Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watanzania waishio London,
Uingereza baada ya kumaliza mkutano nao kwenye ubalozi wa Tanzania
nchini humo, juzi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kuanza kazi kwa
kupambana na wala rushwa kurejesha umoja, ili rasilimali zilizopo
ziwanufaishe Watanzania wote.
Alisema katika mapambano hayo, wanalenga pia kushughulika na
waliosababisha uwapo wa watumishi hewa baada ya kumaliza kuwabaini
watumishi hao kote nchini.
“Jambo tuliloamua kuanza nalo ni kupambana na rushwa. Tumeamua
kufanya hivyo kurudisha umoja na maelewano miongoni mwa Watanzania,
tunataka tuibadili Tanzania iwe ni ya Watanzania wote… tumechoka
kuambiwa sehemu fulani mradi umekamilika halafu ukienda kuangalia hukuti
kitu na fedha ile haipo,” alisema na kushangiliwa na Watanzania waishio
Uingereza.
Majaliwa alizungumza na Watanzania hao juzi kwenye mkutano
uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini London, Uingereza. Waziri
Mkuu alikuwa nchini humo akimwakilisha Rais John Magufuli kwa mwaliko wa
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuhudhuria mkutano wa kujadili
namna ya kupambana na rushwa.
Alisema, Tanzania ina rasilimali nyingi na manufaa ya rasilimali hizo hayapaswi kuwa neema kwa wachache bali wananchi wote.
Akizungumzia suala la kusaka watumishi hewa, Majaliwa alisema Serikali itawashughulikia wale wote waliohusika katika hilo.
“Wafanyakazi hewa wamefikia zaidi ya 10,000 na tumeokoa zaidi ya Sh
bilioni 4.5 zilizokuwa zikipotea kila mwezi. Tukikamilisha kusaka
watumishi hewa, sasa tutataka kujua ni akina nani walikuwa wakipokea
fedha hizo. Waliohusika tutashughulika nao,” alisisitiza.
Alisema hivi sasa Serikali inalenga kuwa na watumishi wanaofanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na uwajibikaji mahali pa kazi.
“Hiki ndicho kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano na suala hili
litakuwa endelevu”, alisema Majaliwa. Uchumi na viwanda Akizungumzia
kuhusu ukuaji wa uchumi, Waziri Mkuu alisema, lengo la Serikali hivi
sasa ni kuona kuna ukuaji wa uchumi unaoenda sambamba na huduma
zinazotolewa kwa wananchi.
Majaliwa alisema, viwanda vingi viliuzwa na watu waliovinunua wakageuza kuwa ni maghala ya kufugia wanyama.
“Sisi tunataka vifufuliwe ili teknolojia mpya na za kisasa zije
Tanzania. Nafasi ya kuwekeza iko kwa Watanzania wote walioko nyumbani na
ninyi mlioko nje,” alisema.
Alisema, ardhi ipo ya kutosha na akawataka wawaalike marafiki zao
kuwekeza nchini, ili mradi wawe ni watu makini, wenye nia ya dhati ya
kuwekeza kwa mitaji na si madalali.
Alisema Serikali inataka usindikaji wa mazao na bidhaa ufanyike
nchini badala ya kupeleka mazao ghafi nje ya nchi. Alisema kwa njia hiyo
Tanzania itakuwa imezalisha ajira kwa wananchi wake.
“Kuna Watanzania wanaishi Botswana, Ujerumani na Poland wameshaleta
wawekezaji nchini. Kwa mfano wa Poland wameleta mradi wa umeme katika
vijiji vitano wilayani Ileje. Kwa hiyo ninyi endeleeni kuishi Uingereza
lakini mhakikishe kuwa ukaaji wenu hapa unaleta tija kule nyumbani.
Kumbukeni Tanzania na muwe tayari kuihudumia Tanzania,” alisema.
Bunge ‘Live’
Akijibu swali kuwa ana maoni gani juu ya Bunge kutorushwa ‘live’,
Majaliwa alisema, hatua hiyo ilichukuliwa ili kuwawezesha watu kufanya
kazi kama ambavyo kaulimbiu ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu inavyosema.
“Bunge la Tanzania lilikuwa ni pekee katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki na duniani ambalo lilikuwa likirushwa moja kwa moja kuanzia
asubuhi hadi usiku. Ina maana katika kipindi cha Bunge la bajeti, ambalo
linaendeshwa kila siku kwa miezi mitatu, Watanzania nao wangekuwa
‘Live’ kwa miezi mitatu,” alisema.
Alisema, walilazimika kujifunza kutoka kwenye mabunge mengine. “Hivi
hapa Uingereza mnaangalia Bunge ‘live’ kila siku?” Alihoji Waziri Mkuu
na kujibiwa kuwa linarushwa kwa kipindi kisichozidi dakika 15 wakati wa
maswali kwa Waziri Mkuu pekee.
Akitoa ufafanuzi, aliwaeleza kuwa Bunge la Tanzania linarusha ‘live’
kila siku asubuhi wakati wa maswali ya kawaida na Alhamisi asubuhi
wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu, lakini mijadala yote hurekodiwa na
kuhaririwa na kisha kurushwa kuanzia saa 8:00 hadi saa-9:00 mchana na
saa 3:00 hadi saa 4:00 usiku kwa siku husika.
Waziri Mahiga alonga Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga
alisema, kuitishwa kwa mkutano wa kupambana na rushwa nchini Uingereza
ni moja ya jitihada za Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuanzisha vuguvugu la
uanaharakati wa mapambano dhidi ya rushwa.
“Kukosekana kwa utawala bora, changamoto za ugaidi, biashara za dawa
za kulevya, biashara ya kusafirisha binadamu na uwepo wa rushwa na
ufisadi ni baadhi ya mambo yaliyofanya dunia ibadilike. Haya mambo
zamani yalikuwa hayana mahali pa kuzungumzwa, kwa hiyo vikao kama hivi
vitasaidia kukabili tatizo hili,” alisema Balozi Mahiga.
Alisema rushwa ni kama pweza mwenye vichwa vingi na mikia mingi.
Waziri Mkuu David Cameron ameamua kuanzisha jambo hilo kutafuta njia za
kukabili janga hilo kubwa.
“Sote tunatambua kuwa mataifa mengi yangependa kuwemo katika hii
‘movement’ lakini ni faraja kuona kwamba Tanzania imo miongoni mwa
waanzilishi na hii ni kwa sababu ya uongozi na ujasiri wa Rais Dk John
Magufuli ambaye kwa kweli ni ‘game changer’ (akimaanisha kuwa amebadili
mwelekeo wa Taifa hili) kwani ana utashi wa kisiasa na ana ujasiri wa
kukemea maovu,” alisema huku akishagiliwa.
Mkurugenzi Mkuu Takukuru Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola alisema,
vita ya rushwa nchini Tanzania ni endelevu na inafanyika kuitikia mwito
alioutoa Rais Magufuli wakati akizindua Bunge la Tanzania Novemba 20,
2015.
Alisema wanatumia mbinu mbalimbali kupambana na rushwa lakini kubwa
wanayoenda nayo hivi sasa ni kutoa elimu kwa watoto na vijana ili
kuwabadilisha tabia na utamaduni uliojikita kwenye jamii.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 15 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment