Spika wa Bunge, Job Ndugai akifungua semina kwa wabunge. |
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema kuna fungu la fedha limetengwa na Bunge kwa ajili ya mafunzo ya wabunge katika makundi mbalimbali nje ya nchi, ili kubadilishana uzoefu na mabunge mengine.
Ndugai alisema hayo mjini Dodoma jana wakati wa Semina ya Wenyeviti wa Kamati za Bunge, iliyokuwa na lengo la kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati katika kutekeleza majukumu yao ya kikatiba kwa ufanisi zaidi.
Alisema pamoja na mkakati wa Bunge wa kubana matumizi, lakini inafika wakati inakuwa ni lazima wabunge katika makundi mbalimbali ikiwemo ya vijana, wanawake na kamati, kujifunza na kuona namna mabunge mengine ya nje yanavyofanya kazi.
“Agizo la Rais John Magufuli halikukataza safari za nje moja kwa moja ila lengo ni kupunguza safari kama ambavyo sisi tumefanya. Lakini inafika wakati mtu lazima aone wenzie wanafanya nini duniani, ni sehemu ya mafunzo ila kikubwa wasiwe wengi na isiwe kila wakati, tayari fungu hilo lipo,” alisema Ndugai.
Alisema mafunzo hayo yatakuwa ya wabunge wote lakini watakuwa wanakwenda kwa makundi kama, vijana, wanawake, pamoja na kamati za Bunge. Akizungumzia changamoto bungeni alisema uwepo wa wabunge wapya ni changamoto kubwa na kwamba wanakuwa kama wanaanza upya jambo aliloahidi kuendelea kufundishana taratibu.
“Uwepo wa wabunge wapya wengi ni changamoto kubwa bungeni ni kama tunaanza upya, kwa hiyo kuna kazi kubwa ya kuwekana sawa katika muda mfupi kuhakikisha kuwa wote wanakwenda vizuri” alisema.
Wabunge mbalimbali waliokuwepo katika semina hiyo walichangia mambo kadhaa ikiwemo adhabu kuwa ndogo kwa wabunge ambao wanavunja sheria na kuleta fujo bungeni ili iwe fundisho.
Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu (CCM), alisema malumbano na kashfa yanatokea bungeni kwa sasa sio mazuri, kiasi kwamba endapo Bunge lingekuwa linaoneshwa ‘live’, lingetia aibu.
Aidha alisema adhabu zinazotolewa kwa mbunge anayekosea ni ndogo, ndio maana hawajifunzi.
“Mtu anaona atafungiwa siku mbili au tatu na atakuwa huru,” alisema. Balozi Rajabu pia alizungumzia suala la Bunge kupitisha bajeti na kuiamini serikali, lakini inakuwa haitekelezwi ipasavyo kutokana na ukweli kuwa wizara hupatiwa fedha kidogo kuliko iliyopitishwa.
“Hili suala la sisi tunakaa na kupitisha bajeti, kama kipindi hiki halafu fedha hazipelekwi kwa wakati na wakati mwingine haziendi kabisa, sisi kama Bunge tunafanyaje? Serikali haina fedha nafasi yetu tuliopitisha bajeti ni ipi?’’ Alihoji Balozi Rajabu.
Chanzo Habarileo.
0 comments:
Post a Comment