ajili ya kutolea huduma za
uchunguzi ikiwemo CT Scan, MRI, Xray, Ultra Sound, ICU, vyumba vya
wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu na vyumba vya wagonjwa wa
kulipia na kuchangia.
Jengo hilo lililokamilika kwa asilimia 95, litakapokamilika litatumia
Sh bilioni 27.23 ambazo ni mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF).
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 11 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment