Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
KAMPUNI 52 zimetuma maombi kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo juzi, alipozungumza na
Watanzania waishio Zambia katika mkutano uliofanyika ubalozi wa Tanzania
jijini Lusaka.
“Haya maombi yamekwishapokelewa na wenye makampuni wamekwishahojiwa,
kuangalia uwezo walionao katika suala zima la uwekezaji wanaotaka
kuufanya, na tukiwapata wenye uwezo na wenye nia ya dhati watapatiwa
miradi ya kuiendesha,” alisema.
Aliwataka watanzania hao waishio Zambia, watumie fursa ya uwepo wao
kutafuta marafiki ambao wanaweza kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali
nchini. Alisema serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu wakati
wananchi wanahitaji kupatiwa huduma muhimu.
“Serikali peke yake haiwezi kufanya kazi ya uwekezaji kwa hiyo
tunahitaji kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za kifedha na
washirika wa maendeleo na ndiyo maana kule kwenye mkutano nimewaeleza
washiriki kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi,” alisema.
Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika, kutawezesha wananchi wengi
zaidi kujiingiza katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuinua uchumi wa
nchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Alisema malengo ya Serikali ya awamu ya tano ni kuona kuwa nchi
inakuwa na mitambo mingi ya kuzalisha umeme na umeme wote unaozalishwa
na mitambo hiyo inaunganishwa na gridi ya taifa kuondokana na tatizo la
mgao wa umeme nchini.
Alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati vikiwemo gesi asilia,
makaa ya mawe, madini ya urani, maji, upepo, nishati ya joto kutoka
ardhini na nishati inayotokana na vinyesi vya mifugo, ambayo alisema
vinatumika kwa watu wachache (siyo kitaifa).
Alisema kupatikana kwa gesi asilia nchini kumeleta neema, ambapo
mabomba ya gesi yamekwishajengwa kutoka Mtwara hadi Kinyerezi na kutoka
Kilwa- Songosongo hadi Dar es Salaam. “Sasa hivi kuna utafiti unaendelea
juu ya uwezekano wa kusambaza gesi ya kupikia majumbani.
Tumeanza pale Mikocheni (DSM) na sasa hivi wanafanya utafiti mwingine
kule Mtwara ili wananchi waweze kutumia gesi hii kupikia badala ya
mkaa,” alisema. Akielezea kuhusu uwekezaji kwenye makaa ya mawe, Waziri
Mkuu alisema serikali imelenga kutumia makaa ya mawe ili kuendeshea
mitambo ya kwenye viwanda vikubwa, badala ya kutumia umeme au mafuta ya
dizeli kama inavyofanyika sasa.
“Baadhi ya wenye viwanda wanabadilisha mifumo ya kuendeshea mashine
zao ili iweze kuendana na teknolojia ya makaa ya mawe pindi tu uchimbaji
ukishika kasi,” alisema. Akifafanua kuhusu juhudi za serikali katika
kusambaza nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema tangu kuanzishwa kwa
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), vijiji zaidi ya 3,000, kati ya vijiji
12,000 vilivyopo nchini, vimefikiwa na nishati ya umeme.
“Tulianza na REA awamu ya kwanza, awamu ya pili na sasa tunaenda
awamu ya tatu. Hata mkipiga simu kwa ndugu zenu vijijini, mtakuta katika
kila kata kuna vijiji kati ya vinne hadi vitano ambavyo vimefikiwa na
nishati ya umeme kupitia mradi wa REA,” alisema. Waziri Mkuu alirejea
nchini jana.
Chanzo HabariLeo
Wednesday, 25 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment